DIAMOND PLATINUMS YAMKUTA MAZITO,MASHEHE WAMJIA JUU,GUMZO KILA KONA

 
NA mwandishi wetu, Risasi Jumamosi
Dar es Salaam: Kitendo cha kuposti picha inayomuonesha akiwa ametoboa pua na kuvaa kipini kilichofanywa na staa wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ kimemfanya yamkute mazito kufuatia mashehe kumjia juu na kuwa gumzo.
Gumzo lilianza juzikati baada ya Diamond kutupia picha kwenye akaunti yake ya Instagram, ikimuonesha akiwa amevaa kipini, kama wafanyavyo wanawake, kitendo kilichoamsha mjadala mkubwa kwa mashabiki na wadau mbalimbali wa muziki wake.
Wapo waliomuunga mkono kwa maelezo kwamba hakuna mtu anayepaswa kumuingilia kwa sababu hayo ni maisha yake binafsi, huku wengine wakienda mbele kwa kuwatolea mfano mastaa wengine wakubwa duniani kama Chris Brown, Wiz Khalifa, marehemu 2Pac na wengineo kwamba nao waliwahi au wametoboa pua.
Hata hivyo, kundi jingine kubwa, lilimjia juu msanii huyo na kumtaka kuacha kuiga mambo yanayofanywa na wasanii wa Ulaya na Marekani na badala yake, awe kioo cha jamii kwa kuenzi na kudumisha mila na tamaduni za Kitanzania.
Baada ya kufuatilia sakata zima, Risasi Jumamosi liliwatafuta viongozi mbalimbali wa dini ya Kiislam ambayo Diamond ni muumini wake na kuwauliza kama kitendo hicho alichokifanya msanii huyo ni sahihi ambapo walimjia juu na kumshutumu vikali.
Ismail Yahya, shehe wa msikiti mmoja maarufu Kijitonyama, alisema: “Anachokifanya huyu bwana ni upotofu na kinyume na sheria za dini ya Kiislam. Ni makosa kwa mwanaume kutoga pua, kuvaa kipini, hereni, mikufu au kujichora tatuu. Sasa huyu bwana kafanya yote kaona haitoshi, kaamua na kuvaa kipini kabisa, ni makosa makubwa na kinyume na mafundisho ya dini.”
“Astaghafirullah! Anachokifanya huyu msanii ni makosa makubwa na kinyume kabisa na dini ya Kiislam. Atakuwa anafanya makusudi huyu kwa sababu naamini alisoma madrasa na alifundishwa kijana wa Kiislamu anavyotakiwa kuwa, iweje leo ajifananishe na mwanamke? Ni makosa makubwa kwa mwanaume wa Kiislam kutoboa pua,” alisema Ally Moshi, Shehe wa Madrasatul Nuur jijini Dar es Salaam.
Hata hivyo, meneja wa msanii huyo, Salam Sharaf alibuka baadaye kwenye mitandao ya kijamii na kumtetea Diamond kuwa picha hiyo si halisi bali ilitengenezwa.

Comments

Popular posts from this blog