Ugomvi wa wabunge wa CCM na UKAWA wafikia pabaya
Sakata la wabunge wa Ukawa
kususa vikao vya Bunge vinavyoongozwa na Naibu Spika, Dk Tulia Ackson
limefika pabaya baada ya baadhi ya wawakilishi hao kuanza kutowasalimia
baadhi ya wabunge wa CCM.
Hatua hiyo ilikuwa dhahiri jana baada
ya Ukawa kutangaza kuwa hawatashirikiana na wabunge wenzao wa chama
tawala katika shughuli za kawaida za kijamii, kama vile michezo na
kutumia kantini ya Bunge, wakisema wenzao wameanza kuwabagua.
Mbali na kitendo hicho, wabunge hao
pia walitoka kimyakimya bungeni baada ya Dk Tulia kuingia, lakini safari
hii hawakufanya mbwembwe za kujiziba midomo kama walivyofanya juzi.
Jana asubuhi, mbunge wa CCM Kangi
Lugola alisema kuwa alisikitishwa baada ya kudai kuwa Mbunge wa
Chadema (Viti Maalumu), Lucy Magereli hakumjibu salamu yake wakati
akiingia bungeni licha ya kumsalimia mara tatu na kuwa katika umbali
mfupi wa kusikika.
“Kusalimia ni jambo la utamaduni
wetu. Nilikuwa namsalimia mbunge wa kike wa Ukawa, lakini hakujibu.
Lakini, nikajua ni sababu ya wao kufunga mdomo na plasta, nikamtania au
kwa sababu ya plasta hujibu ili isije kudondoka hakuitikia,” alisema Lugola.
Alisema ameshtushwa na hali ilipofikia
na hajui sababu za msingi za wabunge wa Ukawa kufanya vitendo hivyo,
kinyume na udugu na utamaduni wa Watanzania.
Mbunge huyo machachari, alisema Kubenea alimziba mdomo Msigwa kwa mkono ili asizungumze chochote.
Naye mbunge wa Sumve (CCM ) Richard
Ndassa alisema jambo wanalolifanya wabunge wa Ukawa siyo jema na halina
tija kufanywa na wawakilishi hao wa wananchi.
“Sisi ni wabunge, hivi inapofikia kususa kuongea na wabunge wenzako, hatima yake nini?” alisema.
“Mimi nilienda kuwasalimia kama
kawaida ambavyo huwa tunafanya kwa wabunge awe CUF, CCM au Chadema, sasa
unavyosusa una maanisha nini,” alilalamika Ndassa.
Alisema kitendo cha kutosalimia ni cha
juu sana na kwamba iwapo Ukawa wanashauriwa na mtu basi inawapasa
kuchuja mambo mengine, likiwamo hilo la kuwasusa wabunge wenzao.
Juzi Mbunge wa Vunjo (NCCR-Mageuzi),
James Mbatia wakati anawaongoza wabunge wa Ukawa kutoka bungeni
aliwatuhumu wabunge wenzao wa CCM kuwa wanawabagua
Naye Mbunge wa Ubungo Saed Kubenea alisema; “Leo
tumekubaliana hatutashiriki katika michezo na wabunge wa CCM, hilo
tumeanza leo asubuhi kwenye mazoezi katika viwanja mbalimbali, hivi sasa
tunatafakari hata kutafuta uwanja wetu.
“Tukikutana katika uwanja mmoja, sisi tutatumia upande mmoja na
wao watatumia upande mwingine, hatuchanganyani, hata salamu leo kuna
mmoja kanisalimia nimekwepesha mkono wangu,”
Kubenea alisema hata katika mechi zinazoandaliwa kwa ajili ya timu ya wabunge UKAWA hawatashiriki katika kipindi hiki cha wiki mbili zilizobakia za bajeti.
“Si katika michezo tu, hata katika mahusiano, tumekubaliana kama kuna wabunge wana mahusiano ya kimapenzi na wabunge wa CCM yasitishwe kwa muda wa wiki mbili mpaka tutakavyoamua vinginevyo,” alisema Kubenea.
Kubenea alisema hata katika mechi zinazoandaliwa kwa ajili ya timu ya wabunge UKAWA hawatashiriki katika kipindi hiki cha wiki mbili zilizobakia za bajeti.
“Si katika michezo tu, hata katika mahusiano, tumekubaliana kama kuna wabunge wana mahusiano ya kimapenzi na wabunge wa CCM yasitishwe kwa muda wa wiki mbili mpaka tutakavyoamua vinginevyo,” alisema Kubenea.
Comments
Post a Comment