BREAKING NEWZ:Vurugu Tena Bungeni, Ni Kuhusu Wanafunzi 7000 wa UDOM Waliotimuliwa.
Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania bila kujali itikadi ya vyama vyao, leo wametoka nje
ya ukumbi wa bunge hilo baada ya Naibu Spika, Tulia Ackson kukataa
kujadiliwa kwa kauli ya serikali kuhusu wanafunzi 7000 wa Chuo Kikuu Cha
Dodoma (UDOM) waliosimamishwa.
Chuo Kikuu cha Dodoma kwa kutekeleza
agizo la Maziri wa Elimu, Prof. Joyce Ndalichako hivi karibuni
kiliwasimamisha masomo zaidi ya wanafunzi 7,000 wa kozi maalumu ya
ualimu wa sayansi kwa ngazi ya stashahada na kuwataka waondoke chuoni
hapo mara moja.
Wabunge waliwasilisha hoja kwa Naibu
Spika, Tulia Ackson ili kulishinikiza bunge kuijadili kauli ya serikali
kuhusu wanafunzi hao waliotimuliwa ambapo Naibu Spika alikataa
kusikilizwa hoja hayo ndipo vurugu zikaanza na kumlazimu Naibu Spika
kufunga Kikao cha Bunge kilichokuwa kikiendelea na kuwaamuru wabunge
wote watoke nje.
Juzi, lilitolewa tangazo chuoni hapo likiwataka wanafunzi hao
kuondoka kuondoka chuoni hapo. Tangazo hilo lilieleza kuwa kutokana na
matatizo yaliyopo katika ufundishaji wa stashahada hiyo, Serikali
kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi
imeamua wanafunzi hao kurejea majumbani na wataelezwa mustakabali wao
“mapema iwezekanavyo”.Makamu Mkuu wa chuo hicho, Profesa Idrisa Kikula alitafutwa vyombo vya habari na alipotakiwa kufafanua suala hilo, alisema kwa ufupi kuwa suala hilo lipo lakini akaelekeza apigiwe simu Ofisa Uhusiano wa chuo hicho, Beatrice Baltazal kwa maelezo zaidi.
Baltazal alipotafutwa alisema
kusimamishwa kwa wanafunzi hao kulitokana na agizo la Serikali na
wametakiwa kulitekeleza. Kuhusu lini na nini hatima ya wanafunzi hao,
alisema bado hawajui hadi hapo watakapoelekezwa vinginevyo.
Hata hivyo, kulikuwa na malalamiko kwa wanafunzi hao juu ya namna
walivyopewa taarifa za kusimamishwa masomo yao kwa ghafla na kutakiwa
kuondoka.Kozi ya stashahada ya ualimu wa sayansi, ilianzishwa maalumu kwa agizo la Rais Jakaya Kikwete kwa lengo la kuziba pengo la walimu wa sayansi na ilikuwa inatolewa UDOM pekee. Waliokuwa na sifa za kujiunga na kupewa mikopo ni wanafunzi waliomaliza kidato cha nne na kufaulu vizuri masomo ya sayansi.
Wanafunzi hao waliokuwa wamekopeshwa na Serikali wamesimamishwa siku mbili baada ya wenzao zaidi ya 480 wa Chuo Kikuu cha St. Joseph kusimamishwa baada ya kubainika hawakuwa na sifa za kudahiliwa.
Comments
Post a Comment