Kutoka Arusha: Mbaroni kwa kutupa mapacha
Mtuhumiwa Happiness Joel
JOSEPH NGILISHO, Amani
ARUSHA: AMENASWA! Msako uliofanywa na wananchi wa Kitongoji cha Namayana, Kata ya Kiranyi wilayani Arumeru mkoani hapa, kufuatia tukio la mwanamke kudaiwa kutupa vichanga mapacha, umefanikiwa kumnasa mtuhumiwa Happiness Joel (29), tembea na Amani.
Mwenyekiti wa kitongoji hicho, Elias Naigisa akizungumza na gazeti hili mwanzoni mwa wiki hii, alisema June 7, mwaka huu alipata taarifa ya kutupwa kwa vichanga viwili katika chemba ya choo kinachomilikiwa na mkazi wa kitongoji hicho, Elibariki Loti.
Alisema baada ya taarifa hiyo, yeye na wananchi walikwenda kushuhudia na kukuta vichanga hao wamefariki dunia na kutoa taarifa kwa jeshi la polisi huku yeye na wananchi wake wakianzisha msako mkali kumbaini mwanamke aliyekuwa na ujauzito.
“Polisi walifika na kuchukua miili ya vichanga hao na kwenda kuihifadhi katika chumba cha maiti katika Hospitali ya Mkoa ya Mount Meru kusubiri uchunguzi,” alisema mwenyekiti huyo.
Aliendelea kuweka wazi kuwa June 8, mwezi huu, yaani siku moja baada ya tukio hilo, wananchi walifanikiwa kumbaini mtuhumiwa huyo ambaye pia alikuwa na mtoto wa miaka 2 mgongoni na baada ya kuhojiwa, alikiri kuhusika na tukio hilo.
Alisema mtuhumiwa huyo alieleza kwamba ni kweli alikuwa na ujauzito na aliamua kutupa vichanga hivyo baada ya kujifungua kwa kile alichodai ni bahati mbaya.
Hata hivyo, taarifa nyingine zinadai kuwa mama huyo aliwatupa watoto hao kutokana na aibu baada ya kuwa tayari ana mtoto mdogo mgongoni ambaye bado anamnyonyesha.
Kwa upande wa mwanaume aliyempa ujauzito huo aliyetambulika kwa jina moja la Godlucky, alikiri kumpa ujauzito mwanamke huyo na kusema kuwa amesikitishwa na tukio hilo.
Comments
Post a Comment