Mrembo abakwa, auawa!
Na Gladness Mallya, RISASI MCHANGANYIKO
CHALINZE: Inauma sana! Mrembo
Sijaona Issa (25) mkazi wa Pela, Chalinze mkoani Pwani, amebakwa na
kuuawa kikatili na watu wasiojulikana, ingawa yapo madai ya wivu wa
kimapenzi.
Akizungumza kwa uchungu, mama mzazi wa
marehemu alisema kuwa tukio hilo lilitokea wiki iliyopita baada ya
wasamaria wema kukuta mwili wa mwanaye umelazwa uwanjani ukiwa
umefunikwa na kanga moja.
“Jumanne jioni marehemu alirudi kutoka
kazini saa tatu usiku, akala chakula kama kawaida na kuingia chumbani
kwake na sikujua kama alitoka mpaka asubuhi ya saa moja Alhamisi, ambapo
kuna kijana alikuja na kuniuliza kama marehemu yupo ndani, nikaenda
chumbani kwake sikumkuta, nilikuta tu nguo zake alizotoka nazo kazini na
viatu.
“Baada ya kurudi na kumwambia hayupo
ndipo huyo kijana alisema amekutwa ameuawa uwanjani karibu na Tanesco,
ndipo kaka yake akaenda kumuangalia na kukuta kweli ni yeye,” alisema
mama huyo.
Waombolezaji
“Mwanangu alikuwa na uhusiano wa
kimapenzi na kijana mmoja (jina linahifadhiwa) lakini miezi kadhaa
iliyopita marehemu alishindwana na kijana huyo kutokana na kudai ana
wivu sana kwani alikuwa akimpiga kila siku, siku moja aliwaita wajomba
zake na kuwaambia kwamba hamtaki tena huyo mtu.
“Kijana aliposikia hivyo palepale alitoa
kauli kwamba kama amemkataa atamfanyia kitu ambacho hatakisahau katika
maisha yake, hivyo hata siku hiyo walienda kuonana usiku huo na
tunaamini huyo kijana ndiye katekeleza mauaji hayo kwani alishaahidi,”
alisema mama huyo.
Mama huyo aliiomba serikali kuchunguza
vizuri mauaji hayo kwani mwanaye alifanyiwa unyama mkubwa, ikiwa ni
pamoja na kutobolewa macho, kuvunjwa bega na kunyongwa.
Naye Mwenyekiti wa Pela na mji mdogo wa
Chalinze, Hussein Mramba alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kueleza
kuwa mwili wa marehemu ulionekana kuwa na majeraha kama shingo
kuvunjwa, bega kisa kikidaiwa kwamba kulikuwa na mgogoro wa kimapenzi na
mpenzi wake.
“Ni kweli tukio hilo limetokea na
ninaahidi kuwa niko bega kwa bega na familia pamoja na jeshi la polisi
ili kuhakikisha wauaji wanajulikana na kukamatwa,” alisema mwenyekiti
huyo.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Pwani,
Boniventura Mushongi hakupatikana kupitia simu yake ya mkononi ili
azungumzie suala hilo, kwani iliita kwa muda wote bila kupokelewa.
Marehemu alizikwa Alhamisi iliyopita katika Makaburi ya Msuwa yaliyopo
kijijini hapo.
Comments
Post a Comment