Mhariri wa Gazeti la Dira na Mwandishi wake Wapandishwa Kortini
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, imewapandisha kizimbani, mhariri
na mwandishi wa gazeti la Dira ya Mtanzania, Musa Mkama na Prince Newton
kwa kosa moja la kuandika habari za uongo zilizoleta mtafaruku kwa
jamii.
Akisoma hati ya mashtaka jana mbele ya Hakimu Respicius Mwijage,
Wakili wa serikali, Timon Vitalis na Hellen Mushi, alidai mahakamani
hapo kuwa, mnamo Juni 20 katika eneo la Biafra Kinondoni, Jijini Dar es
Salaam washtakiwa hao waliandika na kuchapisha habari za uongo katika
gazeti la ‘Dira ya Mtanzania’ toleo la 424 la tarehe 20 hadi 26 ambazo
zilisababisha hofu na mshtuko kwa jamii kwa kutoa taarifa za uongo kuwa ’Kifaru cha kivita cha Jeshi la Wananchi(JWTZ), chaibwa.’
Alidai kuwa kitendo hicho ni kosa kisheria na ni kinyume na sheria ya magazeti.
Wakili Vitalis alidai kuwa, upelelezi wa kesi hiyo bado unaendelea
na kuiomba mahakama hiyo kupanga tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.
Hata hivyo, washtakiwa hao walikana shtaka hilo na Hakimu Mwijage
aliwataka kuwa na wadhamini wawili ambao kila mmoja atasaini bondi ya Sh
milioni 5.
Washtakiwa hao walikidhi masharti ya dhamana na Hakimu Mwijage aliahirisha kesi hiyo hadi Julai 5 mwaka huu itakapotajwa tena.
Hata hivyo, chapisho hilo hilo katika ukurasa wa mbele na wa pili
lilichapa kwa maandishi makubwa meusi na mekundu taarifa iliyosema: ‘Mwakyembe atuhumiwa kutapeli Bil.2.’ ambayo yalimuudhi Harrison Mwakyembe, Waziri wa Katiba na Sheria.
Mwakyembe aliyasema hayo jana wakati akizungumza na wanahabari
Mjini Dodoma na kudai kuwa, chombo hicho kimekosa weledi na kimepotosha
umma kutokana na chapisho hilo.
“Hii si mara yangu ya kwanza kutuhuma na baadhi ya habari kwa
sababu mbalimbali zikiwemo za kisiasa, napenda nikiri mbele yenu kuwa
sijawahi, kushuhudia upotoshaji mkubwa na wa makusudi na uzushi
uliopitiliza na chuki binafsi iliyo bayana kama ambavyo gazeti hili
limefanya,” alisema Dk. Mwakyembe na kuongeza;
“Nina taarifa kuwa, wameuza sana magazeti; naambiwa print order
(idadi ya nakala) yao imeongezeka na kwamba taarifa yao imesambaa kwenye
mitandao ya jamii, hivyo dunia nzima inajua mimi nina tuhuma za wizi,
za utapeli.”
Pia alisema, gazeti hilo lililendelea kuandika tena Juni 20 wiki hii kwa kuuthibitishia ulimwengu kuwa, “Dk.
Mwakyembe ni tapeli na ushahidi wao mkubwa wametaja barua iliyowahi
kuandikwa na Kampuni ya Power Pool mwaka 2010 na mimi kutumiwa nakala
kwa mtandao (e-mail) wanayodai ni yangu. Kwa busara za gazeti hili, huo
ni ushahidi tosha kuwa mimi ni tapeli.
“Gazeti hilo halina staha na miiko ya uandishi wa habari, kikosi
chetu cha jeshi huko Kisarawe kilielezewa kama kikundi cha wahuni hivi
kinachopiga wananchi hovyo hovyo, kinapiga risasi za moto hovyo hovyo
hadi kumpiga mwananchi moja kiunoni.”
Wakati huo huo alitoa tahadhari kwa televisheni kutosoma magazeti
yenye taarifa tata akitoa mfano wa habari zilizoandikwa na gazeti la
Dira kwamba, kifari cha jeshi kimeibwa.
“Tutafungua kesi hii Mahakama Kuu ya Tanzania, tutawapa taarifa
kila tunavyoendelea. Bado tunaangalia impact (athari) na kuhusika kwa
vyombo vikubwa vya habari kama ITV na STAR TV kutangaza taarifa za
magazeti tata bila uangalifu ili na wao tuwahusishe katika kesi hii,” alisema na kuongeza;
“Kesi hii, nina uhakika, itajenga msingi imara wa wajibu na uhuru wa vyombo vya habari Tanzania kwa muda mrefu ujao.
Comments
Post a Comment