Kitwanga afunguka kwa mara ya kwanza, kutua bungeni wiki ijayo
ALIYEKUWA Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga, amesema yupo imara na amerejea nchini akiwa na matumaini mapya.
Pamoja na hali hiyo, amesema
kuwa hivi sasa anajipanga kufanya kazi usiku na mchana kuhakikisha
anaisaidia nchi pamoja na wapigakura wake na kuwa na maendeleo ya kweli
na Jumatano ya Julai 29, ataripoti bungeni.
Kauli hiyo aliitoa Dar es Salaam jana baada ya kurejea akitokea nchini Israel ambako alikwenda kwa shughuli zake binafsi.
Alisema licha ya mtihani uliomkuta,
kwa sasa yupo imara kwa ajili ya kuwatumikia wapigakura wake kwa
kuwawakilisha vema ndani ya Bunge.
“Niko imara kabisa na nina nguvu na
matumaini mapya, nimeingia nchini jana (juzi) nikitokea nchini Israel
ambako nilikuwa na shughuli zangu binafsi. Unajua mimi ni mtaalamu (wa
mawasiliano) na wewe unajua kabla sijaingia kwenye siasa nilikuwa
nafanya nini.
“Kifupi ninasema nilikwenda Israel
kwa shughuli zangu binafsi kabisa ambazo kwa kipindi cha wiki tatu
nilizokuwa huko nimefanya. Hata wanaosema nilikwenda kulia kwa Bwana nao
ni mawazo yao, maana unajua ile ni nchi takatifu kutokana na historia
yake,” alisema Kitwanga.
Alipoulizwa amepokeaje hatua ya
kufutwa kwake kazi na Rais John Magufuli kwa kile kilichoelezwa ni
ulevi, alisema kwa sasa hawezi kusemea jambo hilo kwani aliyemteua ndiye
mwenye mamlaka ya kumwajibisha.
“Rais ni mtu mkubwa anaweza kufanya
jambo lolote ili mradi havunji sheria, hata kilichotokea kwangu ni
mamlaka yake halali, ingawa Mungu ndiye muweza wa kila jambo. Mimi ni
Mkristo safi, nasi tumefundishwa kusamehe saba mara sabini na kusahau
yaliyopita,” alisema.
Akieleza mikakati yake, Kitwanga
alisema kuwa baada ya kuripoti bungeni wiki ijayo, atakuwa na ziara ya
wiki tano ndani ya jimbo lake ambako atazungumza na wapigakura wake na
kueleza yaliyomsibu hatua kwa hatua.
“Sitaki kuingia ndani sana ila
mengine nitayasema nikiwa jimboni, lakini si kwa lengo la kubishana na
mtu, na uzuri kila hatua ambayo nimepitia hata wapigakura wangu
walikuwepo kwa uwakilishi wa madiwani wa Misungwi ambao walikuwa mjini
Dodoma,” alisema.
Mei 21, mwaka huu, Rais Magufuli
alimng’oa Kitwanga kuhudumu kama Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi
kutokana na madai ya ulevi, huku taarifa zaidi za ndani zikieleza kuwa
alianza kushughulikiwa bila yeye mwenyewe kujua.
Comments
Post a Comment