Kangi Lugola Afurahia Sefue Kutumbuliwa…..Ataka Majipu Sugu Wizara ya Kilimo Yaliyoota Sehemu Nyeti Yatumbuliwe
Mbunge wa Mwibara (CCM), Kangi Lugola jana alichangia Bajeti ya
Wizara ya Kilimo kwa hisia kali huku akimpongeza Rais John Magufuli kwa
kumtumbua Katibu Mkuu Kiongozi.
Ingawa hakumtaja kwa jina, Balozi Ombeni Sefue ndiye Katibu Mkuu
Kiongozi aliyeondolewa na Rais Magufuli Machi mwaka huu bila kubainisha
sababu ikielezwa kwamba angepangiwa kazi nyingine.
Lugola alisema Rais Magufuli ameonyesha kwa vitendo kuwa anamuenzi
Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere kwa kauli yake kuwa Ikulu ni
mahali patakatifu.
Mbunge huyo alitoa kauli hiyo Bungeni mjini Dodoma wakati
akichangia hotuba ya Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Mwigulu Nchemba.
Lugola alisema kwa kuwa alikuwa akichangia kwa mara ya kwanza
bajeti ya Serikali ya Awamu ya Tano, ni vyema akampongeza Rais kwa namna
anavyotumbua majipu kwa ujasiri na bila kupepesa macho.
Lugola akirejea kauli inayosema “kama unataka mali utaipata
shambani”, alimtaka Waziri Nchemba kutumbua majipu katika wizara yake.
“Hatuwezi kupata mali shambani kama hutatumbua majipu kwenye
wizara yako ambayo yameota sehemu nyeti .. Rais ametumbua jipu la
watumishi hewa. Wizara ya Kilimo ina wakulima hewa na ni jipu ambalo
unatakiwa ulitumbue nchi nzima.”
Huku akiungwa mkono na baadhi ya wabunge alisema vocha za pembejeo
kwa wakulima ni jipu akisema baadhi ya watumishi wanasajili wakulima
hewa na wengine wakiwa ni marehemu na Serikali inaendelea kuwalipa.
Huku akiwataja baadhi yao kwa majina, Lugola alitoa mfano wa kata
moja jimboni kwake ambako wakulima hewa wamelipwa vocha zenye thamani ya
Sh46.3.
Alisema jipu jingine ni mbegu za pamba aina ya Quton ambazo hazioti
akisema zimelalamikiwa na wabunge lakini mwekezaji anakumbatiwa. “Hili
ni jipu ikiwezekana ukitoka hapa ukatumbue jipu hili.”
Mbunge ahoji kilimo cha mirungi
Mbunge wa Same Mashariki (Chadema), Naghenjwa Kaboyoka aliitaka
Serikali kuzungumza na Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta, ili kujua ni kwa
nini wamehalalisha kilimo cha mirungi.
Alisema Rais huyo ametoa Dola za Marekani milioni mbili, sawa na
Sh4 bilioni za Tanzania ili kusaidia ustawi wa kilimo hicho, ambacho kwa
Tanzania ni kosa la jinai kulima na kusafirisha.
“Rais Kenyatta ameruhusu kilimo hiki tukizingatia kwamba tuko
Jumuiya ya Afrika Mashariki. Tutahakikishaje kwamba hii mirungi
haitaingia kwetu?” alihoji.
Alimtaka Waziri wa Kilimo awasiliane na Kenya ili kujua sababu za
kuruhusu kilimo hicho na namna ambavyo wataweza kudhibiti kisilete
madhara Tanzania.
Ataka marufuku ya nyavu
Mbunge wa Kigoma Kaskazini (CCM), Peter Serukamba aliitaka Serikali
kupiga marufuku uzalishaji wa nyavu za kuvulia samaki ambazo
haziruhusiwi badala ya kuwakamata wavuvi. “Kwa nini nguvu kubwa
isielekezwe katika kudhibiti uzalishaji wa hizi nyavu. Mpige marufuku
uzalishaji wake badala ya kwenda kuzikamata kwa wakulima na kuzichoma,”
alisema Serukamba.
Wizara ihame Dar
Mbunge wa Nchemba (CCM), Juma Nkamia alitaka makao makuu ya Wizara
ya Kilimo yahame kutoka jijini Dar es Salaam na kwenda katika mikoa
yenye mifugo mingi.
Pia aliishauri Serikali kujenga mazingira yatakayovutia kujengwa
kwa viwanda vya nyama kwenye mikoa yenye mifugo mingi badala ya
kusafirisha mifugo hai umbali mrefu.
Msimamo wa kambi ya upinzani
Akiwasilisha hotuba ya msemaji mkuu wa kambi rasmi ya upinzani
Bungeni, waziri kivuli wa wizara hiyo, Magdalena Sakaya (CUF), alisema
itaendelea kulaani ubakaji wa demokrasia Zanzibar.
“Tutaendelea kulaani kubakwa kwa demokrasia kulikotokea huko
Zanzibar katika Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba mwaka jana,” alisema.
Akizungumzia wizara hiyo, Sakaya alisema taarifa ya Mdhibiti na
Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) inaonyesha asilimia 75 ya
machinjio nchini hayana huduma na vifaa vinavyozingatia usafi na ubora
wa nyama.
“Hali hii si nzuri hata kidogo kwa kuwa magonjwa ya kuambukiza
nchini hayataisha kutokana na uchafu uliopo katika machinjio ambayo
yanalisha maelfu ya walaji wa nyama,” alisema.
Pia kambi hiyo imeitaka Serikali kupitia upya mikataba yote
iliyoingiwa na wawekezaji katika mashamba makubwa kuona kama ina
masilahi kwa nchi.
Kambi hiyo ilisema kati ya Sh60.3 bilioni ambazo ziliidhinishwa na
Bunge katika mwaka fedha 2015/2016, Sh19.3 zilizotengwa kwa ajili ya
maendeleo hazikupokewa.
Alisema taarifa ya wizara inaonyesha kuwa hadi Machi 31,2016,
wizara hiyo ilikuwa haijapokea hata shilingi moja, hivyo akasema hata
mipango inayotaka kutekelezwa sasa itakuwa ni ngonjera.
“Hii mipango ambayo ipo kwenye taarifa ya wizara na ile
iliyotolewa katika hotuba ya Waziri Mkuu ni ngonjera tu za kuwafariji
wadau lakini ukweli sekta ya mifugo na uvuvi iko mahututi.
“Kambi rasmi ya upinzani inaona kwamba kukua kwa sekta hizi itakuwa
ni ndoto kwani hali halisi ni kwamba hakuna fedha za kuendeleza malengo
yaliyowekwa katika awamu ya kwanza,” alisema.
Aliikumbusha Serikali kuwa inatakiwa kulipa Sh2 bilioni
zilizotokana na amri ya Mahakama kutokana na kesi ya kukamatwa kwa meli
ya uvuvi maarufu “samaki wa Magufuli.”
Alisema Serikali inawajibika kulipa fedha hizo kutokana na kufanyika kwa uamuzi ambao haukuzingatia sheria
Comments
Post a Comment