Tanzia: Aliyekuwa Mkurugenzi wa Jiji la Dar, Wilson Kabwe Afariki Dunia
Marehemu Wilson Kabwe.
ALIYEKUWA Mkurugenzi wa Jiji la
Dar es Salaam, Wilson Kabwe amefariki usiku wa kuamkia leo nchini India
alikokuwa ameenda kutibiwa. Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Isaya Mwita
amethibitisha kutokea kwa msiba huo.
Rais John Pombe Magufuli, Aprili 19
alimsimamisha kazi Bw. Wilson Kabwe kutokana na ufisadi katika
utekelezwaji wa mikataba mitatu, inayohusu maeneo ya ukusanyaji mapato
ya Stendi Kuu ya Mabasi Yaendayo Mikoani ya Ubungo na kodi ya uegeshaji
magari katikati ya jiji na kuisababishia serikali hasara ya pesa
zaidi ya bilioni 3.
Rais Magufuli alichukukua uamuzi huo
siku ya uzinduzi wa daraja la Kigamboni, ambapo kabla ya Rais kuhutubia,
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda alitoa hotuba fupi ya
maswala kadhaa ya Mkoa wa Dar es Salaam ikiwemo ripoti ya tume
aliyounda kuchunguza utekelezwaji wa mikataba hiyo.
Kabla ya kuhamishiwa jijini Dar es
Salaam, Kabwe alikuwa ni Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza ambaye
alihamishiwa Mwanza akitokea Mbeya baada ya kutuhumiwa kwa ufisadi wa
mabilioni kadhaa jijini humo.
Taarifa zisizo rasmi zinasemekana kuwa
tangu siku ‘alipotumbuliwa’ na Rais Magufuli mbele ya halaiki ya watu,
alipatwa mshtuko ambapo alipelekwa nchini India ili kupatiwa matibabu
ambako mauti yamemkuta.
Comments
Post a Comment