TANZANIA NA JAPAN KUANZISHA USHIRIKIANO KATIKA MATUMIZI YA TEHAMA.
Mwakilishi
Mkuu wa Shirika la Kimataifa la Maendeleo la Japan (JICA) nchini
Tanzania Bw. Toshio Nagase akimweleza jambo Katibu Mkuu wa Wizara ya
Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Faustin Kamuzora (kushoto).
Mwakilishi
Mkuu wa Shirika la Kimataifa la Maendeleo la Japan (JICA) nchini
Tanzania Bw. Toshio Nagase (kulia) akizungumza na baadhi ya watendaji wa
Wizara hiyo upande wa Mawasiliano wakiongozwa na Katibu Mkuu Wizara ya
Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Faustin Kamuzora.
Katibu
Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Faustin
Kamuzora (kushoto) akisisitiza jambo alipokutana na Mwakilishi Mkuu wa
Shirika la Kimataifa la Maendeleo la Japan (JICA) nchini Tanzania Bw.
Toshio Nagase. Bw. Toshio Nagase amekutana na kufanya mazungumzo na
Katibu Mkuu wa Wizara hiyo kuhusu namna Japan na Tanzania zinavyoweza
kushirikiana katika masula ya TEHAMA.
Picha na Aron Msigwa –MAELEZO
Na. Aron Msigwa –MAELEZO
TANZANIA
na Japan zinatarajia kuanzisha ushirikiano katika matumizi ya
Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kwa kuwaunganisha
wafanyabishara na vijana wanaojihusisha na masuala ya TEHAMA ili waweze
kunufaika na fursa zilizopo katika nchi hizo.
Hayo
yamebainishwa leo jijini Dar es salaam na Katibu Mkuu wa Wizara ya
Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Faustin Kamuzora mara baada ya
kukutana na kufanya mazungumzo na Mwakilishi Mkuu wa Shirika la
Kimataifa la Maendeleo la Japan (JICA) nchini Tanzania Bw. Toshio Nagase
ambaye alimtembelea ofisini kwake kueleza nia ya Shirika lake na nchi ya Japan kutaka kuwekeza kwenye Sekta ya TEHAMA nchini Tanzania.
Amesema
mara baada ya kukamilika kwa taratibu zote za ushirikiano katika sekta
ya TEHAMA vijana na wafanyabishara wa Tanzania wataweza kushirikiana na
vijana na wafanyabiashara kutoka Japan katika kubadilishana uzoefu na
ujuzi katika masuala ya TEHAMA na kuwawezesha kujiajiri wenyewe au
kuajiriwa ndani na nje ya nchi.
Prof.
Kamuzora amesema kuwa Tanzania na Japan kwa muda mrefu zimekuwa
zikishirikiana katika masuala mbalimbali ya maendeleo kupitia miradi ya
ushirikiano hususan ujenzi wa miundombinu na masuala ya Ufundi.
Aidha, amesema
kuwa Tanzania imekuwa ni nchi ya kuigwa duniani na kupigiwa mfano kwa
kuwawezesha wananchi kupata huduma ya kutuma na kupokea pesa kupitia
simu za mkononi na kufanya malipo mbalimbali.
“sisi
kama Serikali tunawakaribisha wenzetu wa Japan kuja Tanzania
kushirikiana nasi kuendeleza Sekta ya Mawasiliano na kuwekeza nchini
kwetu ili wananchi wetu wanufaike na maendeleo ya Sekta hii kama ambavyo
wenzetu wamepiga hatua kwa kuwa na kampuni za vifaa vya TEHAMA kama
vile kampuni ya Sony”. Amesema Prof. Kamuzora.
Amesisitiza
kuwa Serikali ya awamu ya tano chini ya uongozi wa Rais John Magufuli
imeweka msisitizo katika uanzishaji na uendelezaji wa viwanda kwa lengo
la kukuza ajira miongoni mwa watanzania na kuongeza kuwa mkakati uliopo
ni kuanzisha viwanda vya kuzalisha vifaa mbalimbali vya TEHAMA kwa kuwa
Soko bidhaa hizo lipo.
Ameongeza
kuwa Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na JICA imejipanga kuwekeza
katika Elimu,Ujuzi na Stadi kwa vijana ili waweze kutengeneza Program
za TEHAMA ambazo zinahitajika ndani na nje ya nchi hivyo kukuza uchumi
miongoni mwa vijana hao.
Kuhusu
kuwekeza katika Elimu katika masuala ya TEHAMA Prof. Kamuzora
amesisitiza kuwa hakuna nchi iliyowahi kuendelea duniani bila kuwa na
wabunifu wake wa ndani na kuongeza kuwa Tanzania sasa inao vijana wenye
uwezo wanaofanya vizuri katika Teknolojia ya Habari na Mawasiliano.
“Dhana
ya kutengeneza viwanda lazima ihusishe ubunifu wa kutengeneza Programu,
hakuna nchi iliyoendelea bila kuwa na wabunifu wa ndani tunachohitaji
sasa ni uwepo wa vijana ambao wakao tayari ” Amesisitiza Prof. Kamuzora.
Prof.
Kamuzora amesema Tanzania inazo fursa nyingi za kuwawezesha vijana
ikiwemo uanzishaji wa viwanda vidogo na vya kati vya kutengeneza
programu za TEHAMA hivyo ushirikiano ulioonyeshwa na JICA utawezesha
viwanda vya kutengeneza vifaa mbalimbali kuanzishwa kupitia wabunifu
waliopo.
“
Tanzania tunao vijana wabunifu wenye uwezo, kupitia Tume ya Sayansi na
Teknolojia ( COSTECH) wameweza kubuni na kutengeneza teknolojia
mbalimbali kusaidia shughuli za Kilimo na uhifadhi wa Maliasili hapa
nchini” Amesema.
Aidha, amesema Wizara kwa kushirikiana na JICA inafanya mpango wa kuwakutanisha wafanyabiashara;
wawekezaji; kampuni; sekta binafsi na wadau mbalimbali wa Sekta ya
Mawasiliano wa Tanzania na Japan ili kubadilishana uzoefu na kuainisha
fursa na maeneo ya kushirikiana kwa lengo la kuendeleza sekta hiyo na
ushirikiano wa nchi hizo mbili kwenye Nyanja ya TEHAMA.
Kwa
upande wake mwakilishi Mkuu wa JICA nchini Tanzania Bw. Toshio Nagase
akizungumza mara baada ya kufanyika kwa mazungumzo hayo amesema kuwa
Tanzania na Japan kwa miaka mingi zimekuwa na ushirikiano wa karibu
katika masuala mbalimbali.
Ameipongeza
Tanzania kwa kupiga hatua na kufanya vizuri katika matumizi ya TEHAMA
kwenye huduma za fedha kwa njia ya Simu na kubainisha kuwa Japan inayo
mengi ya kujifunza kupitia mafanikio haya.
Amesma
JICA imejipanga kusaidia awamu ya pili ya program zao nchini Tanzania
hususan kwenye Miundombinu, uwekezaji kwenye TEHAMA na masuala ya
kiufundi katika maeneo mbalimbali ambayo miradi ya ushirikiano
inatekelezwa.
Nagase
ameeleza kuwa Japan imejipanga kushirikiana kikamilifu katika masuala
ya TEHAMA hususan kuwawezesha vijana na wafanyabiashara wa Tanzania na
Japan kubadilishana uzoefu, ujuzi, ufundi katika masuala ya TEHAMA.
Amebainisha
kuwa Japan iko tayari kushirikiana na Sekta binafsi nchini Tanzania
kupitia biashara na uwekezaji kwenye makampuni yanayojishughulisha na
TEHAMA.
Comments
Post a Comment