Siri Imefichuka...CUF Watoa Sababu za Maalim Seif Sharif Hamad Kuishi Serena Hoteli Pamoja na Gharama Iliyotumika Hadi sasa
SIRI
imefichuka kuhusu hatua ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya
Umoja wa Kitaifa ya Zanzibar (SUK), Maalim Seif Sharif Hamad, kuishi
hotelini jijini Dar es Salaam.
Maalim
Seif ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), amekuwa
akiishi katika Hoteli ya Serena jijini Dar tangu aliporuhusiwa kutoka
Hospitali ya Hindu Mandal Machi 8, mwaka huu alipokuwa amelazwa kwa
matibabu.
Akizungumza
jijini Dar es Salaam jana, mmoja wa ofisa wa ngazi za juu wa CUF,
alishangazwa na hatua ya baadhi ya watu kuhoji kiongozi huyo kuendelea
kuishi hotelini hapo.
Alisema
hatua ya kiongozi huyo kuishi hotelini ni matokeo ya Serikali ya
Mapinduzi Zanzibar (SMZ), kushindwa kutekeleza ahadi ya kumpa nyumba
pindi anapokuwa Dar es Salaam katika shughuli zake.
Alisema
kutokana na hali hiyo imekuwa ni utaratibu kwa kiongozi huyo kufikia
katika hoteli hiyo na gharama za kuishi hotelini hapo hulipwa na SMZ kwa
mujibu wa sheria.
“Tangu
mwaka 2010 Maalim aliahidiwa atapewa nyumba na Serikali ya SMZ lakini
hilo halijafanyika, hiyo nyumba hajapewa hadi leo ndiyo maana mara zote
akija Dar hufikia hotelini.
“SMZ
ndiyo wenye jukumu la kulipa na si vinginevyo, kwani hata kama kama
kuna viongozi wa SMZ wamepewa nyumba kwa muda wote, lakini Maalim Seif
hajapewa, sasa kama unataka kujua kwa undani unaweza kuwauliza viongozi
wa Serikali wao ndiyo wenye majibu zaidi,” alisema ofisa huyo ambaye
hakutaka jina lake liandikwe
Gharama zilizotumika kwa siku 7
Kwa
mujibu wa chumba anachoishi kiongozi huyo chenye hadhi ya rais ambacho
hutozwa kwa Dola za Marekani 2,801.50, ambapo dola moja ni sawa na Sh
2,180. Hivyo kwa siku saba hadi kufikia leo Serikali imemlipia Maalim
Seif, Sh milioni 42.946.
Kauli ya CUF
Alipotafutwa
Kaimu Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Mawasiliano ya Umma wa CUF, Hamad
Masoud Hamad, alisema hatua ya Maalim Seif kuishi hotelini inatokana na
maagizo ya daktari wake ambaye amemtaka apumzike kwa sasa.
Alisema
kutokana na hali hiyo baada ya kuruhusiwa kutoka hospitali alipokuwa
akipatiwa matibabu alikwenda katika Hoteli ya Serena anapofikia kila
mara anapokuwa jijini Dar es Salaam.
Alipoulizwa
ni nani anayelipa gharama za kuishi hotelini hapo, Hamad alisema
wanaoweza kuzungumzia suala hilo ni viongozi wa SMZ.
“Magufuli
(Rais), alipokwenda kumwona alimuuliza ni nani anayemlipia gharama za
hoteli na Maalim alisema wazi ni SMZ, lakini ninachotaka kuwaambia
Maalim Seif hana nyumba Dar es Salaam.
“…
kama wapo viongozi waliopewa nyumba wa SMZ ni hao lakini si Maalim
Seif, tangu mwaka 2010 hana nyumba na hufikia hotelini, hana nyumba ya
Serikali wala yake binafsi,” alisema Hamad.
SMZ wazungumza
Alipotafutwa
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa pili wa Rais wa Zanzibar, Mohamed
Aboud ili kupata ufafanuzi wa suala hilo, alisema Maalim Seif anastahiki
zake kama kiongozi wa SMZ ikiwemo kupatiwa haki ya matibabu pamoja na
mahala pa kuishi.
“SMZ
ni wajibu wake kuwahudumia viongozi na wananchi wake kwa ujumla, Maalim
Seif bado ni Makamu wa Kwanza wa Rais hivyo ana wajibu wa kuhudumiwa.
“Na
katika hili anahudumiwa na SMZ ikiwemo kulipiwa hoteli pindi awapo nje
ya Zanzibar na si hilo tu pia tunahusika kumpa stahiki zake zote ikiwemo
matibabu.
“Kwa
kawaida pindi kiongozi yoyote wa kitaifa anapokuwa Dar es Salaam na
kama hana nyumba SMZ hulipa malazi ya kiongozi wake na Maalim bado ni
kiongozi na hata kama akiondoka kwenye uongozi bado anazo stahiki zake
ikiwemo kuhudumiwa kama kiongozi mstaafu,” alisema Waziri Aboud.
Alisema
pamoja na hali hiyo kwa sasa Serikali ya Muungano ndiyo inayolipa
gharama za Maalim Seif kuishi hotelini kwa agizo la Rais Dk. John
Magufuli.
Alisema
ahadi ya Rais Magufuli ya kusaidia kulipia hoteli anayoishi Maalim Seif
inaonesha ni namna gani Serikali zote mbili ya Muungano na ile ya
Zanzibar zinavyoshirikiana kwa dhati.
“Kwa
ubinadamu wake Rais Magufuli tunamshukuru sana kwani inaonesha namna
gani kiongozi huyo wa Jamhuri ya Muungano alivyo na mapenzi mema na
Zanzibar pamoja na viongozi wake.
“…
ila pamoja na yote SMZ bado ina wajibu wa kutekeleza wajibu wake wa
kuwatunza viongozi wake wote wakiwemo waliokuwa ndani ya Serikali pamoja
na wale waliostaafu,” alisema Aboud
Comments
Post a Comment