Umuhimu wa maziwa mwilini

ziwaaaUnywaji wa maziwa unaopendekezwa na Shirika la Afya Duniani (WHO)  ni mtu mmoja kunywa lita 200 kwa mwaka.
Tovuti za Bodi ya Maziwa Tanzania (TDB) zinaonesha kuwa Mtanzania hunywa wastani wa lita 47 tu kwa mwaka. Wakati unywaji huo wa maziwa si wa kuridhisha, kiwango cha watoto wetu kudumaa bado ni kikubwa ambapo asilimia 35 hudumaa.
Sababu kubwa inayofanya watoto hao kudumaa ni ukosefu wa vyakula vyenye virutubisho mwilini. Maziwa yana virutubisho vyote muhimu kwa ujenzi wa afya ya binadamu kwani yana protini ya daraja la kwanza, mafuta, madini, vitamin na sukari ya asili ya lactose na maji.
Maziwa hutupatia takriban vitamini zote ambazo huyeyuka kwenye mafuta. Nazo ni vitamini A, D, E na K. Vitamini A huhusika na shughuli mbalimbali mwilini. Mfano afya bora ya ngozi zetu kuwa nyororo na ng’avu na pia kuwa na uwezo wa kuzuia wadudu wasiingie mwilini. Vile vile vitamini A hutumika pia kuyapatia macho uimara wa kuona. Na hasa kuona usiku au kwenye mwanga hafifu. Ukosefu wake hudhoofisha macho na hata kuleta upofu, ngozi kusinyaa na kuonekana iliyozeeka hata kama ni ya kijana.
Vitamini D husaidia mwili kuweza kufyonza madini ya Calcium. Bila kuwepo vitamini D Calcium hupotea bure kwa kutolewa nje kama kitu kisichohitajika. Japokuwa vitamini D tunaweza kuipata kwenye jua la asubuhi, lakini watu wengi hawawezi kulipata jua hilo hivyo ni bora kujiwekea uhakika wa kupata vitamini D kwa kunywa maziwa.
Umuhimu wa madini ya Calcium ni kiungo muhimu katika ujengaji wa mifupa. Hasa kwa wajawazito na watoto ambao mifupa yao bado inajengeka. Mwili imara hubebwa na mifupa imara. Na mifupa imara inajengwa na madini ya Calcium. Ni bora kujijengea mifupa imara, meno na sehemu ya mifupa.
 Hakika kila mtu anahitaji meno bora na imara, vilevile Calcium hutumika katika misuli wakati wa kujikunja na kunyooka. Pia husaidia katika mtandao wa ufahamu mwilini Nerve Conduction. Mbali na Calcium maziwa hutupatia madini ya Sulphur, Sodium na Phosphorous ambayo mwili pia huhitaji kwa kazi zake mbalimbali.
Maziwa pia hutupatia sukari (wanga) japo kwa kiasi kidogo. Kwa kuzingatia umuhimu wa maziwa tunaisisitiza jamii kunywa maziwa katika milo ya kila siku ila unywaji kupita kiasi hasa yale yenye krimu husababisha kuongezeka kwa uzito.

Comments

Popular posts from this blog