Hatimaye Siwema wa Nay Atoka Gerezani!
Na Gladness Mallya, RISASI MCHANGANYIKO
HABARI njema! Mzazi mwenzake na
msanii wa Bongo Fleva, Emmanuel Elibariki ‘Nay wa Mitego’, Siwema Edson
aliyehukumiwa miaka miwili jela kwa kosa la kutishia kwa njia ya
mtandao, hatimaye ametoka jela.
Akipiga stori na Risasi Mchanganyiko,
Nay wa Mitego alisema katika harakati za kushughulikia ili mzazi
mwenzake huyo atoke alifanikiwa kupata mawakili wawili ambao mpaka
Jumamosi iliyopita walifanikisha zoezi la Siwema kutoka na sasa
atatumikia kifungo cha nje.
Nay wa Mitego alisema alilazimika
kupambana kwa nguvu zote si kwa sababu anataka kuwa naye isipokuwa kama
mzazi hakujisikia vizuri kuona mama wa mwanaye yuko jela wakati yeye
anao uwezo wa kufanya kitu kwa ajili ya kumsaidia.
“Kulikuwa kuna njia mbili za kufanya,
kukata rufaa au kubadilishiwa kifungo, mawakili wangu waliniambia
niwaachie wao watamaliza.
“Hivi ninavyoongea na wewe niko mbali na
mjini lakini taarifa za Siwema kutoka jela ninazo, kwa hiyo sina
maelezo mengine zaidi ya hayo ila namshukuru Mungu kwa kulifanikisha
hili,” alisema.
Aprili mwaka huu Siwema alihukumiwa
kifungo cha miaka miwili jela katika Mahakama ya Wilaya ya Ilemela
mkoani Mwanza kwa kosa la kutoa vitisho kwa kutumia mtandao.
Siwema na Nay walikuwa ni wapenzi wa
muda mrefu ambapo walifanikiwa kupata mtoto mmoja lakini akiwa bado
mchanga, Nay alimfumania mzazi mwenzake huyo na mwanaume mwingine na
hivyo kuvunja uhusiano wao huku akimchukua mwanaye huyo ambaye kwa sasa
analelewa na mama wa Nay.
Comments
Post a Comment