CHADEMA Wafungua kesi mahakama ya Afrika Mashariki dhidi ya Serikali

 Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) jana kimefungua rasmi kesi dhidi ya Serikali katika mahakama ya Afrika Mashariki kupinga zuio la kufanya mikutano ya hadhara ya kisiasa.

Naibu Katibu Mkuu wa Chadema (Bara), John Mnyika aliwaambia waandishi wa habari kuwa wameamua kufungua kesi hiyo kwakuwa tamko hilo la Serikali ni kinyume cha katiba na mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki pamoja na sheria ya vyama vya siasa.

Mnyika ambaye aliambatana na mwanasheria wa chama hicho, John Mallya alisema kuwa wamekusanya ushahidi wa kutosha wa matamko ya katazo la kufanyika mikutano ya kisiasa na namna chama hicho kilivyozuiwa kufanya mikutano hiyo sehemu mbalimbali nchini.

“Tumeleta vielelezo vya zuio lenyewe la polisi kama ushahidi wa kwamba ni kweli polisi wa Tanzania wametoa agizo kama hilo. Pili, tumeleta vielelezo vya mikutano iliyozuiwa… mikutano ya Kahama, Mahafali ya wanachuo wa Chadema kule Dodoma, Mahafali yaliyofanyika kule Moshi na mikutano mingine,” alisema Mnyika.

“Katiba na sheria zetu zingekuwa zinaruhusu kumburuza moja kwa moja mahakamani Rais Magufuli, basi leo mashtaka yangekuwa dhidi ya Magufuli. Lakini  mwanasheria wa Serikali anasimama kwa niaba ya Serikali,” aliongeza.

Naibu Katibu Mkuu huyo wa Chadema alisema kuwa mbali na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Wamemshtaki pia Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kwani analo jukumu la kusimamia mikataba ya Jumuiya hiyo.

Alisema kuwa kesi hiyo ni aibu kwa Serikali ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa kuzingatia kuwa Rais Magufuli ndiye mwenyekiti wa jumuiya hiyo kwa sasa.

Comments

Popular posts from this blog