Mahakama Yagomea Pingamizi la Mbowe kwa Jeshi la Polisi
KESI ya madai iliofunguliwa na
Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(Chadema) ya kuiomba mahakama kupiga marufuku zuio la Polisi, leo
limetupiliwa mbali.
Mbowe alifungua kesi hiyo namba
79 ya mwaka 2016, baada ya hivi karibuni Jeshi la Polisi kupiga
marufuku mikutano ya hadhara kwa madai kwamba, hali ya usalama nchini si
salama.
Mbowe ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la
Hai, Kilimanjaro katika shauri hilo, aliwashtaki Mkuu wa Polisi Wilaya
ya Geita na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), kwa madai wanahusika
kuzuia kufanyika kwa mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa.
Mbowe ni Kiongozi wa Kambi Rasmi ya
Upinzani bungeni, walitangaza kufanya oparesheni iliopewa jina ‘Okoa
Demokrasia nchini’ iliyokuwa na lengo la kuishtaki serikali kwa wananchi
kwa kile alichodai, kuendesha nchi bila kufuata katiba ya nchi.
Hata hivyo, baada ya kupigwa marufuku
kwa maandamano, Mbowe alifungua kesi ya madai katika Mahakama Kuu ya
Tanzania Kanda ya Mwanza, akiiomba kutengua zuio hilo la polisi.
Mohammed Gwae, Jaji wa Mahakama Kuu ya
Tanzania Kanda ya Mwanza, leo amepitia ombi lililopelekwa mahakamani
hapo na upande wa mlalamikaji anayewakilishwa na mawakili John Mallya na
Gasper Mwanalelya na kutoa uamzi.
Jaji Gwae akitoa uamuzi wa ombi la
walalamikaji amedai kuwa, amefikia hatua hiyo baada ya walalamikaji
kukosea kifungu cha kupeleka shauri hilo kortini kitendo
kilichosababisha kulitupilia mbali.
Amesema kuwa, walalamikaji baada ya
kupeleka ombi hilo kortini, upande wa wajibu maombi unaoongozwa na
mawakili, Seth Mkemwa na Robert Kidando waliweka pingamizi wakiomba
mahakama kutokusikiliza ombi hilo.
Jaji Gwae amesema kuwa, walalamikaji
katika ombi lao walikosea kutumia kanuni ya tano kifungu kidogo cha tatu
cha sheria ya mwaka 2014 badala ya kanuni ya tano kifungu kidogo cha
pili ambacho kilitakiwa kutumiwa.
“Waleta maombi wametumia kanuni ya tano
kifungu kidogo cha tatu badala ya kutumia kanuni ya tano kifungu kidogo
cha pili kilichotakiwa kuwepo katika kuleta ombi na kama kifungu hiki
hakijatumika hapo na ombi halipaswi kupokelewa,” amesema Jaji Gwae.
Hata hivyo Jaji Gwae amesema, licha ya
kuwekewa pingamizi na wajibu maombi, walalamikaji wamesema kanuni na
kifungu hicho ndivyo vilitakiwa kuwepo na hivyo vinavyopaswa kuwekwa sio
sahihi.
Amesema kuwa, katika shauri la namna
hiyo, kanuni na vifungu vilivyotakiwa kuwepo ni kanuni ya tano kifungu
kidogo cha pili na kanuni ya tano na kifungu kidogo cha vya sheria ya
mwaka 2014 na kwamba wao waliviweka katika maelezo (Statements) badala
ya (chember samers).
Mallya, mwanasheria wa mpeleka maombi
amesema kuwa, baada ya kukosea kanuni na vifungu hivyo, watapeleka kwa
mara nyingine ombi na kulifanyia marekebisho kama Jaji Mohamed Gwae
alivyoelekeza.
Chanzo: Mwananchi
Comments
Post a Comment