Tamko la Madiwani Misungwi: Kitwanga Hakulewa Kama Ilivyopotoshwa.
Ndugu Waandishi wa habari,
Karibuni kwenye mkutano huu mfupi ambao lengo lake ni kutoa taarifa yetu
fupi kuhusu ukweli uliojificha kuhusu kitendo kilichopelekea Mh. Rais
Dk. John Pombe Magufuli kutengua uteuzi wa Waziri wa Mambo ya Ndani,
Charles Kitwanga.
Tunaamini kwa uwezo mliona kama waandishi wa habari, taarifa hii itafikia umma wa Watanzania kama ilivyokusudiwa.
UFAFANUZI
Kama mnakumbuka mnamo tarehe 20 Mei
mwaka huu, Rais Dk John Pombe Magufuli alichukuwa uamuzi wa kutengua
uteuzi wa Waziri wa Mambo ya Ndani, Charles Kitwanga ambaye pia ni
Mbunge wa Misungwi kwa kosa la kwamba Mhe. Kitwanga aliingia bungeni
akiwa amelewa.
Sisi wananchi wa Jimbo la Misungwi
tumesikitishwa sana na taarifa na uamuzi huu kwa kuwa tunaamini kuwa
kuna dhamira iliyojifika iliyopelekea Mhe Rais kufanya maamuzi haya.
Ukweli ni kwamba huu ulikuwa mpango
wenye dhamira ovu na uliogubikwa na uongo mwingi ukilenga kumchonganisha
Mbunge wetu na Mhe. Raisi uliopangwa na waovu wachache ambao wamebanwa
na Serikali hii ya Awamu ya tano kupitia wizara hiyo nyeti kwa usalama
wa nchi.
Itakumbukwa kuwa, Mhe Charles kitwanga
alinadiwa na Mhe Rais na wanaCCM na baadae kupigiwa kura kwa wingi na
wananchi wa Misungwi kwa ajili ya uwezo wake na dhamira yake njema ya
kulinda taifa letu.
Sisi wananchi wake, tunaamini katika uwexo wake, uadilifu wake na nidhamu ya kazi aliyonayo, hatuna mashaka na hili.
Baada ya kuteuliwa na Mhe Raisi kama
Waziri wa mambo ya ndani, amekuwa muadilifu na kafanya mengi katika
kuimarisha usalama na kufanya maamuzi yengi mazuri kwa maslahi ya taifa.
Hili lilimtengenezea maadui wengi
ndani ya serikali, ndani na nje ya CCM, mtandao wa dawa za kulevya,
walioachishwa kazi NIDA na Uhamiaji.
Watu hawa ndio waliochochea na
kutengeneza mkakati wa kumchafua Mhe Kitwanga na walikuja dodoma
kuhakikisha dhamira yao ovu inatimia.
USHAHIDI WETU
Miongoni mwetu tulikuwa mjini Dodoma
pamoja na madiwani wa Jimbo la Misungwi ambao tulikwenda kumtembelea
Mbunge wetu bungeni, tulizungumza mengi kwa ajili ya jimbo letu na
katika kikao chetu hapakuwa na chembe ya kilevi chochote na hata kesho
yake alipoinga bungeni alikuwa mzima wa afya ya kimwili na akili timamu
na tunawahakikishieni kuwa Kitwanga hakuwa amelewa.
Ndugu waandishi wa habari asubuhi ya
tarehe 20 tulielekea bungeni kwa mwaliko wa Charles Kitwanga, tukiwa
sehemu ya mualiko uliowajumuisha Madiwani wa jimbo lake tukiwa
tumeambatana naye tukaingia ndani ya ukumbi wa bunge,tukashuhudia
anajibu swali, baada ya kujibu swali la mbunge Sakaya, tulitoka nje na
kupiga picha na madiwani wote wa Misungwi waliokuja kumtembelea Dodoma.
Baada ya zoezi la kupiga picha
kukamilika pale nje ya ukumbi wa Bunge, tulitoka na kuelekea Chuo Kikuu
cha Dodoma (UDOM) kwa lengo la kututembeza maeneo yote ya Dodoma, lakini
ilipofika jioni wakati tukirejea nyumbani tukiwa naye, ghafla tukaona
habari zikisambazwa kwenye mitandao ya kijamii kuwa Waziri Kitwanga
amevuliwa uongozi kwa kuwa alionekana na Waziri Mkuu akiwa amelewa.
Ndugu wanahabari, tulishangazwa wote
kwani tulikuwa tumekaa naye pale nyumbani kwake Dodoma (site 2) tukipata
chakula cha usiku, alionekana kutoaamini na hata madiwani pia na
wengine ambao tulikuwepo hapa nyumbani kwake hatukuamini.
Tunachosema ni kwamba waziri Kitwanga hakulewa kama ambavyo imepotoshwa, bali ulikuwa ni mkakati wa kumchafua na kuhakikisha anavuliwa wadhifa wake ili watu hawa waendelee kufanya maovu yao.
Mtandao wa dawa za kulevya, pamoja na
wale waliokuwa wanamshutumu kwamba amehusika kuondolewa kwao kazini
wakiwemo Watu wa NIDA, Mbunge wa Jimbo la Chalinze, Ridhiwani Kikwete,
Mfanyabiashara Said Lugumi pamoja na kundi mafisadi waliokwapua
mabilioni ya fedha NSSF.
Pia na baadhi ya wabunge wa CCM na
Upinzani ambao walikuwa hawafurahishwi na kasi ya utendaji kazi wa
Kitwanga katika Wizara ya Mambo ya ndani.
Kwa niaba ya wananchi wenzetu
tunamuomba na kumtahadharisha Mhe. Rais awe makini na makundi la
wafanyabiashara wa madawa ya kulevya, pamoja na lile kundi la
wanamtandao masalia ndani ya CCM na serikalini na kwenye vyombo nyeti
vya ulinzi na usalama, ambayo kwa ujumla yalikuwa na mkakati kabambe wa
kuhakikisha wanamtenganisha na kumpotosha Mhe Raisin a kumjaza habari
zisizo za kweli.
Ndugu waandishi wa habari,
kilichotushangaza zaidi baada tu ya Kitwanga kuvuliwa madaraka yake ya
uwaziri, kuna watu walianza kufanya sherehe wakishangilia hususani wale
waliovuliwa madaraka NIDA pamoja na NSSF,Uhamiaji na wale wanaotuhumiwa
kuhusika na madawa ya kulevya.
Ndugu waandishi wa habari, tunajua
namna kundi la Said Lugumi, Ridhiwani Kikwete na kampuni yao walivyokuwa
wanadhamini kwa mbinu za kifedha katika vita hii ya kitwanga ili
aondolewe, lakini baada ya kuondolewa, wakajifanya kutoa taarifa ya
kushangazwa kuondolewa kwake,
Kitwanga amekuwa mtumishi wa serikali
akiwa mtumishi mwandamizi benki kuu Tanzania (BOT),amekuwa mbunge na
Naibu waziri kwa miaka 10,lakini hata siku moja hakuwahi kuonekana
amelewa. Ni muadilifu na ana nidhamu ya kazi, na nidhamu hii ndiyo
iliyomfanya aaminiwe na kupewa dhamana hii.
MAAZIMIO YETU
=Tunaliomba Bunge kumuomba radhi Mhe. Charles Kitwanga kwa kumdharirisha mbele ya wapiga kura wake wa Jimbo la Misungwi familia
yake pamoja na watanzania wote waliokuwa wanaamini utendaji wake
kupitia video iliyochezewa na wataalamu wa IT katika studio za Bunge ili
kufanikisha lengo la kumuonyesha Kitwanga kuwa alikuwa amelewa bungeni.
=Tunamuomba Waziri Mkuu, Kassim
Majaliwa ambaye ndiye Kiongozi Mkuu wa Serikali bungeni atoe uthibitisho
wa kikemia unaotanabaisha wazi kama Kitwanga alikuwa katumia kilevi
wakati akiwa bungeni maana hakuna kipimo chochote kilichofanyika
kudhibitisha uvumi huu.
=Tunaliomba Bunge lifanye uchunguzi na
kubaini wale wote waliosambaza ile video inayoonyesha Kitwanga akiwa
anaongea na kuonekana amelewa wakati kiuhalisia hakulewa na alijibu
maswali yote vizuri
=Tunaliomba Bunge kuchunguza idara ya
habari ya Bunge pamoja na studio ile ya Bunge ambao wamehusika na
kuhariri ile picha ya video iliyokuwa inasambazwa kwenye mitandao ya
kijamii.
=Tunahoji uhalali wa kumvua mtu
madaraka kwa sababu ya ulevi bila uthibitisho wa daktari ambaye kisheria
ndiye mwenye mamlaka hayo kugundua kilevi cha mtu.
= Tunaomba Watanzania wote
waliosikitishwa na taarifa hizi wajue tu kwamba ile video ambayo imemtia
hatiani Kitwanga ilihaririwa kwa ustadi mkubwa kupitia wafanyakazi wa
Bunge ambao wanapitia zile asadi za bunge pamoja na baadhi ya
wafanyakazi wa serikali kwenye vyombo vya ulinzi na usalama ambao
hawakupenda kitwanga aendelee kuwa pale ,kwa nia ya kumhujumu na sasa
wanasema kwenye vyombo vya habari ili kuhalalisha uhujumu huo.
=Tunaomba mamlaka ya mawasiliano
Tanzania (TCRA) kuangalia picha zinazosambazwa kwenye mitandao ya
kijamii dhidi ya Mhe Mbunge wa Misungwi ambazo zinaonekana kumchafua
wachukue hatua dhidi ya watu hao kwani kisiasa zinaendelea kumchafua na
kumharibia kwa wapigakura wake,familia yake,mama yake mzazi ,ndugu zake .
=Tunajiandaa kuchukua hatua kwa Bunge za kisheria kama watashindwa kuthibitisha tuhuma hizo
dhidi ya Charles Kitwanga ambazo tunaamini zimetengenezwa kwa maslahi
ya makundi yanayompinga ndani ya Serikali wakiwemo mtandao wa dawa za
kulevya.
Pia tunamuomba Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania kuwa makini kundi la wanamtandao walio ndani ya
serikali ambalo linaongozwa wahafidhina wasio taka mabadiliko ndani ya
serikali .
Imeandaliwa na madiwani wa Jimbo la
Misungwi pamoja na wakereketwa wa jimbo hilo.Baraka Kingamkono,Gaudency
Tungaraza na IDDY Majumuisho.
Asanteni na Mungu awabariki
Comments
Post a Comment