Sumaye Amkejeli Rais Magufuli kwa kazi anayofanya
FREDERICK Sumaye, Waziri Mkuu Mstaafu ameeleza kushangazwa na
Serikali ya Rais John Magufuli kupenda kusifiwa zaidi na kuchukia
kukosolewa
Sumaye bila kumtaja jina Rais Magufuli ameleza kushangazwa na hatua
ya serikali kuminya uhuru wa habari na kwamba, kufanya hivyo kunalenga
kuficha madudu yanayofanywa na watendaji wake.
“Wapowatawala ambao hawapendi kusemwa lakini wanapenda sana
kusifiwa. Kiongozi mwenye tabia ya udikteta hataki kusikia kingine zaidi
ya sifa zake tu.
“Huyo ni mtu hatari na katika nchi ya namna hiyo hakuna uhuru wa
habari wala uhuru wa kutoa maoni kwa woga wa kupotezwa kusikojulikana,” amesema Sumaye.
Akizungumza leo na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam katika
maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari yaliyoratibiwa na
Chama cha Waandishi wa Habri za Siasa (TAPOREA), Sumaye amesema,
serikali inakiuka Katiba ya nchi.
Amesema, serikali yoyote inayopambana na vyombo vya habari na
kuminya uhuru wa kufanya kazi zao huwa ina tatizo kwa upande wa
wanaotawala.
Akitolea mfano wa hatua ya serikali kuzuia matangazo ya moja kwa
moja ya bunge Sumaye amesema, kwa kufanya hivyo serikali imevunja
Katiba.
“Unapoondoa matangazo ya moja kwa moja ya vipindi vya Bunge,
kwanza ni kuvunja katiba. Ibara ya 18 (d) ya Katiba inasema, kila mtu
ana haki ya kupewa taarifa wakati wote.
“Kwa kuzuia Bunge kuoneshwa ‘live’ (moja kwa moja) wewe serikali
unataka kutoa taarifa ya Bunge kwa wakati unaoutaka na kwa taarifa
unayoitaka wewe,” ameeleza Sumaye.
Kuhusu sababu iliyotolewa kwamba, matangazo hayo yanatumia gharama ya Sh. 4 bilioni amesema haina mashiko.
Sumaye amesema, hata kama matangazo hayo yatarushwa na ofisi za
bunge bado, gharama zitaongezeka zaidi kwa sababu Bunge litahitaji
kununua mitambo pamoja na kuajiri wafanyakazi wake.
Sumaye amesema, serikali yenye demokrasia ya kweli lazima ikubali wananchi wake kutoa maoni.
“Serikali yoyote yenye utawala bora, ingependa mambo yake
inayoyafanya kwa ajili ya wananchi wake mambo hayo yajulikane kwa
wananchi hao.
“Ukiona serikali inaficha mambo yake lazima kuna mambo wanayoyafanya ambayo hayafai na wasingependa jamii ijue,” amesema Sumaye.
George Maziku, Mkurugenzi Mtendaji wa TAPOREA amezungumzia ripoti
ya hali ya uhuru wa waandishi wa habari na uhuru wa vyombo vya habari
kimataifa, iliyotolewa na Shirika la Waandishi wa Habari Wasio na Mipaka
lenye Makao Makuu yake nchini Ufaransa haipendezi.
Amesema, ripoti hiyo inaonesha kuwa, katika miaka 10 iliyopita
zaidi ya waandishi wa habari 800 kutoka mataifa mabalimbali duniani
wameuawa wakiwa wanatekeleza kazi zao.
“Kitisho kingine kwa uhuru wa vyombo vya habari nchini ni
utamaduni mpya ulioasisiwa na kuimarishwa na watawala wa sasa na
kuvishinikiza vyombo vya habari kutomkosoa Rais John Magufuli na
serikali yake.
“Matokeo yake, vyombo vingi vya habari nchini vimelazimika kuandika habari za kumfurahisha Rais Magufuli,” amesema Maziku
Comments
Post a Comment