Mdosi mbaroni kwa ujambazi Moshi
Issa Mnally na Richard Bukos, UWAZI
DAR ES SALAAM: Watu watatu
akiwemo mmoja mwenye asili ya Kiasia ‘Mdosi,’ wametiwa mbaroni na polisi
Moshi mkoani Kilimanjaro kwa tuhuma za ujambazi, Uwazi limeezwa.
Akizungumza na waandishi wetu kwa njia
ya simu mwishoni mwa wiki iliyopita, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa
Kilimanjaro, ACP Wilbroard Mtafungwa alisema kuwa watuhumiwa hao
wanashikiliwa na jeshi hilo baada ya kukamatwa kutokana na ushirikiano
wa polisi na raia wema.
Akielezea jinsi polisi walivyowanasa
watuhumiwa hao, Kamanda Mtafungwa alisema kuwa walimkamata kwanza mmoja
Fredil Guston maarufu kwa jina la Chedieli ambaye ni mkazi wa Majengo,
Moshi.
Aidha, alisema Chedieli aliwataja
wenzake ambao ni Frank Nkya maarufu kwa jina la Chabufa na Frank
Mbesanyo Domani ‘Ausho’ mkazi wa Pasua na walipopekuliwa walikutwa na
vitu kadhaa vya wizi.
“Sasa hawa wakamtaja bosi wao ambaye ni
kiongozi wao mkuu wa ujambazi, Mhindi aitwaye Multazi Mohammed (52)
maarufu kwa jina la Bisuza Tazani, mkazi wa Majengo Mwembeni, Moshi.
“Huyu Mhindi ndiye mtunzaji wa silaha
wanazotumia kufanyia ujambazi kwani baada ya kupekuliwa alikutwa na vitu
kadhaa vya wizi na alipohojiwa alitupeleka shambani ambako anaficha
silaha.
“Huko shambani alikuwa ameficha kwenye
mahindi shotigani aina ya Greener yenye namba 43769 ikiwa imefungwa
katika mfuko wa nailoni ikiwa imekatwa mtutu na kitako,” alisema
Mtafungwa.
Aliongeza kuwa uchunguzi wao ulionesha
kuwa silaha hiyo iliibwa kwa Gerard Mosha mkazi wa Rosho Kilemi, Wilaya
ya Moshi Vijijini Machi, 2014 na siku ya tukio hilo Mosha alijeruhiwa
vibaya kwa kukatwa panga kichwani, kupigwa na nondo na kuibiwa vitu
kadhaa dukani kwake.
“Tutawafikisha mahakamani wakati wowote tukikamilisha upelelezi,” alisema.
Comments
Post a Comment