Vigogo wote Wakala wa Misitu Tanzania (TFS) Watumbuliwa MAJIPU
SERIKALI
imemuondoa katika nafasi yake Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Misitu
Tanzania (TFS), Gerald Kamwenda na wakurugenzi wenzake, katika jitihada
za kufumua na kusuka upya shirika hilo.
Waziri
wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe, ametangaza hatua hiyo
ya serikali jana alipokutana na vyombo vya habari na kuongeza kuwa,
watumishi wengine 41 wamehamishwa vituo vya kazi.
Alifafanua
kuwa hatua hizo ni sehemu ya utekelezaji wa agizo la Waziri Mkuu,
Kassim Majaliwa, lililotaka kufumuliwa na kusukwa upya kwa TFS ili
kuongeza ufanisi.
Kutokana
na hatua hiyo, Waziri Maghembe alisema Profesa Dos Santos Silayo
ameteuliwa kuwa Kaimu Mtendaji Mkuu wa TFS, wakati Kamwenda anahamishiwa
Chuo cha Viwanda vya Misitu kilichopo Moshi.
Aidha,
Mwanaidi Kijazi aliyekuwa Mkurugenzi wa Usimamizi wa Raslimali za
Misitu na Nyuki, yeye amekwenda kuwa Mhifadhi Mkuu Amani Nature Reserve
na nafasi yake inachukuliwa na Zawadi Mbwambo.
Waziri
Maghembe alisema Mohamed Kilongo aliyesimamishwa kazi Januari 5, mwaka
huu uchunguzi umeonekana hana hatia na hivyo anaendelea kuwa Mkurugenzi
Mipango na Matumizi Endelevu ya Rasilimali za Misitu.
Alisema
Wizara imeamua Mkurugenzi wa Idara ya Misitu na Nyuki, Gladnes Mkamba
ahamishiwe Idara ya Mipango makao makuu na nafasi hiyo kuteuliwa Dk
Ezekiel Mwakalukwa, kuwa Kaimu Mkurugenzi.
Aidha
Monica Kagya aliyekuwa Kaimu Mkurugenzi Msaidizi wa Maendeleo ya
Ufugaji Nyuki, anakuwa Mtafiti Mwandamizi Idara ya Nyuki (Tawiri).
Alisema Kagya ni mtaalamu wa masuala ya nyuki, hivyo atahamishiwa
Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori, ili ashughulikie utafiti wa masuala
ya nyuki.
Pia
alisema katika Idara ya Wanyamapori, Profesa Alexander Songorwa anakuwa
Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori, nafasi ambayo ilikuwa
ikishikiliwa na Herman Kerayo ambaye anahamishiwa Idara ya Mipango Makao
Makuu.
Profesa
Ramadhan Kideghesho, yeye anakwenda kuwa Mkuu wa Chuo cha Mweka wakati
Mabula Misungwi aliyekuwa Meneja Mradi Selous, anakwenda Chuo cha
Wanyamapori Pasiansi na nafasi yake inachukuliwa na Jaffary Lyimo, huku
Robert Mande akipelekwa kuwa Kaimu Mkurugenzi msaidizi Uzuiaji Ujangili.
Waziri
Maghembe alisema Majjid Ally ameteuliwa kuwa Kaimu Mkuu wa Kitengo cha
Leseni, nafasi iliyokuwa ikishikiliwa na Haji Mpya ambaye amehamishiwa
Shamba Jipya Songea kuwa Ofisa Misitu Alisema Julai 18, mwaka huu Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa alikutana na viongozi na watumishi wa Wizara hiyo
na watendaji wakuu na watumishi wa TFS na kuagiza kufumuliwa na kusukwa
upya kwa wakala huo.
Katika
mkutano huo, Waziri Mkuu alitaka kuondolewa kwa utitiri wa vituo vya
ukaguzi na kuwekwa vituo vichache na kuondolewa kwa ofisi za makontena
yanayotumiwa na ofisi ya TFS, badala yake watumishi wanaofanya ukaguzi
wasimame mahali pa wazi ili kuondoa mianya ya rushwa na kuweka uwazi
katika utendaji.
Comments
Post a Comment