'Ni vizuri mwanaume, amfiche mkewe vipato vyake’
Ukipata bahati ya kukaa kwenye vijiwe vingi vya wanaume, kauli za ‘mwanamke usimueleze kila kitu’ huwa zinatawala. Wanaambizana kwamba ili uhusiano udumu, usimueleze kila kitu mwanamke. Wanasema mfiche asijue kila kitu.
Taswira hiyo imeanza kama utani lakini
pengine kadiri siku zilivyokuwa zinazidi kusonga mbele, sasa inakuwa
kama sheria. Wanaume wanasambaziana mbinu hiyo ili kukabiliana na
wanawake zao. Wanaona ni bora kuwaficha baadhi mambo ili mambo yaende
vizuri.
Mwanaume anaamini akimficha baadhi ya
vitu mkewe, inasaidia kumfanya aishi kwa amani. Hataki kumueleza kila
kitu kinachomhusu kwani anaamini uwezo wake wa kukabiliana na mambo
hauwezi kuwa sawa na yeye hivyo bora amfiche.
Hali hiyo haikuja hivihivi, imetokana na
visa mbalimbali wanavyokutana navyo katika uhusiano. Wanafikia hatua ya
kuwafananisha wanawake na watoto. Kwamba hata kama mwanaume hana fedha,
hapaswi kumueleza mwanamke kuwa hana fedha.
Kwamba mwanamke usimueleze vyanzo vyote
vya mapato maana ukimueleza ni tatizo. Lazima ataleta usumbufu. Atakuwa
wa kwanza kuhoji matumizi na kutaka kila kitu wapange wao.
Mwanaume asipokubaliana naye, anakuwa wa
kwanza kuleta chokochoko ambazo mwisho wa siku zinasababisha mtafaruku
ndani ya nyumba. Hapo ndipo wanaume wengi wanapopakwepa.
Wanakubali kuumia kimoyomoyo. Hamuelezi
hata siku moja ukweli kuhusu mapato yake. Hata kama hana kitu, mkewe au
mchumba wake akiomba fedha, anampa tu matumaini kwamba asiwe na wasiwasi
atampatia siku fulani hata kama hana uhakika wa kuzipata.
Utasikia: “usijali baby nitakupa kuwa mvumilivu.”
Tafsiri ya wanaume hao ni kwamba, hata
ukiwaeleza ukweli, wanawake wana kasumba ya kutoelewa. Wanaume wanaamini
kwamba wanawake wengi wanapenda matokeo chanya ya mambo yao bila kujua
ugumu au mazingira ambayo wanaume wanayapitia.
Hiyo ndiyo sababu ya wanaume wengi
hulazimika kuwaficha mishahara wake zao wakiamini wakijua ni tatizo.
Wanaamini kwamba watalazimisha matumizi hata yasiyo ya lazima kwa kuwa
wanajua mishahara ya mabwana zao.
Wanashindwa kuwaeleza kwa sababu
wanaamini wanawake hawana fikra ya kujua hatima ya kesho. Wanawazia
matumizi ya leo tu. Kwa ujumla, wanaume huamua kuficha vyanzo vyao ili
tu kuepusha ugomvi.
Wakati mwingine wanaamua kuficha baadhi
ya vyanzo ili mwanamke ‘atakapong’ang’ania’ matumizi ya baadhi ya vyanzo
anavyovijua, anajua vipo vya ziada ambavyo vitamfanya awe huru kutokana
na kutohojiwa matumizi yake.
NINI CHA KUFANYA?
Kama nilivyofundisha wiki iliyopita,
wawili ambao mna uhusiano ambao upo ‘serious’, hamna sababu ya
kufichana. Hapa nawazungumzia wale ambao wanaelekea kwenye ndoa au
tayari wapo kwenye ndoa. Nilisema wenye uhusiano wa aina hiyo, wanapaswa
kuondoa u-mimi.
Mnapaswa kutumia u-sisi. Kwamba nyinyi
sasa mnakuwa mwili mmoja hivyo hakuna sababu ya kufichana katika mambo
yenu. Muelezane ukweli hata kama ni mgumu. Hamna sababu ya kufichana
kwani nyinyi ni mwili mmoja.
Wanawake wanapaswa kukubaliana na
mazingira ya wanaume. Mtengenezee mazingira ya kumuelewa mumeo au
mchumba wako kwamba hata akikuambia hana kitu, hauwezi kuleta kelele.
Utamtia moyo hivyo wakati utapita.
Uchunguzi unaonesha wanaume wengi
hupenda kuwaficha wanawake wao kwa sababu tu, hawapendi malumbano.
Wanaamini wakiwaeleza ukweli wake zao kitakachofuata ni malumbano hivyo
ni bora kumficha baadhi ya mambo.
Japo inasaidia kudumisha lakini hakuna kitu kizuri kama kuambizana ukweli.
Tukutane wiki ijayo kwa mada nyingine nzuri.
Comments
Post a Comment