Hii Ndiyo Sababu ya Wanafunzi 7802 UDOM Kurudishwa Nyumbani
JUMUIYA ya Wanataaluma ya Chuo
Kikuu cha Dodoma (UDOMASA) imesema kilichotokea si walimu kugoma
kufundisha programu ya Stashahada Maalumu ya Elimu, Sayansi, Hisabati na
Tehama, bali tatizo ni kutoelewana na Menejimenti ya chuo kutokana na
mazingira mabovu ya uendeshaji wa programu hiyo chuoni hapo.
Aidha, imelaani kitendo cha wanafunzi
7,802 wa Programu Maalumu ya Ualimu wa Msingi na Sekondari,
waliorudishwa nyumbani bila kupewa muda wa kutosha kujiandaa kwa
kuzingatia umri wao na mazingira waliyokuwa wanaishi, hali inayofanya
wazagae mitaani huku wakiwa hawana pa kwenda.
Hayo yako kwenye tamko lililotolewa
jana na Katibu wa jumuiya hiyo, Lameck Thomas, ambalo lilieleza kuwa
lawama zimekuwa zikitupwa kwa walimu kutokana na taarifa hizo kutolewa
na upande mmoja, ambao ni Menejimenti ya chuo kwenda serikalini bila
kuwepo na taarifa yoyote kutoka kwa walimu kupitia jumuiya yao.
Thomas alisema si kweli kama walimu
waligoma kufundisha lakini tatizo kubwa ni kutoelewana kati ya walimu na
Menejimenti ya chuo kutokana na mazingira mabovu ya uendeshaji wa
programu hiyo chuoni hapo.
“Hatuzungumzii fedha zaidi
tunazungumzia suala la kuboresha elimu ili taifa lipate walimu wa
baadaye katika kufundisha Sayansi, Hisabati na Tehama, vifaa vya
kufundishia navyo ni changamoto kubwa,” alisema.
Katibu huyo alisema kama Jumuiya ya
Wanataaluma wanapata hisia kwamba Wizara ya Elimu, imeamua kwa makusudi
kushirikiana na uongozi wa chuo kupotosha uhalisia wa jambo hilo kwani
hakuna hata wakati moja ambao wamefanya mawasiliano na walimu wenyewe
kupata ukweli kutoka upande wao.
“Alichosema waziri bungeni juzi ni
taarifa ya upande mmoja ambayo haitatupeleka kwenye utatuzi wa kudumu wa
suala hili kutokana na ukweli kwamba walimu nao wana mengi ya
kuzungumza,” alisema katibu huyo.
Alisema serikali imejenga desturi ya
kuonana na menejimenti za vyuo pindi yanapotokea matatizo bila kupata
taarifa kutoka vyanzo vingine hali ambayo imekuwa inasababisha vyanzo
sahihi vya matatizo kutojulikana kwa uwazi.
Alisema changamoto za ufundishaji
kutokana na uhaba na walimu kulingana na idadi ya wanafunzi waliopo.
Akitoa mfano alisema kwa sasa Chuo cha Sayansi Asilia na Hesabu, kina
upungufu wa walimu 128 waliokuwa wanahitajika kufundisha programu hiyo
kwa ufanisi; na kwa muhula uliopita walimu 72 tu ndio walibeba mzigo wa
upungufu huo na muhula huu hali ilikuwa inaelekea kuwa mbaya zaidi.
“Wingi wa wanafunzi na uhaba huu wa
walimu ulisababisha upangaji wa ratiba na kufundisha kutokana na ukweli
kwamba kozi ziligawanywa katika mikondo mingi ambayo walimu
walilazimishwa kuifundisha huku wakiwa na majukumu ya kufundisha kozi za
shahada na majukumu mengine,” alifafanua.
Alisema chuo kimekuwa na desturi ya
kupokea wanafunzi wengi bila kuzingatia idadi ya walimu waliopo na
miundombinu ya kufundishia na kujifunzia na hiyo si mara ya kwanza kwa
chuo kufanya hivyo, kwani mwaka 2008 walileta wanafunzi wengi ambao
matokeo yake walimu kufundisha masomo mengi kuliko uwezo wao wa kazi.
Alisema taarifa iliyotolewa na Ofisi
ya Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Taaluma ilipotoshwa, kwani haijaeleza
ukweli wa madai uliowasilishwa na chuo husika.
Alisema katika Chuo cha Sayansi Asilia
na Hesabu taarifa inasema yaliyowasilishwa ni madai ya Sh milioni 367.8
na kupungua mpaka Sh milioni 90 wakati uhalisia ni kwamba madai hayo
hata yangebanwa namna gani yasingepungua mpaka chini ya Sh milioni
223.7.
Alisema mfano mwingine ni Chuo cha
Elimu Masafa na Sayansi za Kompyuta ambao taarifa inasema waliwasilisha
madai yanayozidi Sh milioni 100 wakati taarifa ya chuo inasema ni madai
ya Sh milioni 53.7 tu.
Mwenyekiti wa jumuiya hiyo, Edson
Baradyana alisikitishwa na yaliyotokea na kuitaka serikali kufanya
jitihada za makusudi ili kumaliza mgogoro huo na hilo litawezekana kama
walimu, wanafunzi na Menejimenti kukaa pamoja.
Baradyana alisema wanafunzi
hawakutendewa haki kwani ilitolewa notisi ya ghafla ya kuondoka chuoni
huku wengine wakiwa hawana nauli na hawakujua pa kwenda hali inayofanya
waendelee kuzurura mitaani.
Alisema wanaamini kama Menejimenti ya
chuo ingeonesha ushirikiano wa karibu kwa walimu wanaofundisha programu
hiyo na kushirikiana, hayo yasingetokea au yasingekuwa makubwa kiasi
hicho.
“Lazima kuangaliwa na kutatuliwa
kwa changamoto nyingine zilizoibuliwa na wanataaluma na wanafunzi katika
uendeshaji wa programu hiyo badala ya kujikita kwenye suala la malipo
tu, serikali iwe na utaratibu wa kuwasiliana na walimu na wanafunzi mara
kunapotokea matatizo vyuoni ili kupata taarifa toshelezi kutoka pande
zote,” alisema Mwenyekiti wa Udomasa.
Aidha, wakati wa kurejeshwa nyumbani
kwa wanafunzi hao wa Udom kukibebwa kisiasa na vyama vya upinzani,
taarifa ya serikali imeeleza kuwa wahadhiri waliogoma, walitaka kulipwa
posho ya zaidi ya Sh milioni 900.
Akitoa taarifa ya pili bungeni juzi
usiku, Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi,
Profesa Joyce Ndalichako alisema wanafunzi hao si sehemu ya kazi
zilizoko katika mikataba ya ajira ya wahadhiri hao, ila ni sehemu ya
kazi ya ziada.
Kwa kuwa kazi hiyo ni ya ziada,
Profesa Ndalichako alisema walikubaliana walipwe posho ya kazi ya
nyongeza ambayo uongozi wa Chuo Kikuu cha Dodoma ulikuwa tayari kutoa
zaidi ya Sh milioni 200.
Kwa mujibu wa Profesa Ndalichako,
wahadhiri hao walisisitiza kuwa wanataka posho hiyo iwe zaidi ya Sh
milioni 900, jambo lililokataliwa na Mkaguzi wa Ndani wa Mahesabu wa
Udom aliyesema kuwa kiwango hicho ni kikubwa kuliko uhalisia wa kazi
yenyewe.
Kutokana na kutokubaliana kati ya
wahadhiri hao na uongozi wa Udom, wahadhiri hao ndio wakaitisha mgomo wa
kufundisha wanafunzi hao huku wakiendelea na kazi za kufundisha walio
katika programu za shahada ya kwanza na kuendelea.
Profesa Ndalichako alisema kwa uamuzi
huo wa wahadhiri, serikali isingeweza kuwachukulia hatua kwa kuwa
wamegomea kazi ya ziada na si kazi waliyoajiriwa na kuingia mkataba na
chuo.
Kwa hali hiyo, Profesa Ndalichako
alisema serikali ililazimika kuingilia kati ambapo Mei 10, mwaka huu
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Stella
Manyanya alikwenda chuoni hapo kutafuta suluhu.
Mbali na Naibu Waziri, alisema hata
makatibu wakuu wa wizara hiyo nao walikwenda kuzungumza na wahadhiri hao
bila mafanikio, huku wanafunzi hao wakikaa chuoni bila kuingia darasani
kwa wiki ya tatu.
Profesa Ndalichako alisema mbali na
madai ya wahadhiri hao, pia wakati wa kutafuta suluhu ya jambo hilo,
walitazama suala la tija kwa wanafunzi hao wa diploma maalumu ambao ni
zaidi ya 7,800 na pia kwa wanafunzi wa shahada ya kwanza ambao pia
wanapaswa kufundishwa na wahadhiri hao.
Kutokana na kukosa masomo kwa wiki
tatu mfululizo na kuwepo kwa uwezekano wa kukosekana tija katika
ufundishaji, Profesa Ndalichako alisema ndio uamuzi wa kuwarudisha
nyumbani wanafunzi hao ukafanyika ili serikali iangalie upya utaratibu
wenye tija zaidi wa kuwaendeleza wanafunzi hao.
Aidha, Profesa Ndalichako alisema
wakati wanafunzi hao wakitakiwa kurudi nyumbani, walizingatia hali yao
ya kipato, kwa kuwa tayari walikuwa wameshapewa fedha za kujikimu za
siku 60 tangu Aprili 21, mwaka huu.
Profesa Ndalichako aliwataka wanafunzi
hao kuvuta subira wakati serikali inatafuta namna bora ya kuwapatia
elimu hiyo kwa kuzingatia tija kwao.
Comments
Post a Comment