Hatimaye Mtatiro ‘Amchana’ Prof. Lipumba, Amuita ni Jemedari Aliyekimbia Vita
Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi
ya CUF, Julius Mtatiro amesema aliyekuwa mwenyekiti wa chama hicho,
Profesa Ibrahim Lipumba amekiacha chama kwenye wakati mgumu baada ya
kujiuzulu wakati wa Uchaguzi Mkuu wa 2015.
Agosti, mwaka jana, Profesa Lipumba
alitangaza kujiuzulu nafasi hiyo na kukabidhi barua kwa uongozi baada ya
kushauriana kwa kipindi kirefu na viongozi na wazee wa chama hicho,
akisema nafsi yake inamsuta kwa kuwa walikiuka malengo ya Ukawa.
Hata hivyo, hivi karibuni Profesa
Lipumba aliandika barua ya kutengua uamuzi wa kujiuzulu na uchaguzi
ulipoitishwa ili kujaza nafasi hiyo hakuchukua fomu ya kugombea.
Akizungumza katika mahojiano maalumu,
Mtatiro amesema Profesa Lipumba amekitelekeza chama kikiwa katikati ya
uwanja wa mapambano.
Mtatiro aliyeteuliwa hivi karibuni na
Baraza Kuu la CUF kuongoza kamati ya uongozi wa chama hicho baada ya
kuvunjika kwa mkutano mkuu ulioitishwa kuziba nafasi ya mwenyekiti,
amesema walijaribu kila mbinu kumshauri Profesa Lipumba asijiuzulu bila
mafanikio.
“Tukamuuliza kama ni kujiuzulu kwa nini
usifanye baada ya uchaguzi? Kwa sababu wewe ndiye jemedari wa vita, wewe
ndiye uliyeleta mabadiliko, wewe ndiye mwenyekiti wa Ukawa, sasa leo
vita ndiyo inaanza umeshapeleka askari mstari wa mbele halafu unarudi
nyumbani. Askari kule mstari wa mbele unamwachia nani?” alisema na
kuongeza:
“Kwa hiyo Profesa Lipumba aliondoka na
alituacha katika wakati mgumu sana. Kwa sababu sasa unamwachia chama
Shaweji Mketo (Mkurugenzi wa Uchaguzi- CUF) aende kugawana majimbo na
kina Freeman Mbowe (Mwenyekiti wa Chadema), yule ni kijana, wale ni
wazee…”
Alisema Profesa Lipumba alipoondoka CUF,
heshima ya chama ilishuka kwa sababu hakukuwa na mtu mwenye uwezo wa
kujadiliana na viongozi wengine wa Ukawa na pia ilipoteza majimbo
waliyoyatarajia kuyapata katika uchaguzi.
Aliongeza kuwa CUF ingeweza kupata zaidi ya majimbo 25 kama Profesa Lipumba angekuwapo, lakini yalichukuliwa na vyama vingine.
“Kwa hiyo kupata majimbo 10 ilikuwa ni
kwa sababu ya kuondoka kwa Lipumba. Haya jemedari amekimbia vita,
amesusa kwa sababu ya Ukawa. Lakini tulitarajia aende kunadi wagombea
wake wa CUF, maana yeye ni mwanachama,” amesema Mtatiro.
CREDIT: MWANANCHI
Comments
Post a Comment