RAIS MAGUFULI AKUTANA NA KUFANYA MAZUNGUMZO NA RAIS KENYATTA NA RAIS KAGAME
Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika
Mashariki Dkt. John Pombe Magufuli akiagana na Rais wa Rwanda Paul
Kagame mara baada ya kumaliza mazungumzo yaliyofanyika Ngurdoto nje
kidogo ya jiji la Arusha.
Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amefanya
mazungumzo na Rais wa Jamhuri ya Kenya Mheshimiwa Uhuru Kenyatta, kando
ya Mkutano Mkuu wa 17 wa kawaida wa wakuu wa nchi wanachama wa Jumuiya
ya Afrika Mashariki unaofanyika Mkoani Arusha, ambapo viongozi hao
wamekubaliana kuimarisha mahusiano hususani katika masuala ya kiuchumi.
Baadhi ya
maeneo waliyokubaliana kutilia mkazo katika mahusiano hayo, ni pamoja
na kutekeleza miradi ya maendeleo inayounganisha nchi mbili ikiwemo
ujenzi wa miundombinu, kukuza biashara na kuzalisha ajira kupitia
viwanda.Rais Uhuru Kenyatta amesema amefurahishwa sana kuona Rais
Magufuli yupo tayari kuhakikisha nchi ya Kenya na Tanzania zinakuwa
karibu, na miradi ya maendeleo inaharakishwa.
"Kwa
sababu nia yetu sisi ni kuona maendeleo ambayo yatagusa mwananchi wa
kawaida, tumalize umasikini, uchumi ukue, na hivyo hatuwezi kufanya
tukiwa tumetengana" Amesisitiza Rais Kenyatta.
Kwa
upande wake Rais John Pombe Magufuli, amesema Tanzania na Kenya zina
kila sababu ya kuimarisha mahusiano ya kibiashara hasa katika ujenzi wa
viwanda utakaozalisha ajira kwa kuwa watu wake ni wamoja.
"Wazee
wetu Mzee Kenyatta na Mzee Nyerere walijenga mazingira mazuri ya kuwa na
nchi hizi mbili wakati wakipigania uhuru, sasa sisi vijana wao ni
wakati wetu kwenda mbele kwa ajili ya maendeleo" amebainisha Rais
Magufuli.Dkt. Magufuli amebainisha kuwa nchi wanachama wa Jumuiya ya
Afrika Mashariki zinajenga mahusiano na ushirikiano zinalenga kupata
manufaa hayo ya kiuchumi kwa manufaa ya wananchi wake.
Ameutaja
mradi mmojawapo kuwa ni ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme kutoka
Tanzania kwenda nchini Kenya kupitia Namanga, na akaongeza kuwa Tanzania
itakapoongeza uzalishaji wa umeme na kuanza kuvuna gesi, itaiuzia pia
Kenya, halikadhalika Kenya nayo itauza bidhaa zake Tanzania.
Kabla ya
kukutana na Rais Kenyatta, Rais Magufuli amekutana na kufanya mazungumzo
na Rais wa Jamhuri ya Rwanda Mheshimiwa Paul Kagame, ambapo viongozi
hao wamekubaliana kuzidisha mahusiano kati ya Tanzania na Rwanda ambapo
Rais Magufuli amemhakikishia kuwa serikali yake itakamilisha ujenzi wa
Reli ya kati kwa kiwango cha kisasa yaani "Standard Gauge" ili kurahisha
usafirishaji wa bidhaa na watu.
Rais
Kagame amempongeza Rais Magufuli kwa uongozi wake bora uliolenga
kuimarisha uchumi, ikiwemo kuimarisha bandari ya Dar es salaam ambayo
Rwanda inaitegemea na ujenzi wa Reli ya Kati ambayo pia ni tegemeo kubwa
kwa uchumi wa Rwanda
Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiano, IKULU
Arusha
02 Machi, 2016
Comments
Post a Comment