Polisi Dar wamchunguza Zari!
Zarina Hassan ‘Zari’ au mama Tiffah.
DAR ES SALAAM: Kufuatia kamatakamata ya wafanya-biashara wanaodaiwa
kujihusisha na madawa ya kulevya ‘unga’ Bongo, kuna madai kwamba, Jeshi
la Polisi Tanzania linawachunguza upya mastaa wanaoingia na kutoka kwa
kutumia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) jijini Dar
huku Zarina Hassan ‘Zari’ au mama Tiffah akitajwa kuwemo.Kwa mujibu wa chanzo chetu, hatua hiyo imekuja baada ya jeshi hilo kubaini ‘ingia toka’ ya mastaa hao ambao baadhi yao wamemaliza vitabu vitatu vya hati za kusafiria kwa mwaka mmoja kwa kupigwa muhuri wa uhamiaji kwa sababu ya safari.
CHANZO NI HIKI
“Mimi nawapa habari, jeshi la polisi kupitia Kikosi cha Kuzuia na Kupambana na Madawa ya Kulevya Tanzania linamchunguza Zari na mastaa wengine wanne, leo siwataji. Kisa ni safari zao za kuingia Tanzania mara kwa mara.
“Polisi wanajua kwamba Zari anakuja Bongo kwa sababu ya kumfuata Diamond (Nasibu Abdul) ambaye ni mzazi mwenzake. Ndiyo maana leo yupo Afrika Kusini, kesho Dar es Salaam.
“Lakini jeshi la polisi haliwezi kulegezea hilo eti kisa anamfuata Diamond. Linachotaka kujua ni je, kweli anamfuata Diamond au anasafirisha unga? Si kwamba wanajua anajihusisha na unga bali wanamchunguza,” kilisema chanzo hicho kutoka jeshi la polisi.
Diamond Platinumz.
POLISI NA WASHIRIKA Chanzo kikadai kuwa polisi hao wanashirikiana na
Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania na uongozi wa uwanja huo ili
kufanikisha uchunguzi wao kwa watu wanaopita mara kwa mara.MAMLAKA YA VIWANJA VYA NDEGE
Baada ya taarifa hizo, gazeti hili juzi lilipiga simu Mamlaka ya Viwanja vya Ndege kwa lengo la kutaka kuongea na bosi wao anayekaimu, Mhandisi George Sambali lakini katibu muhtasi (sekretari) wake aliyepokea simu alitaka kujua shida ya gazeti kabla ya kuunganishwa na bosi wake huyo.
Sekretari: “Mamlaka ya Viwanja vya Ndege hapa, nikusaidie nini?”
Amani: “(baada ya kujitambulisha) nataka kuongea na mkurugenzi.”
Sekretari: “Kwa shida gani ndugu?”
Baada ya kuambiwa shida mwanzo hadi mwisho…
Sekretari: “Hiyo siyo hapa, piga simu namba…(anazitaja namba) za uwanja wa ndege kule.”
AMANI NA UWANJA WA NDEGE
Amani lilipiga simu JNIA na kupokelewa na sekretari aliyejitambulisha kwa jina la Joyce Batenga.
Sekretari: “Uwanja wa Ndege Dar es Salaam hapa, naitwa Joyce Batenga, nani mwenzangu?”
Baada ya Amani kujitambulisha na kuanika shida yake, dada huyo alisema:
“Ngoja nikuunganishe na Security Officer (Ofisa Usalama wa Uwanja).”
Baada ya muda, Amani lilipokelewa na ofisa usalama huyo ambaye alikataa katakata kutaja jina lake. Alipoelezwa shida ya gazeti hili, alisema:
“Sisi hapa uwanjani tunamchunguza kila mtu anayepita kutoka na anayepita kuingia. Hatuachi mtu hata mmoja.”
Amani: “Sasa hilo za Zari unasemaje, kuna ukweli wowote?”
Ofisa: “Si kila kitu cha kusema ili kiandikwe gazetini kaka. Kama unaweza njoo tuongee ana kwa ana. Tafuta muda ukifika jitambulishe tutaongea kila kitu lakini si kwenye simu.”
AMANI NA MKUU WA POLISI KITUO CHA UWANJA WA NDEGE
Baada ya hapo, gazeti lilimtafuta kwa simu, Mkuu wa Kituo cha Polisi Uwanja wa Ndege, Leocadia Marcian baada ya kusikiliza madai mpaka mwisho, alisema:
“Sawa, nimekusikia lakini mimi sasa nipo likizo na nipo safarini.”
Amani: “Nani anakukaimu?”
Mkuu wa Kituo: “Siwezi kujua, mimi niko njiani nasafiri, nipo likizo halafu si msemaji.”
AMANI NA KAMANDA WA MADAWA YA KULEVYA
Baada ya kuzungumza na wote hao, gazeti hili lilikwenda mbele zaidi kwa kuongea na Kamanda wa Kikosi cha Kupambana na Kuzuia Madawa ya Kulevya, ACP Mihayo Msikhela ambaye alipoambiwa ishu yote alisema kwa ufupi:
“Tunamfuatilia. Karibuni sana ofisini kwangu.”
Amani: “Tumetoka hapo ofisini kwako muda si mrefu, tukaambiwa upo makao makuu.”
Kamanda Mihayo: “Basi karibuni tena.”
SASA NI DIAMOND
Diamond alitafutwa kwenye simu kwa kutumia mtandao wa WhatsApp ambapo alipopatikana alisema:
“Mimi tangu nimekuwa na Zari sijawahi kumwona akiwa na mambo hayo. Watu wanasema tu. Kule Uganda waliwahi kusema lakini hakuna kitu. Ndiyo maana unamwona anadunda. Mbona yuko poa sana.”
ALIWAHI KUTAITIWA KABISA
Mbali na madai ya Zari kuchunguzwa, Juni mwaka jana, Diamond aliwahi kutaitiwa na askari wa uwanja huo kwa muda wa saa mbili akiwa na mabegi matatu.
Diamond alikumbwa na nusanusa hiyo baada ya kutua uwanjani hapo akitokea Afrika Kusini ‘Sauzi’ alikokwenda kwa shoo ambapo askari walitaka kujiridhisha kama hajabeba unga.
Source:GPL
Comments
Post a Comment