Mfanyabiashara Anayedaiwa Kujipatia Milioni 7 Kwa Dakika Afikishwa Mahakamani Na Kusomewa Mashitaka 199
Hatimaye mfanyabiashara aliyetajwa na Rais John Magufuli kuwa amekuwa
akiibia Serikali takriban Sh7 milioni kwa dakika, amepandishwa
kizimbani na wenzake wanne na kusomewa mashtaka 199, wote kwa pamoja.
Mfanyabiashara huyo, Mohamed Mustafa Yusufali na wenzake
Alloyscious Gonzaga Mandago, Isaac Wilfred Kasanga, Taherali Sujjauddin
Taherali na Mohamed Seif Kabla, walipandishwa kizimbani na kusomewa
mashtaka hayo jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
Washtakiwa wote kwa pamoja wanakabiliwa na mashtaka ya kughushi,
kuwasilisha nyaraka za uongo kwa mamlaka za Serikali, utakatishaji fedha
na kuisababishia Serikali hasara ya zaidi ya Sh15 bilioni.
Katika ya mashtaka hayo, Yusufali maarufu kwa majina ya Mohamedali,
Choma au Jamalii anakabiliwa na mashtaka 198 yeye peke yake huku
wenzake wakikabiliwa shtaka moja la utakatishaji fedha.
Kutokana na wingi wa mashtaka hayo, waendesha mashtaka wawili;
Wakili wa Serikali Mwandamizi, Shadrack Kimaro na Wakili wa Taasisi ya
Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Leonard Swai walilazimika
kubadilishana ili kuwapa muda wa kupumua.
Kutokana na kukabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi na shtaka la
kutakatisha fedha, washtakiwa hao hawakutakiwa kujibu lolote kwa sababu
mahakama hiyo haina uwezo wa kusikiliza kesi hiyo isipokuwa Mahakama Kuu
na kulingana na mashtaka yanayowakabili, hayana dhamana.
Baada ya kumaliza kuwasomewa mashtaka hayo, upande wa mashtaka uliieleza Mahakama kuwa upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika.
Hivyo, Hakimu Mkazi, Huruma Shahidi anayesikiliza kesi hiyo
aliamuru washtakiwa wapelekwe mahabusu hadi Julai 25, kesi hiyo
itakapotajwa tena.
Kabla ya kupandishwa kizimbani, Yusufali alitajwa na Rais Magufuli
kuwa ana mashine inayotoa risiti za kielektroniki (EFD) nje ya mfumo wa
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na kuzisambaza kwa wafanyabiashara
wengine, hivyo kujiingizia Sh7 milioni kwa dakika.
Rais Magufuli alieleza kuwa mtandao wake unawashirikisha watumishi
wa TRA na Wakala wa Usajili wa Kampuni (Brela), hivyo kuisababishia
Serikali hasara ya mabilioni ya shilingi.
Katika mashtaka hayo, Yusufali anakabiliwa na mashtaka 181 ya
kughushi, mashtaka 15 ya kuwasilisha nyaraka za uongo, udanganyifu
katika kulipa kodi moja, shtaka moja la kuisababishia Serikali hasara ya
Sh15,645,944,361, huku shtaka moja tu la utakatishaji fedha ndilo
likimhusisha na wenzake.
Waendesha mashtaka hao walidai kuwa mfanyabiashara huyo alikuwa
akighushi nyaraka za kampuni mbalimbali, kuonyesha kuwa zimesajiliwa na
zinaendesha shughuli zake nchini kihalali wakati akijua siyo kweli.
Pia, walidai kuwa mfanyabiashara huyo alikuwa akiwasilisha nyaraka za uongo TRA.
Kuhusu shtaka la kutakatisha fedha, upande wa mashtaka ulidai kuwa
washtakiwa hao kwa pamoja kati ya Machi 2011 na Januari 2016,
walitakatisha Sh1,895,88500 kwa kujifanya kuwa ni malipo ya mikopo
waliyoipokea kwa watu mbalimbali.
Upande wa mashtaka ulidai kuwa kati ya Januari 2008 na Januari
2016, mfanyabiashara huyo alifanya udanganyifu katika kuwasilisha kwa
Kamishna Mkuu wa TRA taarifa ya uongo ya marejesho ya mapato, hivyo
kuikosesha Serikali mapato ya kodi ya VAT zaidi ya Sh15.6 bilioni
Comments
Post a Comment