BREAKING NEWZ:JPM Avunja Bodi ya TCRA, Amsimamisha Kazi Mkurugenzi Mkuu
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Dkt. John Pombe Magufuli ameivunja Bodi ya Mamlaka ya Mawasiliano
Tanzania (TCRA) na kumsimamisha kazi Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka hiyo
Dkt. Ally Yahaya Simba kutokana na kutosimamia ipasavyo Mkataba wa
utekelezaji wa mfumo wa usimamizi wa mawasiliano ya simu (TTMS), na
kusababisha nchi kupoteza mapato ya takriban shilingi bilioni 400 kwa
mwaka.
Rais Magufuli amechukua hatua hiyo leo
tarehe 26 Aprili, 2016 Ikulu Jijini Dar es salaam baada ya kufanya kikao
cha kazi kati yake na viongozi na wataalamu kutoka Wizara ya Ujenzi,
Mawasiliano na Uchukuzi, Wizara ya fedha na Mipango na Taasisi ya Kuzuia
na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU).
Tarehe 22 Machi, 2013 Mamlaka ya
Mawasiliano nchini (TCRA) iliingia mkataba na kampuni ya SGS juu ya
uwekaji, uendeshaji na uhamishaji wa mapato ya simu ambapo kampuni hiyo
ilipaswa kutekeleza vipengele vitano lakini mpaka sasa kampuni ya SGS
haijaanza kutekeleza kipengele kidogo kinachohusiana na uthibiti wa
mapato ya simu za ndani (Offnet), hali ambayo imesababisha serikali
kukosa mapato yanayokadiriwa kuwa shilingi bilioni 400 kwa mwaka.
Pamoja na kuivunja bodi ya TCRA
inayoongozwa na Profesa Haji Semboja na Kumsimamisha kazi Mkurugenzi
Mkuu wa TCRA Dkt. Ally Yahaya Simba, Rais Magufuli pia amemuagiza Waziri
wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi Profesa Makame Mbarawa Mnyaa kumteua
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka hiyo mara moja.
Aidha, Rais Magufuli amewataka Waziri
Prof. Mbarawa, Katibu Mkuu na Naibu Katibu katika wizara hiyo kuchukua
hatua mara moja ili mfumo wa ukusanyaji wa mapato ya simu kwa simu za
ndani (Offnet) uanze kufanya kazi, na nchi ipate mapato yanayostahili
kukusanywa.
“Waziri hakikisha unachukua hatua mara
moja, nataka tukusanye mapato yote ya serikali yanayostahili na sitasita
kuchukua hatua dhidi ya yoyote atakayekwamisha jambo hili” Amesisitiza
Rais Magufuli.
Gerson MsigwaKaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Dar es salaam
26 Aprili, 2016
Comments
Post a Comment