Askari wa Upelelezi Mwanza Auawa Club Akidai Laptop
Tarehe
21.08.2016 majira ya 10:00 usiku katika eneo la Club ya Villa Park
Resort Kata ya Kirumba Wilaya ya Ilemela Mkoa wa Mwanza, askari namba
g.5092 PC John Nyange wa Ofisi ya Mkuu wa Upelelezi na Makosa ya Jinai
Mkoa wa Mwanza (RCP), aliuawa kwa kuchomwa na kitu chenye ncha kali eneo
la shingoni na mtu aliyekuwa anaugomvi nae.
Inadaiwa kuwa marehemu alikua na
ugomvi wa muda mrefu na mtu aliyejulikana kwa jina Magina Hussein miaka
[27] fundi computer Msukuma na mkazi wa Mtaa wa Kigoto, ambapo marehemu
alikuwa akimdai Bwana Magina Hussein computer aina ya laptop. Ndipo
usiku wa leo majira tajwa hapo juu walikutana eneo la club ya Villa Park
huku mtuhumiwa wa mauaji hayo ikisemekana kuwa alikuwa na wenzake
watano ndipo walimvamia na kumchoma na kitu chenye ncha kali shingoni na
kufariki dunia njiani wakati akipelekwa hospitali.
Marehemu kwa sasa alikuwa ni
mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Stefano Moshi Memorial University College
cha Mjini Moshi, alikuwa anasomea Shahada ya Sayansi ya Habari na
Mawasiliano mwaka wa pili, aidha alirejea Mwanza baada ya kupata likizo
kuja kuiangalia familia yake ndipo umauti ukamkuta.
Watuhumiwa sita akiwepo Magina
Selemani ambaye alikuwa na ugomvi na marehemu pamoja na wenzake watano
wamekamatwa, wapo katika mahojiano na Jeshi la Polisi huku uchunguzi
kuhusiana na kifo hicho ukiwa bado unaendelea, pindi uchunguzi
ukikamilika watuhumiwa wote watafikishwa mahakamani, mwili wa marehemu
umehifadhiwa hospitali ya rufaa ya bugando kwa uchunguzi.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza Naibu
Kamishina wa Polisi Ahmed Msangi anatoa wito kwa wananchi wa Jiji na
Mkoa wa Mwanza, kwamba Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza limesikitishwa na
kifo cha askari huyu kwani limempoteza askari kijana ambaye bado jeshi
lilikuwa linamtegemea.
Lakini pia anawataka watu wenye tabia
za kujichukulia sheria mkononi kwa kuwapiga wengine hadi kufikia
kupoteza maisha kuwa wanafanya kosa la jinai, na kama watu wanadaiana
wafuate taratibu za kisheria zilizowekwa ili kuepusha vifo vinavyoweza
kuepukika, hivyo jeshi la polisi linawataka kuacha tabia hiyo mara moja
kwani hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.
Imetolewa na:
DCP: Ahmed Msangi
Kamanda wa Polisi (M) Mwanza
Comments
Post a Comment