RAIS MAGUFULI AWATAKA WATANZANIA KUJIFUNZA KUTOKA KWA VIETNAM
Na. Lilian Lundo - Maelezo
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli amewataka
watanzania kujifunza kutoka kwa Vietnam namna ambavyo wameweza kupambana
na umaskini kwa muda mfupi.
Mhe.
Rais aliyasema hayo leo Ikulu katika ziara ya Rais wa Jamhuri ya
Kisoshalisti ya Vietnam Mhe. Truong Tan Sang baada ya kusaini mkataba wa
kukuza uhusiano baina ya Tanzania na Vietnam.
“Tanzania
tunatakiwa tujifunze mambo mengi kutoka kwa wenzetu Vietnam ambao
walipata uhuru mwaka 1945 wakaingia kwenye mapigano mpaka mwaka 1976.
Wakati huo pato la muvietnam mmoja lilikuwa dola 100 lakini leo ni dola
2000 na wamepunguza umaskini kwa asilimia 50 kuifanya nchi hiyo kuwa ya
kipato cha kati,” alisema Mhe. Rais
Mhe.
Rais Magufuli aliongezea kuwa, mwaka 1976 Vietnam ilichukua mbegu ya
korosho kutoka Tanzania na kwenda kulima kwao, zao hilo limekuwa
likifanya vizuri kwa nchi yao na wanaongoza kwa kulima korosho Duniani.
Kwa upande wa Tanzania zao hilo limekuwa likitelemka chini kila mwaka.
Vilevile,
Mhe Rais alisema kuwa Vietnam ni nchi inayoongoza kwa uzalishaji wa
samaki lakini Tanzania ambayo ina maziwa 21 pamoja na mito na bahari
kila mahali haijaweza kuifikia Vietnam kwa uzalishaji wa samaki hivyo
lazima watanzania tujifunze na tusiogope kujifunza ili Tanzania itoke
mahali iliko.
Aidha
Mhe. Rais alisema ziara ya Vietnam imekuja wakati muafaka wa kujenga
mahusiano mazuri kwa watanzania na nchi ya Vietnam lakini hasa katika
uchumi ili Tanzania iweze kufanikiwa namna ambavyo wao wamefanikiwa.
Kwa
upande wake, Mhe. Rais Truong alimshukuru Rais Magufuli na watanzania
kwa mapokezi mazuri na ameahidi kuimarisha mahusiano ya nchi hizi mbili
hasa katika sekta ya kilimo, biashara, mawasiliano pamoja na uwekezaji.
Mhe.
Rais Truong Tan Sang ni Rais wa kwanza wa nchi ya Jamhuri ya
Kisoshalisti ya Vietnam kufanya ziara nchini Tanzania. Rais huyo
ameambatana na mawaziri wanne pamoja na wafanyabiashara wapatao 30.
Mahusiano
ya Tanzania na Vietnam yalijengwa na Baba wa Taifa Mwalimu Julius
Kambarage Nyerere na Kiongozi wa Vietnam, Ho Chi Minh kuanzia mwaka 1960
na kupelekea kuanzishwa rasmi kwa mahusiano ya kidiplomasia mwaka 1965.
Comments
Post a Comment