Kingunge azua hofu
Na Mwandishi Wetu, RISASI Mchanganyiko
DAR ES SALAAM: Ukimya wa
mwanasiasa mkongwe nchini, Kingunge Ngombare Mwiru umezua hofu kubwa
baada ya kutoonekana katika matukio muhimu tangu alipojiondoa kutoka
Chama Cha Mapinduzi mwishoni mwa mwaka jana.
Kingunge alijiondoa ndani ya chama
tawala, muda mfupi baada ya kukatwa kwa jina la Waziri Mkuu wa zamani,
Edward Lowassa na kiongozi huyo kujiunga na Chama cha Demokrasia na
Maendeleo (Chadema) ambako alipewa fursa ya kuwania urais wa Tanzania,
akichuana na aliyeibuka mshindi, Dk John Pombe Magufuli.
“Huyu mzee yuko wapi jamani, maana yupo
kimya sana, wenzake wote tunawaona na kuwasikia, wengine wanarudi CCM,
wengine wanaonekana katika matukio, lakini yeye haonekani kabisa,
anatupa hofu kwa kweli,” alisema msomaji aliyejitambulisha kwa jina la
Giggs, akitokea mkoani Mtwara.
Msomaji mwingine, Samson Bilal wa
Tabora, alisema kimya cha mwanasiasa huyo huenda kikawa na mshindo mkuu,
kwani ukimya wake umekuwa siyo wa kawaida.
“Mzee Kingunge kwa kweli hasikiki
kabisa, tunawasikia wenzake aliohama nao akina Msindai, Lembeli, Ole
Madeye, Sumaye na hata Lowassa, lakini yeye yupo kimya,” alisema Samson.
Jitihada za gazeti hili kumsaka mkongwe
huyo wa siasa za Tanzania ziligonga mwamba, baada ya kufika nyumbani
kwake, Kijitonyama jijini Dar es Salaam na kushindwa kupata ushirikiano
kutoka kwa watu waliokutwa, ambao pia walikataa kujitambulisha.
Wakati wa mchakato wa kumtafuta mgombea
urais wa CCM mwaka 2015, mzee Kingunge alijipambanua wazi kuwa alikuwa
akimuunga mkono Edward Lowassa na alikasirika baada ya jina la mtu wake
huyo kukatwa, akisema hadharani kuwa taratibu zilikiukwa makusudi ili
kumpata mtu aliyeandaliwa na chama hicho.
Comments
Post a Comment