Hawa Wamechinjwa Bila Hatia!


Mauaji Sengerema (22)Marehemu Mkiwa Philipo.
Stori: Oscar Ndauka, Risasi Jumamosi
DAR ES SALAAM na mikoani: Inauma sana! Ndilo neno ambalo linafaa kutumika kwa sasa kufuatia kuibuka kwa mauaji  kwa njia ya kuchinja sehemu mbalimbali za nchi hali inayoibua hofu kwa wananchi, Risasi Jumamosi limechimba na kuibuka na ripoti kamili.
Mauaji Sengerema (21)TUKIO JIPYA
Tukio bichi kabisa ni lile la Mei 31, mwaka huu kwenye Kitongoji cha Kibatini, Kata ya Mzizima, Manispaa ya Tanga ambapo watu 8 wameuawa kwa kuchinjwa shingo kikatili na watu wasiojulikana, madai yakitajwa kuwa ni kisasi.
Mauaji Sengerema (2)Marehemu Eugenia Philipo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Leonard Paul, aliwataja watu hao kuwa ni Mjumbe wa Serikali ya Kijiji, Issa Hussein (50), Mkola Hussein (40), Hamisi Issa (20) na Mikidadi Hassan (70).
1Marehemu Anathe Msuya
Wengine ni Mahmoud (anakadiriwa kuwa na umri wa miaka 35 hadi 40), Issa Ramadhani (25) na wachunga ng’ombe wawili walilofahamika kwa jina mojamoja, Kadiri na Salum.
Kwa hesabu za jumla, mpaka Mei mwaka huu, jumla ya Watanzania wasio na hatia 27 wameuwa kwa njia ya kuchinjwa hali inayoibua maswali kwamba, ni roho gani ameingia kwenye taifa kwa sasa.
WAUAJI WAKIMBIA, HOFU YATANDA
Baadhi ya wananchi walioongea na Risasi Jumamosi walisema kuwa, kinachowashangaza ni kwamba, wauaji hao wamekuwa wakiingia mitini baada ya mauaji bila kukamatwa hali inayozidisha hofu kuwa, bado wapo  mitaani kuendeleza ukatili huo.
“Mfano mzuri wale waliochinja watu 3, msikitini Mwanza, wale walichinja watu 7 familia moja, Sengerema, wamekimbia na wanasakwa. Hii ina maanisha kwamba, wapo katika jamii,” alisema Daudi Jawala, mkazi wa Kirumba jijini Mwanza.
BINADAMU WAMEKUWA WANYAMA KULIKO WANYAMA WENYEWE
Kufuatia staili hiyo ya kuua kwa kuchinja, wengine waliozungumza na gazeti hili walisema kuwa, ni ukatili mkubwa kufanywa na binadamu na sasa, binadamu wamekuwa wanyama hata simba wana nafuu.
“We jaribu kufikiria binadamu anachukua kisu, anamkamata mwenzake halafu anapitisha kisu shingoni ili autoe uhai wake.
“Kwa vyovyote vile, wakati uhai wa mwenzake unatoka lazima kuna kutapatapa lakini hilo wachinjaji wala haliwapi shida, ndiyo maana nasema, kwa ukatili huu, tumewapita wanyama,” alisema Mashaka Mgosi, mkazi wa Korogwe, Tanga.
Akaendelea: “Katika taifa ambalo watu waliishi kwa amani, inasikitisha kuona leo hii, watu wote hao  tena bila hatia, wamechinjwa.”
VIONGOZI WA DINI WAZUNGUMZA
Juzi, Risasi Jumamosi lilizungumza na baadhi ya viongozi wa dini ambapo walisema kuwa, roho wa kuua kwa kuchinja amewaingia baadhi ya binadamu kwa vile, hofu ya Mungu katika jamii imeondoka.
SHEHE MKUU MKOA WA DAR ES SALAAM
“Jamii lazima imuogope Mungu, pia kwa kushirikiana na vyombo vya usalama iwafichue wahalifu wanaotekeleza mauaji haya huku na sisi viongozi wa dini tukiendelea kuwaombea watu ili waachane na roho mbaya walizonazo kwani mambo kama haya hatujayazoea, tumekuwa tukiyaona kwenye nchi za wenzetu,” alisema Shehe Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhadi Musa Salum.
NABII NICHALOUS SUGUYE
Naye Nabii wa Huduma ya Neno la Upatanisho (WRM) iliyopo Matembele ya Pili, Kivule jijini Dar, Nicholaus Suguye, yeye alisema: “Ndiyo maana sisi watumishi wa Mungu kila siku tunahubiri Neno la Mungu kwamba watu watubu na kuokoka kwa vile wanaofanya hivyo wanakosa hofu ya Mungu ndani ya mioyo yao.
MAMA RWAKATARE
Mchungaji Getrude Rwakatare ni Mchungaji Kiongozi wa Kanisa la Assemblies of God, Mikocheni B jijini Dar. Yeye alilaani matukio ya watu kuchinjana huku akisema, umefika muda Watanzania wamgeukie Mungu kwa wingi.
“Watanzania waokoke. Wakiokoka watakuwa wanaishi kwa hofu ya Mungu. Mungu hapendi mauaji, Mungu hapendi dhuluma, watu wanachinjana kwa sababu hawana hofu ya Mungu,” alisema mama Rwakatare.
KUMBUKUMBU ILIVYO
Kwa kuanzia mbele kurudi nyuma, Mei 31, mwaka huu, watu 8 wameuawa kwa kuchinjwa katika Kitongoji cha Kibatini jijini Tanga.
WATU 7 FAMILIA MOJA SENGEREMA
Mei 11, mwaka huu, vilio, majonzi, simanzi na sintofahamu vilitawala kwenye Kitongoji cha Nyigumba, Kijiji cha Sima wilayani Sengerema kufuatia watu saba kwenye nyumba moja kuuawa kwa kukatwakatwa mapanga na binadamu wenzao wasio na utu.
Watu hao ni Eugenia Philipo Kwitega, Maria Philipo Kwitega Mabula Makeja, Mkiwa Philipo Kwitega, Leonard Aloyce, Donald na Samson. Watuhumiwa walikimbia.
MSIKITINI MWANZA
Mei 19, mwaka huu, watu wanaokadiriwa kufikia 15 walivamia Msikiti wa Rahman ulioko Ibanda Relini, Utemini wilayani Nyamagana, Mwanza na kuwaua watu watatu, Feruz Elias, Mbwana Rajabu na Khamisi Mponda kwa kuwachinja kwa mapanga kisa kikidaiwa kuwa, kwa nini walikuwa wakiswali wakati wenzao saba walikamatwa na polisi. Watuhumiwa walikimbia.
ANETHE MSUYA
Mei 26, mwaka huu, mwanadada Anethe Msuya (dada wa bilionea marehemu, Erasto Msuya), aliuawa kwa kuchinjwa shingoni katika tukio lililojiri nyumbani kwake, Kibada Block 18, Kigamboni, Dar. Watuhumiwa walikimbia.
MUME, MKE WACHINJWA MARA
Mei 25, mwaka huu, wanandoa Said Somba  na mkewe, Kadogo Ehijo, wakazi wa Kitongoji cha Rugala, Kijiji cha Mazami, Kata ya Bukabwa wilayani Butiama mkoani Mara waliuawa kwa kuchinjwa shingo na watu wasiojulikana.
MUME KUMCHINJA MKE, MTOTO
Mei 5, mwaka huu, Jeshi la Polisi mkoani Pwani lilimshikilia Frowin Peter Mbwale, mkazi wa Kawe, Dar kwa tuhuma za kuwaua kwa kuwachinja mkewe, Oliver Erasto na mtoto wake, Emanuel Frowin kutokana na wivu wa mapenzi katika tukio lililojiri wilayani Bagamoyo.
MWANAMKE ACHINJWA GESTI
Saa 11 jioni ya Aprili 22, mwaka huu, mwanamke mjasiriamali, Yunice Peter Alemo, mkazi wa Gongo la Mboto jijini Dar, alikutwa ameuawa na mwili wake kulazwa kifudifudi juu ya kitanda katika gesti moja iliyopo Wilaya ya Ifakara mkoani Morogoro huku ukiwa na majeraha ya kitu chenye ncha kali na shingo yake hali iliyodaiwa kuwa alichinjwa. Mtuhumiwa alikimbia.
DENTI ACHINJWA KILABUNI
Machi 19, mwaka huu, mwanafunzi wa kidato cha sita Shule ya Sekondari Thaqaafa jijini Mwanza, Amos Kitala aliuawa kwa kuchinjwa na chupa shingoni kwenye kilabu cha pombe za kienyeji kufuatia ugomvi kati yake na  mtuhumiwa ambaye alitoroka.
MATUKIO YA JUMLA
Katika kumbukumbu ambazo tarehe hazioneshi, mtoto Willy Kasiga wa Kigogo jijini Dar, aliuawa kwa kuchinjwa na mtu anayedaiwa kuwa ni wa karibu yake kwa kisa ambacho hakikuwa wazi.
Mwanzoni mwa mwaka, Polisi Mkoa wa Arusha iliwatia mbaroni watu wawili kwa kuhusishwa na tukio la kuuawa kwa kuchinjwa shingo kwa Mkuu wa Idara ya Upelelezi ya Ulinzi wa Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa), Stephen Kisamo.
Miezi ya hivi karibuni, dereva wa lori, Salum Masoud aliuawa kwa kuchinjwa na watu wasiojulikana katika tukio lililojiri wilayani Rufiji Mkoa wa Pwani.
KUTOKA AMBONI
Habari zilizotufikia wakati tunakwenda mitamboni zinadai kuwa, wakazi kwenye Kitongoji cha Kibatini ambako watu wanane waliuawa kwa kuchinjwa, wameanza kuzibomoa nyumba zao na kuondoka kwa kile kilichosemekana kuwa, wanahofia usalama wao.

Comments

Popular posts from this blog