Mwalimu aporwa bodaboda, auawa!
Na Stephano Mango, RISASI MCHANGANYIKO
RUVUMA: Mwalimu wa shule ya
msingi Lupapila iliyopo kata ya Subira, Manispaa ya Songea mkoani
Ruvuma, Christopher Ndimbo (29) wiki iliyopita aliporwa pikipiki yake na
baadaye kuuawa kwa kukatwakatwa na mapanga na watu wanaodhaniwa kuwa
majambazi.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa
Ruvuma, Zuberi Mwombeji, mwili wa marehemu ulikutwa katika Mtaa wa
Making’inda, Kata ya Msamala mkoani hapa saa 12 jioni, Juni 14, mwaka
huu ukiwa umekatwakatwa na kitu chenye ncha kali, baada ya kuwa
ametoweka nyumbani kwake, Mtaa wa Mji Mwema, tangu Juni 11, mwaka huu.
Kamanda Mwombeji alisema marehemu ambaye
pia alikuwa akijishughulisha na biashara ya bodaboda, alikuwa na
pikipiki yake aina ya Sanlg, yenye namba za usajili MC 762 ACK ambayo
imetoweka.
“Mara ya mwisho marehemu alionekana
akiwa katika maeneo ya Uhuru Pub iliyopo kandokando ya uwanja wa michezo
wa Majimaji majira ya saa 2 usiku akisubiri abiria na baada ya kumpata,
aliondoka kuelekea kusikojulikana,” alisema.
Kamanda alisema walianza kumtafuta
marehemu baada ya mkewe, Jeska Kiswaga (22) kutoa taarifa Kituo Kikuu
cha Polisi cha Songea juu ya kutoonekana kwa mumewe ndipo jeshi hilo kwa
kushirikiana na wananchi walipofanikiwa kumkuta akiwa na majeraha
makubwa kichwani na sehemu zingine za mwili.
Comments
Post a Comment