Babu Seya taabani
DAR ES SALAAM: Mwanamuziki nguli nchini
anayetumikia kifungo cha maisha jela, Nguza Viking ‘Babu Seya’ anadaiwa
yu taaban ambapo amekimbizwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) kwa
matibabu.
Mwandishi wetu alimshuhudia Babu Seya
akiwa Muhimbili chini ya ulinzi wa askari magereza watatu na wafungwa
wengine watano katika Jengo la Taasisi ya Mifupa na Mishipa ya Fahamu
(MOI) huku akiwa amedhoofu.
Haikuweza kujulikana mara moja ugonjwa
uliosababisha Babu Seya ahamishiwe Muhimbili kwa matibabu kwa sababu
Jeshi la Magereza lina hospitali yake na mwandishi alipoomba kwa mmoja
wa askari magereza ili aweze kumsalimia mwanamuziki huyo, hakupewa
ruhusa.
Baadhi ya wananchi waliomshuhudia
mwanamuziki huyo akiwa Muhimbili na kuingizwa katika chumba cha daktari
namba 112 walisema, anavyoonekana ni dhahiri ni mgonjwa kwa sababu
hakuwa mchangamfu kama ilivyo kawaida yake.
“Nguza (Babu Seya) mara nyingi huwa
mchangamfu lakini leo amekuwa mnyonge, mwili umepungua na hata ngozi
yake siyo ang’avu, bila shaka anaumwa sana,” alisema mwananchi mmoja
hospitalini hapo.
Hata hivyo, mara baada ya matibabu, Babu
Seya aliingizwa katika gari la magereza na kurudishwa Gereza la Ukonga
kuendelea kutumikia kifungo chake.
Dodosadodosa ya mwandishi hospitalini
hapo ili kujua kinachomsumbua Babu Seya, haikuambulia chochote kwani
daktari mmoja alisema ni mwiko kwao kutaja ugonjwa wa mgonjwa bila
ridhaa yake na ni kinyume cha maadili ya kidaktari.
“Umeniuliza anaumwa nini, kwanza mimi
siye niliyemtibu lakini hata kama ningejua ugonjwa wa Babu Seya, siwezi
kukuambia ni unethical (kinyume cha maadili). Lakini kweli ni mgonjwa na
ndiyo maana ameletwa hapa kutibiwa,” alisema daktari huyo aliyekuwa nje
ya jengo moja akizungumza na mwanamuziki huyo.
Juni 25, 2004, Hakimu Mkuu Mkazi wa
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar, Eddy Lyamuya aliwatia hatiani Babu
Seya na wanaye Papii Kocha kwa kupatikana na hatia ya kubaka na
kulawiti watoto wa Shule ya Msingi Sinza-Mapambano, Dar na kuwafunga
kifungo cha maisha jela huku rufaa ya kesi yao ikiwekwa kiporo kwenye
Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu iliyopo jijini Arusha.
Comments
Post a Comment