Mbunge Nusura… Akamatwe na ‘unga’ Dar

PTKamanda wa Kitengo cha Kupambana na Kudhibiti Madawa ya Kulevya, ACP Mihayo Msikhela
Na Makongoro Oging’, UWAZI
Dar es Salaam: Jeshi la Polisi Kitengo cha Kupambana na Kudhibiti Madawa ya Kulevya, wiki iliyopita nusura limnase mbunge mmoja kutoka jimbo moja lililopo katika moja ya mikoa ya pwani (jina linahifadhiwa) baada ya kumuwekea mtego kutokana na madai kwamba alikuwa akisafirisha madawa ya kulevya ‘unga’ kutoka kwenye ufukwe mmoja wilayani Bagamoyo kuelekea jijini Dar.
Taarifa zilizopatikana kutoka kwa vyanzo vyetu ndani ya jeshi hilo zinadai kuwa, msamaria mwema mmoja alivujisha siri kwa jeshi hilo kwamba, mbunge huyo amebeba unga kwenye gari lake dogo akielekea Dar ambapo bila kupoteza muda, polisi walimuwekea mtego kabambe kwenye njia ambazo alitarajiwa kupita ambapo hata hivyo, aliukwepa baada ya kubadilisha njia.
Taarifa zaidi zinaeleza kuwa, mbunge huyo alikuwa akipita usiku wa saa mbili na mzigo huo lakini inadaiwa kuwa alishtukia kwamba amewekewa mtego hivyo akabadilisha njia na kusababisha asikamatwe.
Habari zinasema kuwa, mbunge huyo amekuwa akihusishwa na biashara hiyo lakini hajawahi kukamatwa kutokana na njia anazozitumia kuendesha biashara hiyo kuwa za ujanja wa hali ya juu huku akiwatumia watu.
“Baada ya kumkosa, ilibidi polisi watawanyike lakini kwa sasa wanaendelea kumfuatilia kwa karibu, naamini akiendelea siku si nyingi atanaswa,” kilisema chanzo chetu kutoka ndani ya jeshi hilo.
Kamanda wa Kitengo cha Kupambana na Kudhibiti Madawa ya Kulevya, ACP Mihayo Msikhela (pichani) alipoulizwa na Uwazi juzi, alisema tetesi hizo amezisikia lakini hajui kinachoendelea kwa sababu ameripoti kazini hivi karibuni na kukabidhiwa ofisi na mtangulizi wake, Kamanda Kamishna Robert Boaz.
source:GPL

Comments

Popular posts from this blog