Huu ndiyo ukweli wa Kitwanga Kuhusu Ulabu
DAR ES SALAAM: Ajali ya kisiasa! Gumzo
kuhusu Rais John Pombe Magufuli ‘JPM’ kumtumbua Waziri wa Mambo ya
Ndani, Charles Muhangwa Kitwanga (56) kwa madai ya kuingia bungeni akiwa
‘amechangamka’ bado liko vinywani mwa Wabongo huku sasa, upande wa pili
wa hali hiyo ukijulikana, Ijumaa Wikienda limechimba.
Ijumaa iliyopita, JPM alitengua uteuzi
wake akidaiwa kuingia mjengoni akiwa amelewa hivyo kukosa umakini wakati
akijibu maswali ya wizara yake.
Habari zilizonaswa na Wikienda zinasema
Kitwanga ni mnywaji lakini si kwa kiwango cha kukosa umakini kiasi cha
kushindwa kutiririka vyema kwenye kujibu maswali, ila siku hiyo
ilisababishwa na msongo.
MSIKIE HUYU
“Mimi sikatai ndiyo, Kitwanga anapiga
ulabu, lakini yule jamaa yuko makini sana. Huenda siku ile alizidisha
lakini naijua sababu.
“Unajua siku za hivi karibuni, jamaa
amekuwa akiandamwa sana na baadhi ya wabunge kuhusu sakata la Kampuni ya
Lugumi na ufungwaji wa vifaa vya kutambua alama za vidole vya wahalifu.
“Alishajieleza sana kuwa, Kampuni ya
Lugumi haikuwa na mkabata na Kampuni ya Infossy, lakini wabunge wapi!
Kila siku walikuwa wakitaka jamaa ajiuzulu licha ya kwamba sakata la
Lugumi liko kwenye kamati ya bunge,” kilisema chanzo hicho.
LEMA AKANUSHA, AWABEBESHA LAWAMA WATU WATATU
Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema),
Godbless Lema ni miongoni mwa wanasiasa waliokuwa wakimwandama sana
waziri Kitwanga wakimtaka ang’atuke nafasi yake hiyo kwa sababu ya
kuhusishwa na Lugumi.
Akizungumza na gazeti hili Jumamosi
iliyopita siku moja baada ya JPM kumtumbua, Lema alikanusha vikali madai
hayo akisema si ya kweli kwa vile yeye na mtumbuliwaji huyo ni
marafiki.
“Ni kweli aliingia bungeni akiwa
‘amechangamka’ au amekunywa pombe kama utenguzi ulivyosema na mimi
sitarajii mbunge aingie bungeni akiwa amelewa.
“Lakini mimi naamini kabisa wanaotakiwa kubebeshwa mzigo ni wasaidizi wake.
“Ninavyojua waziri ana wasaidizi watatu,
kuna katibu mkuu, dereva na mtu mwingine (katibu wa mbunge). Ina maana
hawa wote hawakumshauri waziri baada ya kuona hali yake? Walipaswa kujua
kila kitu juu ya bosi wao ili wamshauri kwa sababu kulewa kazini tena
bungeni ni kinyume na maadili ya utumishi,” alisema Lema.
WALIVYOSEMA WANASIASA
Kwa upande wao, baadhi ya wanasiasa
waliozungumza na Wikienda walisema rais amethibitisha kuwa katika
serikali yake hataki uzembe kwa watendaji wake hasa wale ambao amewateua
mwenyewe.
“Achana na masuala ya kashfa ya mkataba
wa Kampuni ya Lugumi. Unajua kuna baadhi ya watu wanadai hiyo ndiyo
imemng’oa kwa sababu anahusishwa nayo, lakini ninavyojua, hilo rais
hawezi kuliingilia kwani lipo chini ya Kamati ya Bunge na ni mhimili
tofauti,” alisema mwanasiasa mmoja aliyeomba hifadhi ya jina na
kuongeza:
“Tusitafute visingizio, na uzuri zile
video zake akijibu maswali bungeni zipo kwenye mitandao ya kijamii.
Zinaonesha kila kitu, kusitokee mtu akadhani kuwa JPM hajui
kinachoendelea bungeni. Wewe unadhani ni nani anaweza kuthubutu kufanya
hivyo halafu akasalimika kwa Magufuli?”
Baadhi ya wafanyakazi wa Wizara ya Mambo
ya Ndani waliozungumza na gazeti hili kwa sharti la kutochorwa majina
yao gazetini, walisema;
“Kusema ukweli, Kitwanga ukiachia mbali
hiyo pombe iliyotajwa kule bungeni, lakini wauza unga wanamjua na
hawatamsahau. Jamaa amekamata wengi tena bila kuogopa wala kupendelea,”
alisema mmoja wa wafanyakazi hao.
“Mimi siikosoi hatua ya Rais Magufuli
maana lazima kuwepo kwa utaratibu wa wakati wa kazi na wakati usio wa
kazi, lakini kwa wauza unga kama wameshinda, Kitwanga amewakamata wengi,
sasa sijui atakayekuja,” alisema mwingine.
“Jamaa anawakamata sana. hajali wewe
unajuana na nani au na nani, ukishukiwa tu ndani. Naamini wauza unga
wataisha kwa Kitwanga,” alisema mtumishi huyo.
KITWANGA HAPOKEI SIMU
Juzi alipotafutwa Kitwanga ambaye pia ni
Mbunge wa Jimbo la Misungwi (CCM) ili kujua amepokeaje utenguzi huo wa
rais, simu yake iliita bila kupokelewa.
Comments
Post a Comment