Uwoya Aitwa Ikulu ya Kenya
Irene Pancras Uwoya.
IMELDA MTEMA, amani
DAR ES SALAAM: Zali! Kuna madai
kwamba, Rais wa Kenya, Uhuru Jomo Kenyatta amempa mwaliko maalum staa
mwenye mvuto katika sinema za Bongo, Irene Pancras Uwoya kuitembelea
ikulu ya nchini hiyo, ikiwa ni msanii wa kwanza Bongo kupata fursa hiyo,
Amani limedokezwa.
Kwa mujibu wa chanzo, awali rais huyo
aliwahi kutolewa na jarida moja la nchini humo kwamba anazimikia sana
kazi za filamu za staa huyo kutokana na filamu za Bongo Muvi.
ATUMA WATU KUJA BONGO
Mpashaji wetu huyo alizidi kufunguka
kuwa, Rais Uhuru aliwatuma wasaidizi wake kuja Bongo kumsaka staa huyo
ambapo walipata maelekezo sahihi mpaka wakafika nyumbani kwa wazazi
wake, Mbezi Beach jijini, Dar ambako walipata maelekezo sahihi ya
kumpata Uwoya mwenyewe.
UJUMBE WAKUTANA USO KWA USO NA UWOYA
“Baada ya kuelekezwa jinsi ya kumpata
Uwoya, walifunga safari mpaka Sinza Mori (Dar) nyumbani kwake anapoishi
ambapo walifikisha ujumbe ambao walipewa na Rais Kenyatta. Irene
alishtushwa sana na ujumbe huo lakini baadhi ya watu wake wa karibu,
wakiwemo nduguze walimtoa hofu.
“Walimwambia kwa rais kama Uhuru atakuwa
anamuita kwa nia njema kabisa hivyo asiwe na wasiwasi maana yeye alijua
labda kuna kitu alikosea sasa anakwenda kuwekwa kitimoto,” kilisema
chanzo hicho.
UWOYA AKUBALI KUTINGA IKULU YA KENYA
Mpashaji wetu huyo alizidi kuanika
kwamba, baada ya Uwoya kutolewa hofu alikubali mwaliko huo na amepanga
safari ya kwenda Nairobi, Kenya kwa ajili ya kusikiliza wito huo.
AMANI LAMSAKA UWOYA
Baada ya kupata habari hiyo, gazeti hili
lilimtafuta Uwoya, ambapo alikiri kupata mwaliko huo na kusema kuwa,
kuna vitu anavikamilisha vikishakaa sawa atafunga safari ya kwenda huko
kuitikia wito wa rais huyo.
“Ni kweli nimepata mwaliko huo na pia
binafsi nimefurahi sana kwa kweli ila kuna vitu vyangu naviweka sawa
baada ya wiki kama mbili hivi nitakwenda ili nikajue nimeitiwa nini,”
alisema Uwoya.
KUMBUKUMBU
Hii si mara ya kwanza kwa Uwoya kuitwa
ikulu ya nchi nyingine kwani mwaka 2011, Rais wa Burundi, Pierre
Nkurunzinza alimtumia ujumbe mwigizaji huyo akimtaka aende ikulu kwake
kwa ajili ya mazungumzo ya kumtia moyo na sanaa yake, gazeti hilihili
liliripoti.
Ilikuwa Julai 25, mwaka huo, Uwoya
alisema Rais Nkurunzinza alimuita baada ya kusikia kuwa yupo nchini
mwake na alivuta hisia za wengi kutokana na kazi zake za sinema.
Hata hivyo, katika mwaliko huo, Uwoya
alishindwa kuonana na rais huyo kutokana na ratiba yake lakini aliombwa
kutafuta siku kwenda kumtembelea rais huyo.
FILAMU ZATAJWA
Habari ambazo si rasmi zinadai kuwa,
mwaliko wa Uwoya nchini Kenya unaweza kuchangiwa na kazi zake za sanaa
ambapo, kwa sasa nchi za Kenya, Uganda, Rwanda na Burundi, filamu za
Bongo zinatazamwa na maelfu ya watu.
Comments
Post a Comment