Hatma ya Uingereza Kujitoa Jumuiya ya Ulaya
HISTORIA inaibeba Uingereza (England) ikijulikana kama moja ya nchi zenye nguvu zaidi duniani katika masuala ya kiuchumi na kijeshi. Historia hii haipishani na ukweli halisi kwamba katika dunia ya sasa ya utandawazi kila nchi inapigania kujijenga kiuchumi na ikihakikisha usalama wa uchumi wake na taifa kwa ujumla.
Uingereza inabaki kuwa miongoni mwa mataifa yenye nguvu na ushawishi mkubwa katika masuala ya kimataifa ikijivunia historia yake, uchumi wake, nguvu yake ya kijeshi. Hii ni pamoja na nguvu kubwa ya ushawishi iliyonayo ikiungwa mkono na nchi nyingi za Amerika na Afrika.
Kutokana na historia yake yenye kila aina ya ushawishi na kuogopwa, ndivyo lilivyo kila jambo linalofanyika Uingereza ambapo huvutia macho na masikio ya watu wengi duniani vikiwamo vyombo vya habari kufuatilia na kuripoti kila jambo linalotokea kwa haraka.
Inasemeka nguvu yake ya kihistoria na ushawishi wake kimataifa umeifanya ligi kuu yake ya mpira wa miguu maarufu kama English Premier League kuwa ligi maarufu zaidi ulimwenguni ikifuatiliwa na mamilioni ya watu ulimwenguni kote.
Wiki hii Waingereza walipiga kura kujitoa kwenye Jumuiya ya Ulaya. Jumuiya ya Ulaya (EU) inaundwa na nchi 28 (kabla ya Uingereza kujitoa). Ni kura muhimu zaidi kwa Waingereza baada ya mwaka jana watu wa Scotland kupiga kura ya maoni ya ama kujiondoa ama kubaki kwenye muungano wa taifa lao unaojulikana kama United Kingdom (UK) ambako matokeo yalionesha wananchi wengi wa nchi hiyo walipiga kura kubaki kwenye muungano huo.
Wachambuzi waliobobea katika masuala ya maamuzi ya wengi kwa njia ya kura walitegemea Waingereza wengi wangepiga kura ya kubaki kwenye jumuiya hiyo ya Ulaya lakini hali imekuwa tofauti ambapo Waingereza wengi wao wamepiga kura ya kujiondoa kwa asilimia 52%.
Kutokana na nguvu ya kisiasa, ushawishi na kijeshi iliyonayo Uingereza kimataifa ni dhahiri suala la nchi hiyo kujitoa kwenye jumuiya hiyo litaleta madhara makubwa duniani kwa ujumla. Wanadiplomasia wengi na viongozi wengi duniani wamestushwa na uamuzi huu wa wananchi wa Uingereza kujitoa kwenye jumuiya hiyo.
Baada ya matokeo ya awali Rais wa Marekani Barack Obama leo ameomba kuonana kwa dharura na Waziri Mkuu wa Uingereza David Cameron (aliyejiuzulu mara tu baada ya kutangazwa kwa kura hiyo) lengo kubwa likiwa ni kutaka kuzungumzia namna gani wanaweza kukabiliana na hali hiyo ya nchi hiyo kujitoa kwenye jumuiya hiyo.
Wakati huohuo, Rais wa Ufaransa ameitisha kikao cha dharura ikulu kujadili mustakabali wa nchi yao ndani ya Jumuiya ya Ulaya.
Madhara makubwa yanayotabiriwa kujitokeza kutokana na maamuzi ya Uingereza kujitoa ni mengi, miongoni mwake ni yafuatayo.
Kusambaratika kwa Jumuiya ya Ulaya, ni ukweli usiopingika kwamba kwa sasa jumuiya hiyo ipo hatarini kusambaratika baada ya Uingereza kujitoa. Ikumbukwe kwamba ndani ya jumuiya hiyo, Uingereza ilikuwa na nguvu ya ushawishi, hivyo suala lake la kujitoa litafanya na zile nchi ndogo kutaka kujitoa hasa zile zinazofuata nyayo za Uingereza.
Baadhi ya wananchi wa Ufaransa nao wameonesha nia ya kutaka kuweka mapendekezo ya nchi yao kujitoa kwenye jumuiya hiyo. Mwanasiasa Marine Le Pen wa chama cha National Front Party kupitia mtandao wake wa twitter ameandika: “Nimefurahi sana na maamuzi haya, nadhani ni wakati sasa wa nchi zote wanachama hususani Ufaransa kuangalia upya mustakabali wetu ndani ya jumuiya”.
Wadadisi wa mambo wanaona kuna uwezekano mkubwa sana wa nchi nyingi zaidi kujitoa.
Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameron, ambaye alikuwa anaunga mkono Uingereza kubaki ndani ya jumuiya hiyo, tayari amekwishajiuzulu akihitimisha uongozi wake wa muda mrefu ndani ya taifa hili lenye ushawishi na nguvu ya kila namna. Hii ina maana kuwa dola imeangushwa, ni anguko kwa Cameron na inadhibitisha kwamba sasa ameanza kupoteza mvuto ndani ya nchi yake ya Uingereza, hali iliyopelekea serikali yake kuangushwa.
Nchi za Afrika nazo zitaathirika kwa namna moja ama nyingine kwa uamuzi huu wa Waingereza kujitoa Jumuiya ya Ulaya kutokana na ukweli kwamba nchi nyingi zimekuwa zikitegemea misaada moja kwa moja toka jumuiya hiyo. Endapo jumuiya itavunjika basi kuna uwezekano mkubwa sana wa nchi za Afrika kukosa misaada hii ya kudumisha maendeleo yao kwani watalazimika kutegemea misaada toka nchi mojamoja tofauti na sasa ambapo misaada inatoka moja kwa moja toka kwenye jumuiya.
Kuna uwezekano mkubwa sana wa kukwama kwa miradi mingi iliyoanzishwa kwenye nchi nyingi za Afrika iliyokuwa ikitegemea misaada ya moja kwa moja kutoka kwenye jumuiya hiyo.
Hatua ya Uingereza kujitoa EU itaweka mwanzo na mfano mbaya wakati huu ambao wengi wetu tunaamini umoja na kuungana ni nguvu kuliko kujitenga. Wengi wanatafsiri kama mwanzo mbaya wa matabaka ya wenye nacho na wasio nacho ambapo nchi tajiri zitajitenga huku nchi maskini zikitangatanga kwa kupewa mikopo yenye masharti magumu na misaada kupungua kwa nchi maskini. Pia, kuna uwezekano mkubwa wa siasa za kimataifa za kujipendelea kuliko kufanya mambo kwa pamoja.
Kushuka kwa thamani ya sarafu ya Uingereza (Pound) kwa asilimia 7.7 nchini humo muda mchache baada ya matokeo ya kura ya kujiondoa , imeshuka kwa asilimia 10 nchini Ujerumani na inatarajiwa thamani yake itazidi kuporomoka.
Hii ni kutokana na kupoteza mvuto kwenye soko ambao watu wengi wanahofia kufilisika zaidi endapo thamani itazidi kushuka. Ni lazima Waingereza wajipange namna gani watakayakabili madhara yote yatakayosababishwa na wao kujitoa kwenye jumuiya hiyo hasa kutokana na ukweli kwamba wengi wao walitegemea kura ya kubaki ndiyo ingeshinda.
Waziri Mkuu wa Uingereza na washirika wake hawakutegemea kama wananchi wengi wangependekeza nchi yao kujitoa. Kwa kifupi, hawakujipanga na hilo litabaki kuwa historia kwa Waingereza na duniani kwa ujumla.
Japo itachukua miaka miwili zaidi kwa Uingereza kukamilisha taratibu zake za kujitoa ndani ya jumuiya hiyo, kuna uwezekano mkubwa wa kupanda kwa gharama za kupiga simu na matumizi ya simu kwa ujumla barani Ulaya. Hii ni pamoja na kushuka kwa bei ya nyumba nchini Uingereza, kupanda kwa gharama za maisha katika nchi hiyohiyo.
Pia wageni ambao ni wafanyabishara, watapandisha bei za vitu kufidia anguko la sarafu yao, vilevile kushuka kwa thamani ya pesa yao kutafanya gharama ya kununua malighafi kutoka nje ya Uingereza kuwa kubwa zaidi ya sasa. Hivyo, kujiondoa kwao kutawafanya Waingereza wapitie katika kipindi kigumu zaidi katika historia toka kumalizika kwa Vita ya Pili ya Dunia.
Kitakachofuata baada ya kujitoa
Kifungu cha 50 cha mkataba wa kuundwa kwa Jumuiya ya Ulaya kimeeleza bayana ni hatua gani za kufuatwa kwa nchi yoyote ile ndani ya jumuiya endapo itataka kujitoa. Hatua hizo ni kama zifuatazo:-
i). Uingereza kuijulisha Jumuiya ya Ulaya kusudio lao la kimaandishi la kutaka kujitoa ndani ya jumuiya ambapo italazimika kuwasilisha kusudio la kujitoa kwenye mkutano mkuu wa jumuiya utakaoongozwa na rais wa Jumuiya ya Ulaya.
ii). Uingereza na Jumuiya ya Ulaya kukubaliana masharti na vifungu vitakavyowezesha Uingereza kujitoa. (Hapa ni kuangalia kama kuna asilimia za Uingereza kulipwa au kulipa kutokana na wao kujitoa). Kumbuka Uingereza wataendelea kuwa ndani ya jumuiya kwa miaka miwili zaidi pasipo kuchangia au kushiriki mijadala ya jumuiya hiyo bali watashiriki katika makubaliano ya namna gani wanaweza kujitoa.
iii). Bunge la Jumuiya ya Ulaya litatakiwa kupiga kura ya kukubaliana au kupingana na maamuzi ya Waingereza walio wengi kutaka kujitoa. Bunge hilo lina wajumbe 748 kutoka nchi zote wanachama wa jumuiya, 73 toka Uingereza na 675 toka nchi nyingine wanachama. (Hapa kifungu cha 50 cha mkataba hakiweki bayana kama wabunge toka nchi iliyojiondoa wataruhusiwa kupiga kura ama la). Vilevile kifungu hiki hakielezi bayana namna gani nchi husika inaweza kupitisha maamuzi ya kutaka kujitoa japo kwa Uingereza inasemekana azimio litapelekwa bungeni liweze kupitishwa.
iv) Ndani ya kipindi cha miaka miwili Uingereza wanatakiwa wawe wamejitoa ndani ya jumuiya hiyo ambapo kifungu hicho cha 50 cha mkataba kinaruhusu kipindi hiki kuongezwa kwa makubaliano maalumu kati ya jumuiya na nchi inayojitoa. Ni wakati tu ndiyo utakaoamua ukweli iwapo hatua muhimu imekwishafikiwa yaani wananchi walio wengi wa Uingereza wamepiga kura kujitoa katika jumuiya hiyo.
Mwisho, kadri muda utakavyozidi kusonga mbele ndivyo madhara zaidi yatazidi kuwekwa wazi kutokana na ukweli kwamba jambo hili limeleta mshituko ndani ya Uingereza kwenyewe ambako David Cameron tayari amejiuzulu huku viongozi mbalimbali ndani ya EU wakikutana na wasaidizi wao kutafakari nini hatma yao ndani ya jumuiya ya Ulaya huenda jumuiya ikavunjika japokuwa Rais wa Jumuiya hiyo, Donald Tusk, ametoa tamko kuwa jumuiya haitovunjika na bado ina wanachama hai 27 na wiki ijayo watakutana na kutoa tamko rasmi juu ya kujitoa kwa Uingereza.
Comments
Post a Comment