Wabongo wafungukia simu feki kuzimwa
DAR ES SALAAM: Baada ya
Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania ‘TCRA’ kutangaza kuzima simu feki usiku
wa Juni 16, mwaka huu, wananchi mbalimbali wa Jiji la Dar, wamefunguka
ya moyoni:
BARIKI GASTON (MWENGE)
“Kuzimwa simu feki kumeniumiza sana na
siyo mimi tu wapo wengi hasa wenye hali ya chini japokuwa zina madhara
wangetuachia kwa muda mrefu kidogo ili tujipange kwanza.”
HIDAYA SAID (MWANANYAMALA)
“Serikali ilivyofanya siyo vizuri kwa
sababu hali ya maisha ni ngumu, nafanya mama ntilie hapa sina uwezo wa
kununua simu orijino, wangetuangalia sisi watu wa vipato vya chini
wasingezima ila wangezuia zile zinazoingia nchini lakini hizi
tunazomiliki tubaki nazo.”
JOSEPH VENANCE (MWENGE)
“Suala la simu feki kuzima
limetuchanganya sana maana tulishazoea kununua kwa bei rahisi lakini
sasa haya ni majanga kwa sababu mpaka upate hela ya kununua simu orijino
ni kazi sana lakini inabidi tukubaliane tu hali halisi maana zina
madhara pia Watanzania tujifunze kutumia vitu orijino ili kuipatia kodi
nchi yetu.”
Ramadhan Omari ‘Babu Kaju’ (MWENGE)
“Kiukweli uamuzi wa serikali wa kuzima
simu feki siyo sawa kabisa kwani hawajaangalia uwezo wa mwananchi kwani
kuna watu wanauza maparachichi je, watamudu vipi kununua simu ambazo
siyo feki? Pia muda waliotoa wa miezi mitatu ni mdogo sana walitakiwa
watoe muda hata mpaka Januari mwakani ili watu wajipange maana
imeniathiri sana hata mimi.
“Kwa nini wasingewabana wale wanaoingiza
simu hizi feki nchini, mbona ushuru wao wanachukua? Viongozi wanatakiwa
kuwa makini sana katika maamuzi yao maana siku hizi wanaamua tu,
lilikuja suala la ving’amuzi ndiyo vile watu kibao wakatupa TV zao maana
hawana uwezo huo wa kununua hata kama ndiyo kwenda kidijitali siyo kwa
staili hii jamani.”
PIUS NGONYANI ‘KADODA’ (MWENGE)
“Naona sawa tu serikali ilivyofanya kwa
sababu vitu feki siyo vizuri pia inawezekana kuna kitu serikali inakosa
kama kodi lakini kwa simu orijino kodi itapatikana na imejua madhara ya
simu feki japokuwa wamechelewa sana kwani Watanzania wameshatumia kwa
muda mrefu sana simu hizo wao walikuwa wapi.
Comments
Post a Comment