Mwalimu aliyetuhumiwa kujihusisha kimapenzi na wanafunzi auawa
MWALIMU
Daniel Msalika (42) wa shule ya msingi Nyasosi, wilayani Bariadi, mkoa
wa Simiyu amefariki dunia katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando alikokuwa
amelazwa akitibiwa majeraha.
Majeraha hayo yalitokana na
kushambuliwa na baadhi ya wananchi kwa madai ya kujihusisha kimapenzi na
wanafunzi wa kike wa shule hiyo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Simiyu,
Onesmo Lyanga aliwaeleza waandishi wa habari jana ofisini kwake kuwa
mwalimu huyo alifariki dunia Julai 31 mwaka huu saa nane usiku.
Kamanda Lyanga alisema kuwa siku ya
tukio Julai 27 mwaka huu saa 6.30 usiku, wananchi hao ambao idadi yao
haijafahamika, walivamia nyumba ya mwalimu huyo baada ya kupata taarifa
kuwa kuna mwanafunzi ambaye amelala nyumbani kwake, jambo ambalo
halikuwa la kweli.
“Wananchi hao walipata taarifa ya
kuwa nyumbani kwa mwalimu kuna mwanafunzi ambaye amelala humo hivyo
walimvamia kwa kuvunja mlango na kuanza kumshambulia kwa kutumia silaha
mbalimbali za jadi na kumsababishia majeraha makubwa sehemu za kichwani
na usoni lakini binti waliyemkuta kwake ni mwenye umri wa miaka 18 na
siyo mwanafunzi,” alisema.
Alisema kuwa baada ya uvamizi huo,
mwalimu huyo alikimbizwa katika Kituo cha Afya cha Isanga kupatiwa
matibabu, lakini hali yake iliendelea kuwa mbaya na kupelekwa katika
Hospitali ya Rufaa ya Bugando jijini Mwanza, lakini alifariki dunia.
Kamanda alisema kifo chake, kimesababishwa na majeraha ya kushambuliwa huku tuhuma dhidi yake zikiwa si za kweli.
Alitoa mwito kwa wananchi kuacha
kujichukulia sheria mikononi huku wakisisitiza kuwa wote watakaobainika
kusababisha kifo hicho, sheria itachukua mkondo wake.
Comments
Post a Comment