Unawafanyia nini wazazi wako kipindi hiki wakiwa hai?
Assalam aleikum
mpenzi msomaji wangu. Uhali gani wewe uliyepata bahati ya kunisoma tena
wiki kupitia ukurasa huu? Ni matumaini yangu kwamba kwa rehema zake
Mwenyezi Mungu umzima na unaendelea vyema na mishemishe zako za
kimaisha.
Mimi nitakuwa mchoyo wa shukurani kama
sitatumia fursa hii kumshukuru Mungu kwa kila ambalo amekuwa akinitendea
katika kila siku ya maisha yangu. Niseme tu kwamba Mungu ni mwema sana
kwangu.
Mpenzi msomaji wangu, najua Waislam wako
katika mfungo wa Mwenzi Mtukufu wa Ramadhani na wale wanaofuatilia safu
hii watakumbuka niliwahi kuzungumzia suala la kila mmoja kuiheshimu
imani ya mwenzake.
Asitokee hata mmoja wa kujiona yeye ni bora zaidi ya mwingine au kwamba yeye ndiye ambaye yuko kwenye mstari ulionyooka. Wote
tuko sawa na sote ni ndugu, tofauti zetu za kiimani, kikabila na kirangi zisitufanye tukafarakana.
Baada ya kusema hayo nirudi sasa kwenye
mada yangu ambayo nimedhamiria kukuletea kwa wiki hii. Nawazungumzia
wazazi na yale ambayo kila mmoja anapaswa kumfanyia mzazi wake
aliyefanya jitihada za kumleta hapa duniani kisha kumlea hadi kufikia
hapo alipo sasa.
Kwa nini leo nimeamua kuandika mada hii?
Ni kutokana na tukio lililompata rafiki yangu aitwaye Rashidi Salim wa
Dar ambaye huko nyuma alikuwa na maisha magumu sana huku mama yake
akiishi kwa tabu huko kijijini kwao Mlalo Lushoto.
Mwanzo mwa mwaka huu Mungu akamuwekea
mkono wa Baraka, mambo yakaanza kumnyookea lakini wakati anajipanga
kwenda kumjengea nyumba mama yake sambamba na kumfanyia mambo mengine
ili aishi kwa furaha, yule mama akaugua ghafla na kufariki. (Inna Lillah
Wainna Ilaih Rajiuun).
Lilikuwa ni pigo kubwa sana kwa rafiki
yangu huyo, alijua thamani ya mzazi wake huyo lakini wakati akijiandaa
kumfanya ajisikie kuwa amezaa, Mungu akakatisha ndoto zake.
Wakati rafiki yangu huyo akiumia kwa
kushindwa kumpa furaha mama yake akiwa hai, wapo watu ambao hawajui
kabisa thamani ya wazazi. Wamezaliwa, wakalelewa hadi wakakua na kuwa na
maisha yao lakini leo hii wanajiona wao ndiyo wao, wazazi wao
wamewasahau kabisa kana kwamba wamejileta wenyewe kisha wakajikuza
wenyewe.
Mimi nadhani ni wakati wako wewe msomaji
wangu kujitathmini upya na kuona umewafanyia nini wazazi wako katika
kipindi cha uhai wao ili waweze kujivunia uwepo wako.
Maisha yako ya raha mustarehe hayawezi kuwa na maana kama wazazi wako watakuwa wanaishi kimaskini. Kama ulikuwa hujui,
wengi ambao waliwatelekeza wazazi wao
baada ya kupata vijisenti leo hii wanaishi maisha ya ajabu sana, si
ajabu yamesababishwa na laana za wazazi wao. Unataka hilo likupate ndiyo
uanze kujuta?
Usisubiri hilo, kama umejaaliwa kuwa na
wazazi wako mpaka leo na Mungu amekujaalia kufanya kazi na kuwa na
kipato, hata kama siyo kikubwa sana, wakumbuke wazazi wako.
Kumbuka wakati wewe ‘unawapotezea’
wazazi wako walio hai, wapo ambao wanatamani wazazi wao leo hii
wangekuwa hai ili wawafanyie mambo makubwa. Kwa nini? Kwa sababu wanajua
umuhimu wao, wanajua bila wao wasingekuwa hivyo walivyo leo! Wewe
hulijui hilo?
Mpenzi msomaji wangu, hili si jambo la
kutumia nguvu kubwa sana kukufanya uelewe. Kikubwa hapa ni kwamba,
tuwakumbuke wazazi wetu, tuhakikishe wanaishi maisha wanayostahili
kuishi.
Wafanyie kila unaloweza zuri ili kesho
ukiwa umeondoka duniani, wazidi kukuombea. Pia wakitangulia wao, ubaki
na amani kwamba hukuwatenga bali ulijitahidi kuwafanya wajivunie uwepo
wako.
Ni hayo tu, tukutane tena wiki ijayo.
Comments
Post a Comment