Mume, Mke Wachinjwa Kinyama.
Na Gregory Nyankaira, RISASI MCHANGANYIKO
MARA: Hali mbaya! Wanandoa Said
Somba (48) na Kadogo Ehijo (47), wakazi wa Kitongoji cha Rugala, Kijiji
cha Mazami, Kata ya Bukabwa wilayani Butiama mkoani hapa wameuawa kwa
kuchinjwa shingo na watu wasiojulikana, Risasi Jumatano lina kila kitu.
Diwani wa Kata ya Bukabwa ambaye pia ni
Mwenyekiti wa Kitongoji cha Rugala, Jonas Maswe aliliambia gazeti hili
kuwa, tukio hilo lilijiri usiku wa Mei 25, mwaka huu ambapo watu hao
wakiwa na mapanga walivamia nyumbani kwa Somba akiwa amelala na mkewe na
kuwachinja.
Alisema wakati wanachinjwa, wanandoa hao
hawakupiga kelele na baada ya ukatili huo wauaji hao waliifunika miili
yao kitandani kisha wakatokomea kusikojulikana.
Alisema mauaji hayo yalifanyika kimyakimya kwani hata watoto wa marehemu waliokuwa wamelala nyumba ya pili hawakusikia lolote.
“Asubuhi ya saa 1 mtoto mmoja wa
marehemu aliamka, akaenda kuwaamsha wazazi wake ili wamfungulie mlango
ajiandae kwenda shuleni.
“Mtoto huyo aliwaita wazazi wake mara
kadhaa bila majibu hivyo aliusukuma mlango ambao ulikuwa umeegeshwa tu,
akaingia ndani ya nyumba hiyo na alipoingia chumba cha wazazi wake
aliwaona wamelala wakiwa wamejifunika shuka.
“Aliwasalimia wakawa kimya, aliwashika
na kukutana na dimbwi la damu, akawaona wazazi wake wamefariki dunia
huku wakiwa na majeraha makubwa shingoni.
“Yule mtoto alipiga kelele zilizowaita majirani nyumbani na kushuhudia unyama waliotendewa wanandoa hao,” alisema Maswe.
Mtoto mkubwa wa marehemu hao, Amos Said
(26) alisema kwamba, licha ya kuwepo mifugo mingi nyumbani hapo kama
vile ng’ombe na mbuzi, lakini wauaji hao hawakuchukua mfugo hata mmoja.
Katibu wa Tarafa ya Makongoro, Khamis
Waryoba, alilaani kitendo hicho na kuapa kusaidiana na Jeshi la Polisi
Wilaya ya Butiama kuwasaka watu waliohusika katika unyama huo.
Polisi wilayani Butiama imethibitisha
kuwepo kwa mauaji hayo na kusema kuwa, wanaendelea na msako mkali wa
kuwabaini waliohusika.
Akizungumzia mauaji yanayoendelea,
Sheikh Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Musa, alikemea hali hiyo,
akiwataka Watanzania kumuomba Mungu aepushe roho hizo za mauaji kwani
hali siyo nzuri.
“Jamii lazima imuogope Mungu, pia kwa
kushirikiana na vyombo vya usalama iwafichue wahalifu wanaotekeleza
mauaji haya huku na sisi viongozi wa dini tukiendelea kuwaombea ili
waachane na roho mbaya walizonazo kwani mambo kama haya hatujayazoea,
tumekuwa tukiyaona kwenye nchi za wenzetu,” alisema kiongozi huyo,
akiungwa mkono na mchungaji wa kanisa moja la kiroho lililopo Madale,
Koplo Jacob.
“Siyo jambo la kujivunia sana kuwa na
jamii isiyoogopa mauaji, kila siku unaposikia watu wanauana ni hatari
kwa taifa, sala maalum inahitajika ili kuwakomboa watu kifikra,”
alisema.
Miili ya marehemu hao, ilizikwa Mei 26, mwaka huu, kwenye makaburi ya nyumbani kwao.
Bwana alitoa na Bwana ametwaa, jina lake libarikiwe. Amina.
Comments
Post a Comment