ALIYEKUWA BEKI WA TP MAZEMBE ATUA SIMBA
Kweli Simba wameamua, tayari beki Janvier Besala Bokungu
raia wa DRC, ametua Dar es Salaam kimyakimya ili kumalizana na uongozi
wa Msimbazi.
Bokungu ni beki wa zamani wa TP Mazembe, kama unakumbuka
vizuri ndiye walimchezesha katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika,
Simba ikakata rufaa kwenye Shirikisho la Soka Afrika (Caf), TP Mazembe
wakaondolewa mashindanoni na Simba kupata nafasi ya kucheza na Wydad
Casablanca ya Morocco.
“Tayari wametua hapa nchini na wataanza mazungumzo na
taratibu nyingine, maana Bokungu alikuwa Esperance ya Tunisia. Mimi
ninaamini atasajiliwa Simba maana kiwango chake kipo juu tu,” kilieleza
chanzo.
Caf, ilitangaza uamuzi wa kuiondoa TP Mazembe Mei 14,
2011 na mechi ikachezwa kwenye uwanja huru wa Petrojet jijini Cairo,
Misri, Simba ikatandikwa mabao 3-0, hiyo ilikuwa Mesi 28, 2011.
Bokungu yuko jijini Dar es Salaam pamoja na kiungo
mwingine raia wa DR Congo pia wakisubiri ‘kuonwa’ na makocha au watu
maalum kabla ya kusaini mkataba kama Simba wataridhika nao.
Habari za uhakika kutoka ndani ya Simba zinasema,
pamoja na Bokungu na kiungo huyo, mshambuliaji kutoka Ivory Coast,
Blagnon Frederick kutoka Africa Sports ya Ivory Coast alitarajiwa
kuwasili jana.
“Kama si jana, basi atatua kesho (leo) tayari kabisa
kuanza majaribio na kufanyiwa vipimo kama atakuwa amefuzu,” kilieleza
chanzo. Kwa kipindi hiki Blagnon ndiye mfungaji anayeongoza kwa
kupachika mabao katika ligi hiyo kwao Didier Drogba.
Comments
Post a Comment