RAIS MAGUFULI AONGOZWA KUPIGWA JUJU,VIGOGO WAHAHA KILA KUKICHA
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Pombe Magufuli ‘JPM’
Mwandishi wetu, Amani
DAR
ES SALAAM: Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Pombe
Magufuli ‘JPM’, huenda ndiye mtu anayeongoza kwa kupigwa juju kwa
waganga wa kienyeji kuliko mtu yeyote nchini kwa sasa, Amani linakuja na ushuhuda.
Sangoma
mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Shark Abdullah ‘Kishapu’, akipiga
simu kutoka jijini Tanga mwanzoni mwa wiki hii, aliliambia gazeti hili
kuwa katika miezi ya hivi karibuni, amekuwa akipata wateja, wakiwemo
wafanyabiashara na watumishi wa umma wakimtaka kumpunguza kasi ya
utendaji kiongozi huyo, wakisema inawaathiri.
“Sikiliza
ndugu mwandishi, mimi hapa ni mganga wa kienyeji, nataka nikupe habari.
Kuna watu wengi sana wanakuja hapa kwangu kutaka niwakinge na
tumbuatumbua ya Magufuli, wengine wanataka nifanye ninavyoweza kumfanya
asiweze kutekeleza majukumu yake.
“Nimewapokea
wafanyabiashara na hata viongozi wakubwa, wanataka utumbuaji wa majipu
usiwapitie, wengine wana madhambi ambayo wanataka yasahaulike ili
wasalimike, yaani nakuambia hali ni mbaya,” alisema mganga huyo.
Alipoulizwa
kama anawafanyia kama wanavyomtaka afanye, alisema anachokifanya yeye
ni kuwapa dawa zinazoweza kuwakinga dhidi ya watu wenye nia mbaya
kichawi, lakini si kumroga Rais Magufuli.
Madai
ya sangoma huyo yanafanana na Shazoe Mustafa, aliyepiga simu miezi
michache iliyopita kutoka Bagamoyo, Pwani ambaye alisema vigogo wengi
serikalini, wakiwemo wabunge wamekuwa wakienda kwake kwa ajili ya
‘kumchezea’ Rais Magufuli.
“Kuna
wabunge fulani walikuja hapa na kusema nifanye ninavyoweza ili rais
awape ulaji. Walisema wanataka uwaziri. Yupo kigogo mmoja wa shirika la
umma ambaye alikuwa na hofu ya kutumbuliwa, naye akasema niweke ukungu
ili Rais Magufuli asione jina lake. Kila anayekuja kwangu siku hizi ana
hofu na kutumbuliwa,” alisema Shazoe.
Hata
hivyo, wakati waganga hao wakipata wateja wengi wanaotaka kinga dhidi
ya utumbuaji, waumini wa dini zote wamekuwa hawalali, wakisali na
kuswali kuomba ili Mwenyezi Mungu amlinde Rais Magufuli, kwa vile kazi
yake ni nzito, yenye maadui wengi.
ASKOFU
na Nabii Nicolaus Suguye wa Huduma ya Neno la Upatanisho (WRM),
Matembele ya Pili- Kivule, Dar aliliambia gazeti hili kuwa wamekuwa
wakifanya maombi kila mara kwa ajili ya kumuombea ulinzi Rais Magufuli.
“Mara
kwa mara tumekuwa na ibada maalum ya kumuombea rais ili pepo wabaya
wakae naye mbali. Tunajua vita anayopigana ni kubwa na hatari, binadamu
hawezi kumlinda binadamu mwenzake. Sisi tunataka Mungu ndiye afanye kazi
hiyo, ndiyo maana tunakesha kwa maombi,” alisema Nabaii Suguye
Daniel
Rashid, Mchungaji wa Kanisa la Assemblies of God, Tegeta naye alisema
kwa pamoja, waumini wote wamekubaliana kutenga muda maalum wa kumuombea
ulinzi kwa malaika ili waifanye kazi ya kuhakikisha kiongozi huyo mkuu
wa nchi anakuwa salama.
“Rais
Magufuli anafanya kazi kwa manufaa ya wengi, wachache hawapendi na
bahati mbaya, hawa wachache ndiyo wenye nguvu, wako serikalini na
mitaani, tunajua hatari iliyo mbele yake, ndiyo maana tunamtanguliza
Mungu, ni Mungu tu ndiye anaweza kugeuza mioyo ya wahalifu,” alisema.
Licha
ya wachungaji hao, pia viongozi wa Kiislamu kutoka misikiti mbalimbali
nchini nao wanadaiwa kutenga muda maalum kwa ajili ya kusoma dua ya
kumlinda Rais Magufuli, kwani utendaji wake una faida kwa wanyonge wote
wa Tanzania.
Juzi,
gazeti hili lilimpigia simu Shehe Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhadi
Musa Salum ili kumuuliza kuhusu hilo kwa upande wake lakini simu yake
iliita bila kupokelewa.
source:GPL
Comments
Post a Comment