Binti miaka 8 afanyiwa ukatili wa kutisha!
Mtoto Mariam aliyezibwa uso.
Na Issa Mnally, UWAZI
DAR ES SALAAM: Mtoto
aliyejulikana kwa jina moja la Mariam (10), mkazi wa Mavurunza ‘A’
Kimara King’ong’o, Dar yupo katika mateso makubwa kufuatia vitendo vya
ukatili na unyanyasaji anavyofanyiwa na mwanamke anayedaiwa kuwa ni mama
yake mzazi aitwaye Aisha.
Akionesha sehemu ya shingo alivyokwaruzwa kwa kucha.
Kwa mujibu wa majirani, mtoto huyo
ambaye hata mahudhurio yake shuleni si mazuri, amekuwa katika mateso
hayo ya kupigwa mpaka kujeruhiwa kwa muda mrefu lakini majirani walikuwa
wakishindwa jinsi ya kumnasua kuzingatia kuwa, anayedaiwa kufanya
vitendo hivyo ni mama yake.
Hivi
karibuni, majirani wa eneo hilo wakishirikiana na Mjumbe wa Shina Namba
063, Mavurunza ‘A’ Kwa Kichwa, Janet Moshi waliamua kumwokoa mtoto huyo
baada ya kufukuzwa nyumbani na mama yake huyo majira ya saa 4:30 usiku
bila kuwa na sehemu ya kwenda.
“Ilikuwa
saa nne na nusu usiku, sisi tulikuwa tumekaa kule mbele tukipata moja
moto, moja baridi (pombe) ndipo tukasikia kelele za mama wa mtoto
akimfokea bintiye huku akimpiga na kumfukuza atoke nyumbani kwake,”
alisema mama Mayunga mmoja wa akina mama walioamua kujitoa kumsaidia
mtoto huyo.
“Kila siku anampiga huyu mtoto. Unayaona
hayo majeraha? Yote yametokana na kipigo ambacho anakipata kutoka kwa
mama yake,” alisema mama Donata huku akimgeuzageuza mtoto huyo sehemu ya
shingo ili kuonesha majeraha hayo.
Kwa
mujibu wa mtoto mwenyewe, ambaye anaweza kujieleza kwa ufasaha,
anawashukuru mama Mayunga, mjumbe wa shina na mama Donata kwa kumtoa
mdomoni mwa ‘mamba’ kwani alikuwa katika mateso makubwa.
“Nilikuwa nafanyiwa unyama wa kutisha na
mama, ananipiga, ananifinya, ananigongesha ukutani mpaka natokwa na
damu nyingi hadi zinakauka zenyewe.
“Siku nyingine aliniambia ataniua halafu
aniweke kwenye kiroba na kwenda kunitupa porini. Chakula sili
nikashiba, mengine hayaelezeki,” alisema mtoto huyo.
Juzi, Uwazi lilimtafuta
mama wa mtoto huyo kwa njia ya simu lakini ikapokelewa na mwanaume
aliyesema ni mume au baba wa mtoto huyo ambaye alisema:
“Mimi siwezi kusema lolote kuhusu ishu hiyo kwa sababu suala lenyewe lipo polisi.”
Uwazi: “Basi uje ofisini kwetu tuliongelee hili suala la mtoto wako.”
Baba: “Mimi huko ofisini kwenu siwezi kuja.” (akakata simu).
Hata hivyo, kwa mujibu wa mjumbe wa
nyumba kumi, suala hilo limepelekwa Kituo cha Polisi Kimara na
kuandikishwa kwa faili lenye kumbukumbu KIM/2858/016 TAARIFA. Pia, akina
mama hao walimpeleka mtoto huyo kwenye Zahanati ya Serikali, Kimara na
kupewa fomu ya polisi namba tatu (PF3) yenye namba KMR/10791/2016
SHAMBULIO LA KUDHURU MWILI.
Comments
Post a Comment