Deni La Bil. 7 Lamziba Mdomo Madam Rita.
DAR ES SALAAM: Habari zilizozagaa wiki iliyopita kuhusu Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuidai shilingi bilioni 7 Kampuni ya Benchmark Production inayomilikiwa na mjasiriamali, Ritha Paulsen ‘Madam Rita’, zimesababisha mwanamama huyo kuziba mdomo wake kwa kukataa kuzungumzia sakata hilo.
Gazeti hili lilimtafuta mdau huyo mkubwa wa burudani ambaye pia huendesha shindano la kila mwaka la Bongo Star Search (BSS) kutaka kusikia maoni yake kuhusiana na habari hizo zilizotikisa wiki iliyopita, lakini akawa na jibu fupi;
“No comment kwa sasa, nitatoa taarifa hivi karibuni juu ya jambo hilo, lakini siyo leo, muda muafaka ukifika nitafanya hivyo,” alisema Madam Rita.
Wiki iliyopita, TRA ilitoa muda wa siku 14 kwa kampuni hiyo kuwa imelipa deni hilo linalotajwa kuwa ni la kuanzia mwaka 2009, kupitia kwa meneja msaidizi wa madeni wa mamlaka hiyo, Mkoa wa Kodi wa Kinondoni, Sylever Rutagwelera aliyekuwa ameambatana na Kampuni ya Udalali ya Yono.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Kampuni ya Yono, Scholastica Kevela, alisema wameifungia kampuni hiyo na kuanzia sasa walinzi wa Yono watalinda na baada ya muda wa siku 14, waliopewa kulipa deni hilo ukipita, watachukua hatua nyingine kisheria ya kuuza mali za kampuni hiyo kwa mnada.
Alisema deni hilo ni kubwa kwa sababu ni muda mrefu umepita bila kodi ya serikali kulipwa na kuwashauri Watanzania kuacha tabia ya kulimbikiza kodi kwa sababu deni litakuwa kubwa ila likilipwa kwa wakati linaondoa usumbufu usio wa lazima.
“Yono tumepewa kazi ya kukusanya madeni ya serikali na tutaendelea kuwakamata wale wote tunaopewa kuwafuatilia, lengo sio kuwaumiza ni kuhakikisha kodi ya serikali inakombolewa kwa manufaa ya nchi yetu, kwa maana tunamuunga mkono Rais Dk John Magufuli kuhakikisha taifa letu linaendelea kwa kukusanya mapato stahiki,” alisema Kevela.
Comments
Post a Comment