SPIKA NDUGAI AFANYA MABADILIKO YA BAADHI YA WAJUMBE WA KAMATI ZA KUDUMU ZA BUNGE.
Na Benedict Liwenga-Maelezo.
Spika
wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Job Ndugai (Mb)
amefanya mabadiliko ya baadhi ya Wajumbe wa Kamati za Kudumu za Bunge
ili kuzingatia mahitaji mapya na changamoto zilizojitokeza baada ya
kuunda Kamati hizo mwezi Januari 2016.
Taarifa
hiyo imetolewa leo Jijini Dar es Salaam na Ofisi ya Bunge Kitengo cha
Habari, Elimu na Mawasiliano ambapo imeelezwa kuwa, mabadiliko hayo,
yamefanywa chini ya Kanuni ya 116(3) ya Kanuni za Kudumu za Bunge
inayompa Spika Mamlaka ya kuteua Wabunge kuunda Kamati Mbalimbali za
Bunge.
Taarifa
hiyo imeeleza kuwa, kufuatia mabadiliko hayo ambayo baadhi yake
yamehusu Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti au wote wawili, Kamati za Kudumu
za Bunge zilizoathirika na mabadiliko haya zitawajibika kufanya Uchaguzi
wa viongozi kwa mujibu wa kanuni ya 116 (10).
Baadhi
ya Kamati ambazo zimeathirika na mabadiliko hayo na ambazo zitawajibika
kufanya uchaguzi kwa viongozi ni zikiwemo; Kamati ya Ardhi, Maliasili
na Utalii ambayo itahitaji kupata Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti wapya,
Kamati ya Nishati na Madini ambayo itahitaji kupata Mwenyekiti mpya,
Kamati ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma itahitaji kupata Mwenyekiti mpya,
Kamati ya LAAC ambayo pia itahitaji kupata Makamu Mwenyekiti mpya na
Kamati ya Huduma na Maendeleo ya Jamii ambayo itahitaji kupata Makamu
Mwenyekiti mpya.
Aidha,
taarifa hiyo imeeleza pia mabadiliko hayo kwenye kamati zote yanaanza
mara moja ambapo orodha ya wajumbe waliobadilishwa imeshatolewa na Ofisi
hiyo na kusambazwa katika vyombo vya habari.
Comments
Post a Comment