Licha ya Nay wa Mitego… TRA wamhenyesha Diamond siku 7
MUSA MATEJA, Amani
DAR ES SALAAM: Imevuja! Siku
chache baada ya Mbongo Fleva, Emanuel Elibariki ‘Nay wa Mitego’
kukamatwa na kuhojiwa na Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam
kuhusu chanzo cha utajiri wake wenye utata, mwenzake katika fani, Nasibu
Abdul ‘Diamond’ naye amekumbana na kimbembe cha kuchunguzwa na TRA,
Amani lina kitu mkononi.
TRA ni Mamlaka ya Mapato Tanzania ambayo
inajishughulisha na ukusanyaji wa kodi kwa wafanyabiashara na wananchi
kwa jumla ili kuiletea nchi maendeleo kutokana na pesa hizo za kodi.
Kwa mujibu wa chanzo, Diamond alikumbwa
na kimbembe hicho Juni, mwaka huu kabla ya Nay na kwamba, jamaa wa TRA
walimvamia nyumbani kwake, Madale na kutaka aorodheshe mali zake zote
ili ambazo hazijalipiwa kodi zijulikane.
“Jamani, mmeandika habari za Nay
kukamatwa na polisi na kuhojiwa kwa siku mbili kwa sababu ya utajiri
tata. Sasa mimi nawaambia ubuyu mwingine kwamba, Diamond naye alishikwa
na watu wa TRA, wakawa wanamhoji kuhusu mali zake zote.”
“Walianzia nyumbani kwake Madale,
wakaangalia uhalali wa nyumba yake na vitu vingine kama magari na vyote
ambavyo vinatakiwa kulipiwa kodi.”
“Baada ya kutoka Madale, walikwenda
kwenye nyumba aliyoifanyia ukarabati, ile ya Tandale (Dar). Kule nako
jamaa walifanya mahesabu yao, wanajua wenyewe walichokipata.”
“Baada ya Tandale, wakaona bado,
wakaenda kwenye studio yake (Wasafi Records) iliyopo Sinza Mori, Dar,
nako wakaangalia kila kitu kilichomo na uhalali wake kama havidaiwi
kodi.”
NYUMBA ALIYONUNUA
“Kama vile haitoshi, wakaenda kwenye ile
nyumba aliyonunua, iliyopo Salasala, Dar ambako pia waliipigia thamani
na kuangalia kama alilipia kodi kwenye manunuzi.”
ILICHUKUA SIKU SABA
“Afadhali ya Nay alihojiwa kwa siku
mbili, Diamond ni siku saba, sema tu yeye, jamaa wa TRA walikuwa
wanambana mchana kutwa na kumwachia jioni,” kilisema chanzo hicho.
DIAMOND ACHANGANYA AKILI
Chanzo hicho kilisema kuwa, mwisho wa
kumbana, Diamond aliambiwa anatakiwa alipie kodi kwa kila kitu ambacho
alikwepa kufanya hivyo.
“Lakini jamaa (Diamond), akachanganya
akili zake, akaamua kumtumia kigogo mmoja serikalini ambaye alimsaidia.
Kigogo huyo aliwaambia watu wa TRA wamuachie kwa sababu utaratibu
waliuharibu wenyewe tangu mwanzo kwa kuacha kukusanya mapato kwa uzembe.
Ndipo Diamond akaachiwa,” kilisema chanzo.
Nay wa Mitego.
‘KIAMA’ CHA MASTAA
Kwa mujibu wa chanzo hicho, kilichompata
Diamond na Nay ni mwendelezo wa kampeni ya serikali kuhakikisha mastaa
wote wanaotamba na utajiri, wanalipa kodi na pia utajiri wao uwe halali
huku wale wanaomiliki utajiri usio wa halali, wakitangaziwa mwisho wao
(kiama). Habari ya Nay iliandikwa Gazeti la Ijumaa Wikienda, Jumatatu
iliyopita.
DIAMOND MWENYEWE
Amani lilipomtafuta Diamond ambaye kwa
sasa yupo nje ya Bongo na kumuuliza kwa njia ya ujumbe mfupi wa
maandishi (meseji) kuhusu kuhenyeshwa huko, alibaki kucheka kwa kuandika
‘Teh! Teh!’ kisha akasema: “We acha tu, mambo mengine bwana!” (baada ya
hapo, hakujbu tena meseji).
Juzi, Amani lilimpigia simu Mkurugenzi wa Umma wa Elimu kwa Mlipa Kodi wa TRA, Richard Kayombo ili kumsikia anasemaje, lakini hakupokea.
Comments
Post a Comment