Jinsi Vyakula Vinavyosababisha Magonjwa
Jarida
la Emerging Infectious Diseases linasema kwamba zaidi ya magonjwa 200
yanaweza kusababishwa na chakula. Hata hivyo, vijidudu vinavyosababisha
magonjwa hayo yote si vingi sana.
Huenda takwimu zifuatazo
zinaweza kufanya mtu afikiri hivyo. Kulingana na Shirika la Afya Ulimwenguni
(WHO), kila mwaka watu milioni 130 hivi katika Eneo la WHO huko Ulaya
wanaambukizwa magonjwa yanayosababishwa na chakula.
Katika
mwaka wa 1998, zaidi ya watu 100,000 nchini Uingereza walikuwa wagonjwa kwa
sababu ya kula chakula kibaya, na 200 kati yao walikufa. Inakadiriwa kwamba
kila mwaka watu milioni 76 hivi wanapata magonjwa yanayosababishwa na chakula
huko Marekani, na 325,000 kati yao hulazwa hospitalini, na 5,000 hufa.
Si
rahisi kujua hesabu kamili ya ulimwenguni pote. Hata hivyo, shirika la WHO
linaripoti kwamba watu milioni 2.2 hivi walikufa kutokana na magonjwa ya
kuharisha katika mwaka wa 1998, na milioni 1.8 kati yao walikuwa watoto. Ripoti
hiyo inasema: “Wengi kati ya wagonjwa hao waliambukizwa magonjwa yanayosababishwa
na chakula au maji machafu.”
Huenda
ukashtuka kusikia takwimu hizo kubwa, Lakini je, takwimu hizo zikufanye uwe na
wasiwasi mwingi juu ya chakula? Bila shaka la. Ebu fikiria mfano mwingine. Kila
mwaka watu milioni 4.2 hivi nchini Australia wanapata magonjwa yanayosababishwa
na chakula, yaani watu 11,500 hivi kila siku! Huenda hiyo ikaonekana kuwa idadi
kubwa sana. Lakini kwa upande mwingine: Waaustralia hula milo bilioni 20 kila mwaka, kwa hiyo ni
milo michache sana inayosababisha magonjwa.
Hata
hivyo, hatari ipo. Ni kwa nini chakula kinafanya watu wawe wagonjwa, na
tunaweza kufanya nini kupunguza hatari hiyo?
Jarida
la Emerging Infectious Diseases linasema kwamba zaidi ya magonjwa 200 yanaweza kusababishwa na
chakula. Hata hivyo, vijidudu vinavyosababisha magonjwa hayo yote si vingi sana.
Dakt. Iain Swadling, afisa wa shirika la Huduma ya Kimataifa ya Uchunguzi wa
Chakula, anasema kwamba asilimia 90 hivi ya magonjwa yote yanayosababishwa na
chakula, huenda yanasababishwa na jamii za vijidudu “zisizozidi 24.” Visababishi vya
magonjwa kama vile virusi, bakteria, vimelea, sumu, na kadhalika, huingiaje
katika chakula?
Dakt.
Swadling anataja mambo matano ambayo kwa kawaida husababisha magonjwa: “Kula
chakula kibichi chenye vijidudu; kula chakula kilichotayarishwa na watu
wagonjwa au walioambukizwa viini; kutohifadhi vyakula vizuri na kutayarisha
chakula saa kadhaa kabla ya kukila; kuchafua chakula safi kwa kukiweka pamoja
na chakula chenye vijidudu wakati wa kukitayarisha; kutopika chakula vizuri au
kutopasha moto vya kutosha chakula kilichopikwa kimbele.”
Ingawa
orodha hiyo inaweza kushtua, inaonyesha jambo zuri pia. Jambo hilo ni kwamba
karibu magonjwa yote yanayosababishwa na chakula yanaweza kuzuiwa.
MAMBO
YA KUFANYA
1. SAFISHA.
Nawa
mikono kwa maji ya moto na sabuni kabla ya kuanza kutayarisha kila aina ya
chakula. Nawa mikono baada ya kwenda chooni, na baada ya kushughulikia mtoto
(iwe ni kumbadilisha nepi au kumpangusa makamasi), au kushika mnyama yeyote,
hata mnyama-kipenzi.
Osha
vyombo, mbao za kukatia, na meza kwa maji ya moto na sabuni baada ya
kutengeneza kila aina ya chakula—hasa baada ya kukata nyama, kuku, au samaki na
vyakula vingine vinavyotoka baharini. Gazeti la Test linapendekeza “kuosha
matunda na mboga katika maji ya uvuguvugu” ili kuondoa wadudu na mabaki ya dawa
ya kuua wadudu. Mara nyingi kutoa maganda na kuchemsha vyakula ni njia bora za
kuvisafisha.
Toa
na utupe majani ya nje-nje ya kabichi na letusi (lettuce). Katika sehemu
zenye maji machafu huenda ikawa muhimu kutia dawa ya kuua vijidudu, kama vile
dawa ya kung’arisha, permanganate, au mvinyo wa siki, katika
maji ya kuosha matunda au mboga zitakazoliwa zikiwa mbichi.
2. PIKA VIZURI.
Karibu
bakteria zote, virusi vyote, na vimelea vyote vitakufa ikiwa chakula kitapikwa
kufikia nyuzi Selsiasi 70 (moto kabisa), na si lazima kupika kwa muda mrefu.
Kuku anahitaji kupikwa hadi aive kabisa kufikia nyuzi Selsiasi 80. Chakula
kinachopashwa moto chapasa kufikia nyuzi Selsiasi 75 au kuwa moto na kutoa
mvuke. Usile kuku ambaye bado ni mwekundu au mayai yasiyopikwa vizuri. Samaki
anapasa kupikwa hadi awe laini na kubadilika rangi.
3. USIWEKE VYAKULA PAMOJA.
Usiweke
kamwe nyama, kuku, au samaki mbichi pamoja na vyakula vingine unapofanya
ununuzi, unapohifadhi vyakula hivyo, au unapovitayarisha. Usiache maji ya vyakula hivyo yatone
wala kutiririka kwenye vyakula vingine. Usiweke kamwe chakula kilichopikwa
kwenye chombo kilichokuwa na nyama, samaki, au kuku mbichi ila chombo hicho
kiwe kimeoshwa vizuri kwa maji ya moto na sabuni.
4. HIFADHI VYAKULA IFAAVYO.
Friji
inaweza kuzuia bakteria zisiongezeke, lakini halijoto yake inapasa kuwa nyuzi centigredi
4 tu. Mashine ya barafu inapasa kuwa na nyuzi centigredi 17 chini ya kiwango
cha kuganda. Weka vyakula vinavyoweza kuharibika kwenye friji kabla ya muda wa
saa mbili kuisha. Ukiweka vyakula mezani mapema, vifunike ili kuzuia inzi.
5. UJIHADHARI UNAPOKULA KWENYE MIKAHAWA.
Inakadiriwa
kwamba katika nchi fulani zilizoendelea, asilimia 60 hadi 80 ya watu waliopata
magonjwa yanayosababishwa na chakula walikula vyakula vilivyopikwa mikahawani.
Hakikisha kwamba mkahawa unamokula unafuata sheria za usafi zilizowekwa na
serikali. Agiza nyama iliyopikwa vizuri. Unaponunua chakula mkahawani na
kukileta nyumbani, kile kabla ya muda wa saa mbili kuisha. Endapo muda zaidi
ungepita kabla hujala chakula hicho, kipashe moto vizuri kufikia nyuzi centigredi
75.
6. TUPA CHAKULA UNACHOSHUKU KIMEHARIBIKA.
Afadhali
utupe chakula ambacho unashuku kimeharibika. Si vizuri kutupa chakula kizuri,
lakini matibabu ya ugonjwa uliosababishwa na chakula kilichoharibika
yatakugharimu fedha nyingi hata zaidi.
source:manyandaheath
Comments
Post a Comment