Mdahalo Wagombea Urais Marekani Watawaliwa Na Kejeli Na Vijembe

donald-trump-hillary-clinton-zoom-e55a3b65-f1ef-4ea3-a590-8586f4a4ada1Donald Trump na Hillary Clinton kabla ya kuanza kwa mdahalo huo.
NEW YORK , MAREKANI: Homa kubwa nchini Marekani kwasasa ni uchaguzi mkuu wa rais wa nchi hiyo unaotarajia kufanyika Novemba 4, 2016.
Homa hiyo inachangiwa kwa kiasi kikubwa na wagombea wa pande zote mbili, mwanamama Hillary Clinton wa Chama Cha Democratic na Donald Trump wa Chama Cha Republican ambao kura za maoni zinaonesha wanakabana koo kuwania nafasi hiyo muhimu.
Usiku wa kuamkia leo wagombea hao wamepambana vikali katika mdahalo wa kwanza wa televisheni ambapo wamepingana katika masuala mbali mbali ikiwemo masuala ya sera, kodi, ajira na uchumi.trump….Wagombea hao wakiwa kwenye mdahalo huo.
Vilevile wote wamezungumzia kuhusu Vita vya Iraq na juhudi za kukabiliana na kundi linalojiita Islamic State ambalo inadaiwa chimbuko lake kubwa ni kutokana na vita hivyo.
Msimamizi wa mdahalo huo, Lester Holt alimwuliza Donald Trump mbona hadi kufikia sasa bado hajaweka wazi taarifa zake za ulipaji kodi.
Mwanamama Hillary Clinton amemshutumu mpinzani wake akisema amekuwa akikwepa kulipa kodi na kudokeza kwamba hilo lina maana kwamba bwana Donald Trump hawezi kuwa na wanajeshi imara, pesa za kulipa wanajeshi waliostaafu pamoja na kufadhili elimu na huduma ya afya.
Lakini tajiri huyo kutoka New York amejibu kwa kusema kwamba atatoa hadharani taarifa hizo iwapo Bi Clinton naye atakubali kutoa barua pepe 33,000 ambazo zilifutwa kutoka kwa akaunti yake wakati wa uchunguzi kuhusu tuhuma kwamba alitumia barua pepe ya kibinafsi kwa kazi rasmi alipokuwa waziri wa mambo ya nje wa Marekani.
Bi Clinton amekubali lawama kuhusu kosa hilo na kusema hakuwezi kuwa na “kisingizio”.
Kadhalika, Donald Trump amemlaumu mpinzani huyo wake kuhusu kupotea kwa ajira akisema nafasi za kazi “zinaikimbia nchi” na akalaumu mikataba duni ya kibiashara.
Amesema Hillary Clinton amekuwa mtu wa “maneno mengi, bila vitendo”.
Bi Clinton ameahidi kuongeza uwekezaji na kuahidi kuunda nafasi takriban 10 milioni za kazi.
Mdahalo huo ulioandaliwa jijini New York huenda ukawa mdahala uliotazamwa na watu wengi zaidi katika historia ambapo watu 100 milioni inakadiriwa walitazama mdahalo huo.
Kura za maoni zinaonyesha wawili hao wanakaribiana sana katika uungwaji mkono.
Mambo mengine makuu yaliyoibuka kwenye madahalo:
Trump amesema hata jeshi linajua yeye anafaa kuwa Amiri Jeshi Mkuu, ISIS ni Wadukuzi na jeshi limemuidhinisha kuwa yeye ni mtu thabiti kuwa Amiri Jeshi Mkuu.
Bwana Trump pia amewashutumu Rais Obama na Hillary Clinton kwa kuweka nafasi katika nchi zenye migogoro kama Libya na Syria jambo lililoruhusu kumea kwa makundi kama ISIS na pia kuondoa majeshi mapema nchini Iraq ndiko kumepelekea kuimarika kwa ugaidi wa ISIS.
“Umekuwa ukikabiliana na ISIS maisha yako yote,” Bwana Trump amemkejeli Bi Clinton
Pia amemzungumzia Bi Clinton na kusema hana uwezo wa kudhibiti ukali wa kumuwezesha kuwa rais. Anadai mwanamama huyo ni mpole sana.
Trump amesema Wamarekani Weusi wanaishi “katika jehanamu” nchini Marekani, kwa sababu maisha yao yamekuwa hatari sana.
Akijibu kupigwa risasi kwa watu weusi, bwana Trump amesema suluhu ni kurejesha utawala wa sheria.
Bi Clinton amesema akichaguliwa kuwa rais atatekeleza mageuzi katika mfumo wa sheria kwa sababu “suala la asili limekuwa likiamua masuala  mengi ya muhimu”.
Hillary Clinton “Trump anajenga urafiki na viongozi wa mataifa wahasimu kama Russia, China na Iran na kwamba Rais Putin wa Russia ameruhusu mashambulizi ya mtandaoni kutoka Moscow.”
Pia mwanamama huyo amesema ana wasiwasi na urafiki wa Donald Trump na Vladmir Putin na kwamba Trump hafai kukaa White House.
Baada ya mdahalo kumalizika wagombea wote wamekubaliana kuheshimu matokeo.
Bado midahalo miwili itakayofanyika kabla ya uchaguzi mkuu wa Novemba 4, 2016.
Na Leonard Msigwa/GPL/MTANDAO.

Comments

Popular posts from this blog