SOKO LA FERI LATAKIWA KUTAFUTA GESI YA BEI NAFUU
Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa akielekea kwenye soko la samaki la Feri akitokea
ofisini kwake Magogoni jijini Dar es salaam kukagua hali ya soko hilo
Machi 22, 2016. Kushoto kwake ni Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Raymond Mushi.
Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa akikagua eneo la kukaangia samaki kwenye soko la
samaki Feri la jijini Dar es salaam Machi 22, 2016, Kushoto kwake ni
Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Raymond Mushi.
Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Mama Lishe wakati alipotembelea
soko la samaki la Feri jijini Dar es salaam Machi 22, 2016.
Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa akiwapungia Mama Lishe wakati alipotembelea soko
la samaki la Feri jijini Dar es salaam Machi 22, 2016.(Picha na Ofisi ya
Waziri Mkuu)
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameiagiza Bodi ya soko la Kimataifa la
Samaki la Feri, kukutana na makampuni mbalimbali yanayouza gesi ili
kupata kampuni inayouza kwa bei nafuu zaidi lengo likiwa ni kuwapunguzia
gharama wakaangaji wa samaki sokoni hapo.
Pia Waziri Mkuu Majaliwa alimtaka Meneja wa soko hilo, Bw. Solomon
Mushi kuhakikisha wanakuwa na kifaa maalumu cha kupimia ujazo wa mitungi
ya gesi sokoni hapo ili kubaini kama ni sahihi.
Ametoa agizo hilo leo mchana (Jumanne, Machi 22, 2016) wakati
alipofanya ziara ya ghafla katika Soko la Kimataifa la Samaki la Feri
iliyokuwa na lengo la kuangalia mfumo wa majiko ya gesi sokoni hapo
ambapo aliridhishwa na unavyofanya kazi.
Waziri Mkuu ambaye ametumia dakika 44 kulitembea soko hilo, alitoa
maagizo hayo baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa wafanyabiashara
ambao wamesema wamekuwa wakiuziwa gesi kwa bei kubwa ambayo imekuwa
ikiongezeka mara kwa mara.
Akizungumza kwa niaba ya wafanyabiashara hao, Bw. Ally Iddi amesema
awali walikuwa wanauziwa mtungi wa gesi wenye ujazo wa kilo 32 kwa sh.
70,000 na sasa umeongezeka hadi sh. 98,000 kiasi ambacho ni kikubwa
ukilinganisha na uzalishaji wao. “Nimeulizia kwenye baadhi ya maduka na
kukuta mtungi wenye ujazo kama huo unauzwa sh. 75,000,” alisema.
Kijana mwingine ambaye ni mkaangaji wa samaki, Bw. Mwanya Selemeni
alisema hivi sasa hali ya soko la feri ni nzuri tofauti na walivyokuwa
wakitumia kuni kwa sababu hakuna moshi. Alimuomba Waziri Mkuu ahakikishe
wanafikishiwa gesi ya kutoka Mtwara ili gharama ziweze kupungua.
Mfanyabiashara mwingine wa soko hilo, Bi. Mariam Samweli ambaye
alikuwa akiuza kuni na sasa yeye na wenzake wanataka kufanya biashara
nyingine lakini banda walilokuwa wakilitumia halina umeme licha ya kuwa
wameomba mara nyingi. “Tunaomba kupatiwa umeme ili tuweke vipepeo tuweze
kufanya biashara nyingine,” alisema.
Waziri Mkuu pia alitembelea eneo la mnada wa kuuza samaki sokoni hapo
ambako alielezwa matatizo ya umeme na uzibaji wa mitaro ya maji machafu
hali ambayo inatishia usalama wa afya zao.
“Kuna jipu la umeme hapa, tunachangishwa hela na kumpa mtu ambaye
hatumjui lakini hatujawahi kuona risiti, wao wanaweka umeme juu kwa juu
na umeme wenyewe wala haukai. Mita tunayo hapa lakini hata namba
hatujapewa,” alisema Bw. Omari Masoud kwa niaba ya wenzake.
Kuhusu tatizo la uzibaji mitaro na kutiririsha majitaka, kiongozi wa
mama lishe sokoni hapo, Bi. Fatma Ally aliomba watatuliwe tatizo hilo
ambalo limedumu kwa zaidi miezi miwili.
Akijibu kero zao, Waziri Mkuu alimwagiza Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Bw.
Raymond Mushi asimamie suala la kuweka umeme kwenye hilo banda pamoja
ahakikishe mama lishe wa soko hilo upande wa mnadani waanze kutumia
majiko ya gesi badala ya mkaa.
Kuhusu mitaro, alimwagiza meneja wa soko hilo, Bw. Solomon Mushi
aimarishe uzibuaji wa mitaro katika soko hilo. “ Mwambie mkandarasi
azibue mitaro kila siku jioni na watumiaji wa soko waache kutumia mifuko
ya plastiki kwa sababu inapoingia kule inaziba na wala haiozi,”
alisema.
Aliwataka wafanyabiashara waimarishe usafi kwa sababu ni sehemu ya
chakula. “Lengo letu ni kufanya soko hili liwe kwenye viwango vya
kimataiafa ili mteja anapokuja kununua samaki wabichi ama wa kukaanga
awe na chaguo,” alisema.
Kwa upande wake, Meneja wa soko hilo, Bw. Mushi alisema bodi ya soko
hilo ambayo imeundwa hivi karibuni itakutana kesho kwa mara ya kwanza na
miongoni mwa mambo yatakayojadiliwa ni maelekezo yaliyotolewa na Waziri
Mkuu.
IMETOLEWA NA: OFISI YA WAZIRI MKUU
2 MTAA WA MAGOGONI,
L. P. 3021,
11410 DAR ES SALAAM
JUMANNE, MACHI 22, 2016
Comments
Post a Comment