Harambee ya Mwanafunzi Aliyepoteza Uono Akiwa Chuo Kufanyika leo
Dar es Salaam: Jumuiya ya Chuo
Kikuu cha Mzumbe leo itafanya harambee chuoni hapo ya kumchangia
mwanafunzi Bernadetha Msigwa kwa ajili ya matibabu ya macho ili aweze
kuona tena.
Harambee hiyo itajumuisha wanafunzi, walimu pamoja na watu mbalimbali ambao wameamua kumsaidia binti huyo.
Mhadhiri wa Kitivo cha Utawala cha chuo hicho, Aloyce Gervas alisema harambee hiyo itafanyika kuanzia saa mbili asubuhi.
Alisema baada ya kubaini kuwa tatizo
lake lina tiba ndipo walipoanza kampeni kupitia mitandao ya kijamii:
“Tunashukuru kampeni ya Kipepeo inayoendeshwa na Clouds Media na
wasamaria wengine wote kwa kupokea wito wetu wa kumchangia Bernadetha.
Tunatoa shukrani zetu kwa Rais John Magufuli kwa kutoa mchango wake
baada ya kuona kipindi cha Kipepeo katika kipindi cha ya 360 cha kituo
hicho.
Akimzungumzia mwanafunzi huyo, Gervas
alisema: “Kutokana na hali yake, huwa tunampatia mtihani wa kujieleza,
hapo ndipo utajua ni mwanafunzi mwenye akili na ambaye ana malengo
makubwa ya kufika mbali pamoja na nia kubwa ya kutaka kuona.”
Bernadetha (21) ambaye ni mwanafunzi wa
mwaka wa tatu wa kozi Shahada ya Rasilimali Watu, kwa sasa anaendelea na
vipimo katika Hospitali ya Muhimbili.
Alijiunga na Chuo Kikuu Mzumbe mwaka
2011 baada ya kumaliza kidato cha sita katika Shule ya Sekondari ya
Wasichana Kilakala, Morogoro.
Akizungumza na Mwananchi, alisema alikuwa mzima wa afya kipindi hicho, alikuwa anaona na kufanya kila kitu mwenyewe.
“Mabadiliko yalianza mwanzoni mwa mwaka 2014 muhula wa mwisho baada ya kuanza kusumbuliwa na maumivu makali ya kichwa.”
Alisema alipata matibabu ya kichwa na
macho katika hospitali mbalimbali na hatimaye katika hospitali maalumu
ya macho, lakini haikusaidia.
“Macho yangu yalianza kupoteza nuru ya
kuona kidogokidogo. Hata hivyo, mwishoni mwa mwezi wa tano, 2014 ilikuwa
mara ya mwisho kwangu kuona.
“Naamini naweza kuona tena, ila hata kama sitaona, nitakushukuru kwa moyo na mchango mkubwa ninaoupata,” alisema.
Meneja wa kipindi cha 360 cha Clouds TV,
Hudson Kamoga alisema jana kuwa mpaka sasa michango inaendelea vizuri
na jumla yake itapatikana baada ya harambee ya leo.
Comments
Post a Comment